Kwenda na fashion kunavyowaponza baadhi ya wavaaji

Kwenda na fashion kunavyowaponza baadhi ya wavaaji

 

Imekuwa ni desturi kwa baadhi ya watu kununua bidhaa fulani kutokana na kutangazwa sana. Matangazo hayo huwaweka katika ushawishi wa kutaka kununua bidhaa hiyo ili kujithibitishia kile kilichokuwa kikielezwa katika tangazo juu ya bidhaa hiyo. 

Hali hiyo pia hujitokeza hata katika masuala ya mavazi ambapo baadhi ya watu hujikuta katika mkumbo wa kununua nguo ambazo ameziona kwenye tangazo, au ameona msanii fulani amevaa, bila ya kujua kuwa kuna utofauti mkubwa kati ya nguo ya kwenye tangazo na nguo halisi.

Akizungumza na Mwananchi Scoop, mtaalamu wa masuala ya urembo na mavazi Aisha Mtawa alisema tabia hiyo imekuwa ikiwapelekea baadhi ya watu kununua nguo au viatu ambavyo baadae wanashindwa kuvaa.

Alisema kabla ya kufikiria kununua au kushona nguo inayotrend kwa wakati fulani ni vyema kwanza kujiuliza kama nguo hiyo inaendana na mwili wako, ambapo alitolea mfano kuwa kuna baadhi ya mitindo akivaa mtu mnene anapendeza zaidi kuliko anapovaa mtu mwembamba. 

Pia aligusia baadhi ya watu wanaopenda kununua nguo kwa sababu ya kuona mtu fulani amevaa, alishauri watu hao kuacha tabia ya kuparamia kununua mavazi ya aina fulani kwa kuwa amemuona fulani amevaa na amependeza kwani yawezekana huyo uliyemuona amevaa mwili wake hauendani na wewe.

"Usivae nguo kwa sababu tu umeona fulani amevaa bali vaa nguo inayoendana na mwili wako," anasema.

Anasema kutozingatia hilo kunaweza kusababisha mtu kutumia kiasi kikubwa cha fedha kugharamia kununua nguo ambayo atashindwa kuivaa.

 “Ni muhimu kuzingatia suala la muonekano wa mwili na kuacha kufuata mkumbo katika suala la uchaguaji wa mavazi,” anasema. 

Naye Mwanahamisi Juma ambaye ni mfanyabiashara mitandaoni alifunguka kwa kueleza kuwa wapo baadhi ya wateja wanarudisha nguo kutokana na nguo hiyo kutomkaa vizuri. 

“Tena hii tabia naomba niizungumze leo, sio nzuri kabisa kwani unakuta mteja amekuja dukani umemuuzia nguo aliyoitaka lakini baadaye anakuja dukani kuirudisha kisa haijamkaa vizuri, sasa hili jambo linaturudisha nyuma sana na ndio maana kuna time hatukubali kabisa kurudishiwa vitu dukani,” amesema Mwanahamisi.

Aidha aliongezea kwa kuwaomba wateja pamoja na wadau wanaokwenda na fashion kutazama kwanza nguo pamoja na mwili wake kabla ya kuchukua uamuzi wa kuilipia.

 Mbali na hayo, jambo lingine ambalo kuzingatia ni kuangalia nguo au viatu vinavyokupa uhuru wa kutembea na isiwe kikwazo cha kukufanya ukose confidence njiani. 

Hatukuishia hapo, tulipata wasaa wa kuzungumza na mwanadada Dorice ambaye alidai kuwa anapendelea kununua na kuvaa kila mtindo wa nguo unaotoka kutokana na kuwa anaamini huko ndiko kwenda na fashion.

“Ninapenda kupendeza na kuvaa kuendana na wakati uliopo hivyo hakuna fashion inayoingia mjini ikanipita, cha kuwashauri wenzangu ambao hawapendi kupitwa na fashioni ni kuzingatia au kujua size za nguo wanazozivaa” anasema Dorice.

Aidha kwa upande wa mwanadada Ashura Ngwai ameeleza kuwa aliwahi kufanya kosa mara moja tu hivyo kwa sasa anapoipenda nguo basi huwa anafika dukani kwa ajili ya kuitazama na kuona kama inamfaa.

 “Nakumbuka niliwahi kununua nguo baada ya kuomuona rafiki yangu lakini baada ya kuiagizia ilikuwa tofauti na wala haikuendana na mimi kabisa, na kwa bahati mbaya mwenye duka akanikatalia kurudisha, toka siku hiyo mpaka leo nikiipenda nguo mpaka nikaione dukani,” amesema Ashura Ngwai.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post