Lula Da Silva ashinda tena urais Brazil

Lula Da Silva ashinda tena urais Brazil

Rais wa zamani wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva ameshinda duru ya pili ya uchaguzi baada ya kumuangusha mpinzani wake Jair Bolsonaro na kutoa mwito wa amani na umoja baada ya kampeni kali za uchaguzi huo.

Mwanasiasa huyo wa mlango wa kushoto anayetambulika zaidi kwa jina la Lula amembwaga Bolsonaro kwa ushindi mwembamba wa asilimia 50.9 dhidi ya asilimia 49.17 za Bolsonaro. 

Lula amesema kwenye hotuba yake baada ya ushindi huo mjini Sao Paulo kwamba mshindi ndio chaguo la watu wa Brazil. Akasema ushindi huo si wake pekee yake ama chama chake cha Wafanyakazi bali ni ushindi wa vuguvugu la demokrasia iliyoko juu ya vyama vya siasa na maslahi binafsi na itikadi.

"Ninajiona kama raia wa Brazil ambaye anakabiliwa na mzigo wa kuzijenga upya siasa za Brazil kwa sababu wapinzani wangu walijaribu kunizika nikiwa mzima. Na leo niko hapa, niko hapa kuitawala nchi na kuitoa kwenye hali ngumu sana. Lakini nina imani kwamba kwa msaada wa watu tutapata suluhu ya kuliondoa taifa hapa lilipo na kurejea kwenye demokrasia na amani ili tuweze kuwasaidia wazazi wetu, familia na kuujenga ulimwengu ambao watu wa Brazil wanautaka,” alisema Lula da Silva.   

Lula aidha alitoa wito wa amani na umoja na kuapa kupambana na njaa na kuulinda msitu wa mvua wa Amazon katika utawala wake, bila kuweka kando mikakati ya kurejesha sera muhimu za kiuchumi na kuboresha hali ya maisha.

Rais wa Marekani Joe Biden na Emmanuel Macron wa Ufaransa pamoja na viongozi wengine ulimwenguni wamempongeza Lula kwa ushindi huo. Mkuu wa mahusiano ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell pia amempongeza Lula na hasa mahakama ya juu ya uchaguzi nchini Brazil kwa kutekeleza mamlaka yake ya kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa haki na uwazi.

Kabla ya kuingia kwenye siasa, Lula alikuwa kiongozi wa vyama vya wafanyakazi na kwa mara ya kwanza aliiongoza Brazil kati ya mwaka 2003 hadi 2010. 

Kurejea kwake kunaashiria kishindo cha kiongozi huyo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela mwezi Julai, 2017 kufuatia madai kadhaa ya ufisadi na utakatishaji fedha na kifungo hicho kilimzuia kushiriki kwa namna yoyote kwenye uchaguzi wa mwaka 2018 dhidi ya Bolsonaro.

Ushindi wa mrengo wa kushoto unaifanya Brazil kujiunga kwenye wimbi la kuibuka kwa serikali za mrengo huo lililoanza miaka ya 2000 kuanzia enzi ya Hugo Chavez wa Venezuela na Evo Morales wa Bolivia.

Rais wa Colombia Gustavo Petro alimpongeza Lula kupitia twitter huku Rais wa Bolivia Luis Arce akimpongeza na kusema ushindi wa Lula utaimarisha demokrasia na utangamano ndani ya Amerika ya Kusini. Rais wa Venezuela Nicolas Maduro aliandika demokrasia imeshinda leo.

Bolsonaro anakuwa Rais wa kwanza wa Brazil ambaye hakufanikiwa kushinda kwenye duru ya pili ya uchaguzi tangu taifa hilo liliporejea kwenye demokrasia mwaka 1985 na bado hajasema chochote iwapo atakubali ama kuyakataa matokeo hayo.

Haipo wazi iwapo Bolsonaro atakayakubali matokeo ama la kwa kuwa huko nyuma aliwahi kunukuliwa akisema hatayakubali matokeo iwapo atashindwa kutokana na udanganyifu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags