Kwanini Afrobeats inapenya kuliko Bongo Fleva

Kwanini Afrobeats inapenya kuliko Bongo Fleva

Ni muda sasa kumekuwa na mijadala kwanini muziki wa Afrobeats unazidi kupenya na kupata hadhi kubwa duniani ukilinganisha na aina nyingine za muziki kutokea barani Afrika ikiwemo Bongo Fleva ya Tanzania.
Kwa kulichambua hilo wasanii wa Bongo Fleva na watayarishaji muziki Bongo wamekuwa na maoni tofauti wakati wakizungumza na Mwananchi.

Rapa G Nako, kutoka kundi la Nako 2 Nako Soldiers na Weusi amesema Afrobeats ni muziki wa bara zima la Afrika, hivyo wasanii wa Bongo fleva pia wanaweza kufanya aina hiyo ya muziki na kufanikiwa na kutambulika kama wanatokea Afrika.

"Unajua ukizungumzia Afrobeats moja kwa moja unaugusa muziki kutoka Afrika, kwa hiyo kivyovyote tunatakiwa tufanye muziki ambao utapenya tu na siyo vinginevyo. Kitu kizuri tunachojua kwa Afrika bado Tanzania tunafanya vizuri ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki," amesema G Nako.

Utakumbuka kufuatia kuvunjika kundi la Nako 2 Nako, G Nako na Lord Eyes walijiunga na Nikki wa Pili, Joh Makini na Bonta ambao nao walitokea kundi la River Cap, kisha wakaanzisha kundi la Weusi ambalo hadi sasa limetoa albamu moja, Air Weusi (2021).

Msanii na Prodyuza, Nahreel amesema aina za muziki kutokea Afrika ambazo zimepata kukubalika duniani kama Afrobeats na Amapiano, ni kutokana na kufanyiwa maboresho ya kila mara kitu ambacho Bongofleva inakosa.

"Bongo Fleva ni muziki ambao upo Tanzania na malengo ya wasanii wengi ni kuufikisha mbali, lakini muziki wa dunia unabadilika kila siku na Afrika sasa imekua ina mchango mkubwa duniani. Unaposema Afrika ndiyo hiyo Afrobeats na Amapiano ambayo sasa imeweza kupenya hata duniani," amesema.

"Siku moja tutapoanza kuamini katika Bongo Fleva na kuiboresha (improve) ndipo tutafanikiwa, unajua muziki unapoenda nje lazima uwe umeboreshwa uwe katika viwango vizuri ili uweze kuvutia. Hata hiyo Afrobeats imetokana na miziki mingi, kuna miziki ya Congo, RnB, hip hop hadi ikatengeneza Afrobeats," amesema Nahreel.

Ikumbukwe Nahreel na Aika ndiyo wanaunda kundi la Navy Kenzo ambalo limetoa albamu tatu AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023), huku wakishinda tuzo za muziki Tanzania (TMA), Soundcity MVP, EATV Awards, Hipipo, WatsUp Awards n.k.

Mtayarishaji mkongwe wa muziki Bongo, Master J, amesema Bongo Fleva kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikipiga hatua kwa kasi upande wa kimataifa kiasi kwamba hata kuwatisha wale wanaofanya vizuri duniani na Afrobeats.

"Niwapongeze wasanii wetu kwani kwa muda mfupi mwendo ambao wameenda nao hadi kina Davido sasa wakiangalia nje wanaona vumbi, kwamba wapo karibu, hiyo ni heshima. Kwa sasa kilichobaki ni wasanii wetu kupata 'connection' kitu ambacho Burna Boy kawazidi hapa nyuma," amesema Master J.

Utakumbuka Master J ndiye mwanzilishi wa MJ Records, kwa mujibu wa Master J mwenyewe, studio yake kati ya mwaka 1996 hadi 2010, ilirekodi albamu zaidi ya 500, walifanya kazi na bendi, kwaya na wasanii solo.

Miongoni mwa waliorekodi MJ Records ni Sugu, East Coast Team, Hard Blasters Crew, Afande Sele, Lady Jaydee, Ray C, Kwanza Unit, Deplowmatz, Mr. Paul, Unique Sisters, African Stars Band, DDC Mlimani Park Orchestra na Msondo Ngoma Music Band.

Pia kuna Diamond Sound Band, Akudo Sound Band, Chuchu Band, Hamza Kalala, Kwaya Ya Uinjilisti Kijitonyama Lutheran Church, TOT Band, TOT Taarab, TOT Choir (Marehemu Captain Komba), Marehemu Nasma Khamisi (Sanamu La Michelini/Mtu Mzima Ovyoo).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post