Madaktari waonya matumizi dawa za maji za kikohozi kwa watoto

Madaktari Waonya Matumizi Dawa Za Maji Za Kikohozi Kwa Watoto

Nilianza safari kuelekea Dodoma kwenda kumjulia hali rafiki yangu aliyekuwa akisoma katka moja ya chuo kikuu kikubwa na maarufu hapa nchini.

Licha ya kwenda kumjulia hali lakini lengo lingine la safari ile ni kumuona mtoto aliyejifungua wakati akiendelea na masomo yake  chuoni hapo ambaye aliiugua ghafla wakati wa malezi.

Nilipofika Anna (sio jina halisi) alinipokea na kunikaribisha na mara baada ya kuoga na kupata chakula cha jioni tulianza kupiga stori na hatimaye kunieleza chanzo za mtoto wake kuugua.

Anasema aliamka asubuhi na kuona mtoto anakohoa kutokana na hali hiyo alishindwa kwenda chuo badala yake alikwenda kwenye duka la dawa kutafuta dawa za maji za kikohozi na kumpatia bila kumpeleka hospitali.

Anaendelea kufunguka na kusema alimpatia dawa hiyo mtoto wake lakini wala hakupata nafuu mpaka alipompeleka hospitali na kuelezwa alifanya makosa kumpatia dawa mtoto bila kumpeleka hospitali.

Niliposikia hayo nilisikitika sana na nikajua ndio tatizo linalowakumba wasichana wengi waliomaliza chuo au waliopo chuoni wanaoamua kuzaa.

Hatua hiyo ilinifanya niliporejea Dar es Salaam nikaamua kukutana na madaktari bingwa wa watoto ambao ni Namala Mkopi, Francis Furia, Kiva Mvungi, Theopista Jacob ambao walizungumza kwa niaba ya Chama cha Madaktari bingwa wa Watoto Tanzania (PAT).

Pamoja na mambo mengi madaktari hao wametoa tahadhari juu ya matumzi hayo ya dawa za maji za kikohozi kwa watoto chini ya miaka mitano bila kumpeleka kwa wataalamu wa afya ila kufahamu tatizo kiundani.

Wanasema kuwa kukohoa ni njia moja wapo ya mwili kulinda njia ya hewa, na hivyo mtu anapokohoa huondoa au kuzuia uchafu ambao ungeenda kwenye mapafu.

Wanasema mara nyingi kikohozi kwa watoto husababishwa na maambukizi ya virusi, na huambatana na homa, pua kuziba na mafua.

“Watoto wengi wanaokwenda shule hupata haya maambukizi mara kwa mara,” wanasema madaktari hao

Wanasema Shirika la Afya duniani (WHO) linazuia matumizi ya dawa za kikohozi kwa watoto wenye umri mdogo. Sababu ya zuio hili ni madhara ya hizo dawa ambayo ni pamoja na kulegea, kutapika pamoja na kuharibu meno. 

Hata hivyo madaktari hao wanasema hakuna ushahidi wa kitafiti kuonyesha dawa hizo zinasaidia kwa kikohozi zaidi sana ni kumzuia mtoto asitoe uchafu na majimaji yanayoingia kwenye mfumo wa hewa. 

“Ikumbukwe baadhi ya dawa hizi zinazuia kikohozi na siyo kutibu kilichosababisha kikohozi.Utafiti uliofanyika nchini Kenya umeonyesha dawa hizi hutumika kwa watoto wachanga, kitu ambacho ni hatari.

“Pia utafiti huo ulionyesha uwepo wa mchanganyiko wa dawa mbalimbali zilizowekwa katika chupa moja (mixture of different drugs in the syrup), hili huongeza uwezekano wa kupata madhara zaidi kwa mtoto anayepewa,” wanasema madaktari hao.

Watoa ushauri

Wanasema iwapo mtoto wako ana kikohozi, unachotakiwa ni kumpeleke hospitali iliyo karibu ili wataalamu wa afya wamchunguze na kutambua iwapo ana maambukizi kwenye mapafu ama la.

Pia wanasema wataalamu wa afya watamchungua ili kujua kama ana peumonia na atahitaji kupatiwa dawa za kuua bakteria.

“Kufika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi wa afya ya mtoto wako ni muhimu sana, kuliko kwenda tu katika duka la madawa na kuchukua dawa bila ya kupata ushauri kutoka kwa daktar.

“Ndio maana tunaendelea kusisitiza kuwa mtoto anapoumwa ni muhimu kumpeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi,” wanasema madaktari hao

Aidha madaktari hao wanashauri kuwa mtoto anayekohoa na ana mafua mzazi au mlezi anashauriwa kumpa vimiminika kwa wingi na vitulizo vya kukohoa mfano, asali kwa watoto wenye umri zaidi ya mwaka mmoja.

“Kama hana peumonia anaweza kuwa na maambukizi ya virusi yanayoambatana na mafua na homa. Hahitaji kutumia dawa za kikohozi, mtoto anayekohoa na ana mafua unashauriwa kumpa vimiminika kwa wingi na vitulizo vya kukohoa mfano asali kwa watoto wenye umri zaidi ya mwaka mmoja.

“Pia unaweza kumpatia maji ya limao (lemonade, lemon tea) hata tangawizi,” wanasema madaktari hao.

Hata hivyo wanasema wazazi wanapaswa kukumbuka kuwa kikohozi kinasaidia kukinga njia ya hewa, hivyo wasiwe na wasiwasi kama mtoto anakohoa. 

Wanasema pia kikohozi siyo ugonjwa ni dalili tu, hivyo ni muhimu kumpeleka kwa wataalamu wa afya ili kupata ushauri na kutambua chanzo na namna bora ya matibabu na kusisitiza kuwa  kikohozi sio ugonjwa bali ni dalili. 

Makala hii imekuja ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wasichana hata wazazi ambao maa nyingi wamekua wakijisahau na kuwapatia watoto wao dawa bila ya kwenda hospitali ili kupata ushauri wa mtaalam.

Tatizo hilo limesababisha watoto wengi kupoteza maisha na wengine kuwa na afya duni hiyo ni kutokana na wazazi wao kushindwa kwenda hospitali kupata tiba na kuamini duka la dawa pekee.

Tunatambua kuwa wapo wanafunzi wa vyuo ambao wameolewa na wengine wana watoto unaposoma Makala hii basi ikubadilishe na kukumbusha daima unapaswa kumpeleka mtoto hospitali pindi tu anapougua au kuona dalili mbaya dhidi yake.
Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Janeth Jovin

A writer, reporter, presenter and news anchor for Mwananchi Scoop. Her writings are based on business, money management on Tuesday and health on Thursday on Mwananchi Scoop. Her famous segments on Mwananchi Scoop include KARIA and FASHION.

Latest Post