By RHOBI CHACHA
HATIMAYE taarifa ikufikie kwamba, mwanamitindo Hamisa Mobetto leo Jumamosi, Februari 15, 2025, amelipiwa mahari ya ng'ombe 30 na Stephanie Azizi Ki ambaye ni kiungo mshambuliaji ya Yanga, huku mipango kabambe ya ndoa ikiendelea.
Mahari hiyo imekabidhiwa na Injinia Hersi Said, kwa niaba ya baba mzazi wa Aziz Ki, ambapo nyota huyo wa Yanga aliongozana na baadhi ya wachezaji wenzake kama Pacome Zouzoua, Bakar Mwamnyeto, Yao Kouassi na wengine sambamba na maofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe na Priva.
Kwa upande wa Hamisa aliingia ukumbini na meneja wake Paul Mangoma huku warembo 15 wakitangulia mbele wakiwa wamevaa sare huku wakicheza.
Hamisa ameliambia Mwanaspoti, anamshukuru Mungu kumpata mtu anayeona ndiye anamfaa katika maisha yake na tayari sasa ni mchumba rasmi wa mtu, tena kijana anayempenda kwa dhati.
“Sasa hapa ndio nimefika kwa kuwa nimekutana na mtu mwenye mapenzi ya kweli kwangu. Pia nafsi zetu zimeendana, hapa namuomba Mungu anyooshe mambo yaende kama vile tulivyopanga,” amesema Hamisa.
Kwa upande wake, Azizi Ki alisema anaamini safari yake ya muda mrefu imefika kwa kuwa amempata mwanamke anayempenda kutoka ndani ya uvungu wa moyo wake na kwa upande wake taratibu zote za uchumba amemaliza, anasubiri ndoa watakayofunga hivi karibuni.
Katika utoaji wa mahari hiyo mastaa kibao walikuwepo kuhudhuria sherehe hiyo jambo ambalo ni hatua mpya kuelekea ndoa yao inayotarajiwa kufanyika Februari 16 na sherehe ni Februari 19 kwenye ukumbi wa Superdome Masaki Jijini Dar es Salaam.
Hamisa ni mama wa watoto wawili, amezaa na wanaume wawili tofauti. Na inadaiwa mtoto wa kike amezaa na Mkurugenzi wa EFM Francis Majizo na wa kiume supastaa wa Tanzania Diamond Platnumz .

Leave a Reply