Kwa kiherehere changu yakanikuta makubwa

Kwa kiherehere changu yakanikuta makubwa

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Alhamisi asubuhi na mapema nilikuwa naendesha gari nikitokea nyumbani kwangu Tabata Mawenzi kuelekea kazini kwangu maeneo ya Posta huku nikisikiliza mziki mwororo ambao ulikuwa ukiuburudisha moyo wangu ili kuifanya siku yangu kuwa nzuri kwa siku hiyo.

Nilipokaribia maeneo ya Tabata Bima nilimuona msichana mmoja mrembo hasa akiwa kituoni. Alikuwa ni mjamzito lakini urembo wake ulificha ule ujauzito wake. Alikuwa ni binti mrefu na mwenye rangi ya chokoleti na umbo namba nane.

Nilihisi alikuwa anaenda kazini, na kwa kuwa kulikuwa na dalili ya mvua niliona nimsaidie kumpa lifti. Nilisimamisha gari na kumuuliza kama anaenda Posta nimsaidie kwa sababu ya hali yake ya ujauzito niliona msaada wangu ungekuwa ni muhimu kwake. Yule binti hakukataa aliingia kwenye gari tukaanza safari ya kuelekea mjini.

Tulipofika mjini aliniomba nimshushe pale posta mpya mtaa wa Azikiwe, Sikuweza kufahamu kwamba anafanya kazi wapi kwa sababu hatukuzungumza sana ndani ya gari zaidi ya kusalimiana. Nilipofika kibaruani kwangu niligundua kwamba yule binti alikuwa amesahau pochi yake ndogo ndani ya gari.

Niliamua kufungua pochi ile kwa imani kwamba naweza kupata kitambulisho chake na hivyo kurahisisha mawasiliano. Niliweza kupata kitambulisho chake nikagundua alikuwa anafanya kazi kwenye benki moja maarufu iliyopo mtaa wa Azikiwe.

Nilipiga namba ya hiyo benki na baada ya kumweleza operator aliyepokea simu kuhusu huyo binti aliniunganisha naye. Nilipomweleza kwamba mimi ni yule kijana niliyempa lifti, akadakia haraka haraka na kuniuliza kama niliona pochi yake, nikamjibu kwamba asiwe na wasiwasi kwa sababu ninayo hapo ofisini kwangu. Nilimuuliza ni namna gani naweza kumpelekea hiyo pochi yake. Akanijibu kwamba atanipigia simu karibu na muda wa kutoka kazini. Nilimpa namba yangu ya simu ya mkononi kurahisisha mawasiliano ili anipigie nimpatie pochi yake.

Ilipofika majira ya saa kumi na mbili jioni alinipigia simu na kuniomba kama naweza kumpitishia pochi yake nyumbani kwake maeneo ya Tabata Bima, alinielekeza nyumba anayoishi na kwa kuwa mimi ni mwenyeji katika maeneo hayo, nilipafahamu mahali anapoishi kwa urahisi na nikamuahidi kwamba nikitoka kazini nitampitishia hiyo pochi yake, lakini wakati tukiendelea kuongea mara nikasikia sauti ya kiume kwenye simu.

"Unataka kufanya nini na mke wangu, ngoja nikuone hiyo jioni ukija hapa nyumbani kwangu nitakupiga risasi nikuulie mbali pumbavu kabisa, unacheza na mke wa mtu. Nakwambia nikuone uje hapa nitakumaliza achana na mke wangu kabisa."

Ilibidi nikate simu huku mwili ukinitetemeka na kijasho chembamba kikinitoka nilijikuta nikikata network kwa muda hata sikujua nilitaka kufanya nini kwa wakati ule.

Nilikusanya nguvu na kuendelea na kazi zangu kama kawaida na nilipotoka kazini nilielekea nyumbani moja kwa moja. Nilipofika nyumbani nilioenakana kuwa na lindi la mawazo kiasi kwamba hata mke wangu alinishtukia. Aliponidadisi nilimwambia kwa kifupi tu kwamba ni mambo ya kazi. Kuna wakati nilitaka nimweleze, lakini nikaona atanigeuzia kibao akidhani kwamba labda nina mahusiano na huyo binti mjamzito. Wakati mwingine hawa wake zetu wanaweza kuzusha balaa mahali usipotarajia. Ilinibidi nipige kimya.

Siku iliyofuata yaani Ijumaa majira ya saa tatu asubuhi nikiwa ofisini, yule mwanamke mjamzito alinipigia simu tena, nilipoipokea aliniomba sana radhi. Aliniambia kwamba yule mwanaume aliyenikaripia jana jioni alikuwa ni mumewe. "Kwa kweli hata mimi nimemchoka kwa sababu ya wivu wake, yaani mume wangu hataki kabisa kuniona nawasiliana na mwanaume wa aina yoyote, hata wafanyakazi wenzangu wa kiume huwa hawanipigii simu nikiwa nyumbani hata kama kuna jambo muhimu la kazini. Hata sijui nifanye nini?" Alisema mwanamke yule kwa huzuni.

Nikamwambia, "samahani dada, sitaweza kukuletea pochi yako nyumbani kwako kama unaweza upitie hapa kazini kwangu uje uichukue".

Itaendeleaaaaaaaaaaaa………………….






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags