Mahakama yampa siku 21 Mwijaku kuwasilisha utetezi dhidi ya Kipanya

Mahakama yampa siku 21 Mwijaku kuwasilisha utetezi dhidi ya Kipanya

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imetoa siku 21 kwa mtangazaji wa Crown Media, Burton Mwemba Mwijaku kuwasilisha utetezi wake mahakamani hapo.

Mwijaku amefunguliwa kesi ya madai na mchora katuni maarufu, Ally Masoud Nyomwa akitakiwa kumlipa Masoud Sh5.5 bilioni kwa madai ya kumkashifu kupitia mtandao wa kijamii.

Hata hivyo, Mwijaku kupitia wakili wake, Patrick Maleo ameiomba Mahakama hiyo imuongezee muda ili aweze kuwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi kujibu madai ya Kipanya. Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji David Nguyale anayesikiliza kesi hiyo.

Jaji Nguyale alitoa maelekezo hayo, wakati shauri hili lilipotajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, baada ya waleta maombi kudai kuwa hawajapatiwa majibu na Mwijaku.

Masoud amefungua kesi hiyo ya madai namba 18911 ya mwaka 2024, Agosti 5, 2024 akiomba nafuu 12 ikiwemo kulipwa fidia kwa kukashifiwa mtandaoni na Mwijaku.

Katika nafuu hizo 12, Masoud ambaye ni mtangazaji wa Clouds Media anaomba alipwe fidia ya Sh 5.5 bilioni kutoka kwa Mwijaku kwa madai ya kumshushia hadhi na heshima kupitia mitandao ya kijamii.

Leo, Masoud kupitia wakili wake kutoka kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba alidai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa lakini hawajapatiwa majibu na mjibu maombi.

Wakili Komba baada ya kueleza hayo, wakili wa Mwijaku, Patrick Maleo alidai kuwa mteja wake amechelewa kuleta majibu kwa sababu alikosa wakili.

"Ni kweli mteja wangu alipokea wito wa madai na kwa kuwa alikuwa hajapata wakili, akachelewa muda wa kuwasilisha majibu," amedai Wakili Patrick na kuongeza:

"Baadaye amenitafuta mimi, hivyo naomba niongezewe muda wa kuwasilisha majibu ya utetezi, halafu Mahakama iendelee na utaratibu mwingine."

Wakili Patrick baada ya kueleza hayo, Jaji Ngunyale alimuuliza wakili Komba iwapo ana kitu cha kuongea kuhusiana na majibu ya wakili wa Mwijaku, ambapo alidai hana pingamizi juu ya kuongezewa muda kwa mjibu madai.

Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili alitoa siku 21 Mwijaku awe amewasilisha majibu yake mahakamani na kuwapatia waleta maombi katika shauri hilo.

"Mahakama inakupa siku 21 kuanzia leo, uwe umewasilisha majibu ya utetezi na uwe umewapatia pia nakala upande wa pili.

"Na kesi hii naiahirisha hadi Septemba 24, 2024 kwa ajili ya kupanga utaratibu mwingine wa usikilizwaji," amesema Jaji Ngunyale na kisha kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 24.

Hata hivyo, mleta maombi (Kipanya) na mjibu maombi (Mwijaku) hawakuwepo mahakamani hapo wakati shauri hilo lilipotajwa, badala yake waliwakilishwa na mawakili wao.

Katika kesi ya msingi, Masoud amemshtaki Mwijaku kwa kumkashifu kwa maandishi Juni 4, 2024 kupitia ukurasa wake wa Facebook wenye utambulisho namba 108657908847651 na kwenye akaunti yake ya Instagram aliandika maneno ya uongo yenye nia ovu na kumfedhehesha yakiwemo kwamba yeye KP anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.

Katika hati hiyo ya mashtaka, Mwijaku anadaiwa kuandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba Masoud huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na Serikali hususani marais kwa kuhongwa.

Kipanya anadai kuwa maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochampishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii na duniani yametafsiri kwamba yeye KP sio mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za Serikali au magendo.

“Hivyo kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na sio uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya kijamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa,” ilidai sehemu ya hati ya mashtaka.

Kutokana na maneno aliyotoa Mwijaku kwenye mitandao ya kijamii, wakili Komba ameyachambua katika vipengele 15 akifafanua maana ya maandishi ya Mwijaku kwa tafsiri ya watu wa kawaida ndani ya jamii kwamba mteja wake anaonekana ni mla rushwa, jambazi, tapeli, laghai, asiyeaminika, chanzo cha vijana walioharibikiwa maisha.

Pia, mteja wake hapaswi kuhusishwa katika masuala yoyote ya kijamii ikiwemo kupewa fursa na kufanya kazi na taasisi za Serikali ambazo amekuwa akijihusisha nazo katika elimu na malezi ya vijana shuleni na mitaani.

Katika maombi 12 aliyoomba Kipanya dhidi ya Mwijaku ikiwemo kulipwa fidia za jumla ya Sh5.5 bilioni, Wakili Komba anadai kuwa:"Kutokana na maandishi ya kashfa ya meneno ya uongo aliyotoa Mwijaku na kunukuliwa akikiri na kuomba radhi mbele ya vyombo vya habari Juni 13, 2024 bila kuchukua hatua ya dhati ya kumsafisha kimaandishi Masoud Kipaya, imemuathiri kiajira, kibiashara, kimahusiano ndani ya jamii ya Tanzania kuanzia kwenye familia yake, kisaikolojia na kumshushia hadhi na hesima aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 35.

“Hivyo mteja wangu anaomba Mahakama imuamuru Mwijaku amlipe fidia ya Sh500 milioni ya madhara halisi (specific damages) atakayothibitisha kwa ushahidi mahakamani kutokana na kashfa hiyo na fidia ya madhara ya jumla (general damages) yatakayopimwa na kuridhiwa na Mahakama kwa mamlaka yake ya Sh5 bilioni.”

Pia, Wakili Komba amedai kuwa mteja wake ameomba malipo ya kiadhabu kwa mdaiwa yaani 'punitive damages na malipo ya fidia ya madhara halisi yaambatane na riba ya asilimia 31 tangu kashfa ilipotolewa yaani Juni 4, 2024 hadi utekelezaji wa hukumu utakapokamilika.

Vilevile Kipanya anaiomba Mahakama katika hukumu yake itamke kwamba maneno yaliyoandikwa na kusambazwa na Mwijaku yalikuwa ni ya uongo, yenye nia ovu na kuharibu hadhi na heshima yake.

Kipanya anaiomba Mahakama iamuru Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandikwa na kusambazwa.

Lakini pia, Kipanya anaiomba Mahakama itamke na kumuamuru Mwijaku, wakala wake, wasaidizi wake na mtu mwingine yeyote aliye katika mamlaka yake kutosambaza maneno hayo ya uongo na kashfa dhidi ya Masoud Kipaya.

Mbali na maombi hayo, Kipanya pia ameomba kulipwa gharama ya kesi kutokana na kuajiri mawakili na nafuu nyingine ambazo Mahakama itaona ni haki na zinafaa apewe.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags