Mwandaaji wa shindano la Bongo Star Search (BSS), Rita Paulsen amesema kinachokwamisha washindi wengi wa shindano hilo la kusaka vipaji ni kutotumia pesa walizoshinda kuwekeza kwenye muziki.
Akizungumza na Mwananchi Scoop Rita amesema mara nyingi washiriki wanaoshinda hutumia pesa hizo kuwapa wazazi, kujenga nyumba na kunuua magari.
"Sisi hawa tunawapa hela zao tunampa zote anazichukua haziweki kwenye muziki wazazi wanachukua wengine au anaenda kujenga nyumba, ananunua gari lakini tungekuwa tunawaambia zawadi zao ni hizi watumie kwenye studio na tunatamani kufanya hivyo. Lakini show ikiisha mtu anataka kusikia stori nyingine anataka pesa yake 'cash'.
"Wao kutofanya vizuri hakutufanyi sisi 'brand' yetu ikae sawa, wanaonekana watu hawatoki labda hawalipwi ukweli hela wanalipwa lakini hawapeleki kwenye muziki wanapeleka kwenye vitu vingine kabisa,"amesema
Hata hivyo Rita hakuishia hapo aliendelea kwa kudai washiriki hao kabla ya kushinda hupatiwa elimu ya saikolojia kwa ajili ya kutochanganywa na pesa hizo lakini inaonekana bado haiwasaidii.
"Wanapata presha kutoka kwa ndugu na familia wazazi wanakujaga kudai, tunawapa elimu lakini akishinda anakuwa mtu mwingine siyo yule aliyepewa elimu kwa saababu anajua anashinikizwa, ghafla anakuwa kitu kingine.
"Wazazi wengine wanatoa akaunti zao wanasema tuma huku, hawajui kwamba wakishatoa hizo hazirudi na wanakuwa hawajawekeza chochote kwenye muziki. Kikubwa sisi tunawapa pesa zao na kama hajapewa tunawakilisha kwa BASATA,"amesema
Utakumbuka kuwa shindano hilo la kusaka vipaji tayari limetoa wasanii kama vile Phina, Peter Msechu, Frida Aman, Kayumba na wengine wengi
Leave a Reply