Hivi sasa imethibitika kwamba, watu wasiooa au kuolewa, wanaishi kwa umri mdogo zaidi ukilinganisha na wale ambao wameoa au kuolewa.
Taarifa hizi siyo hadithi bali ni ukweli ambao, una vigezo vyenye kuusimamia. Kwa mfano, kwenye jarida la Epidemiology and Community Health la nchini Marekani, imebainishwa kuhusu utafiti ambao, kwa ujumla ulihusisha zaidi ya washiriki 80,000.
Utafiti huo pamoja na tafiti nyingine, zimeweza kuthibitisha kwamba, watu ambao hawajawahi kabisa kuoa au kuolewa maishani mwao, hufa mapema ukilinganisha na wale ambao walioa au kuolewa na kisha kuachana.
Hii ina maana kwamba, ile tabia ya kuingia kwenye ndoa ili kutoa nuksi, ina manufaa zaidi kwa wanaofanya hivyo, kuliko ile ya watu kutooa au kuolewa kabisa maishani mwao.
Kwa nini watu ambao hawajawahi kabisa kuoa au kuolewa wako kwenye hatari ya kufa mapema? Inaonekana kuna sababu kadhaa, lakini kubwa ni pamoja na ile ya kiafya. Kwa kutooa au kuolewa, mtu anakuwa na maisha ya rahisi kuanzia kwenye kula na wakati mwingine hata kutunza afya yake inakuwa ni vigumu.
Ndani ya ndoa watu husaidiana kukumbushana na kujaliana kuhusu afya ya kila mmoja wao. Kuna kuhimizana katika kukagua na kujali afya, bila kujali hali ya kipato ya mtu. Wanaume wanaonekana kuathiriwa zaidi na adhabu hii ya kutooa, ingawa wanawake nao huathirika.
Tafiti nyingi za kutosha zinaonyesha kwamba, watu ambao hawajawahi kuoa au kuolewa, hukabiliwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu na lehemu (Cholesterol) ya ziada mwilini. Pengine hii inatokana na ile hali ya mtu kukosa mwenzake wa kusaidiana naye kubeba mizigo ya maisha.
Inaonekana pia kwamba, wale watu ambao, hawajawahi kuoa au kuolewa maishani mwao, hukabiliwa na uwezekano wa kufa kwenye ajali, kuuawa au kujiuwa kwa mara mbili zaidi ukilinganisha na wale ambao wameoa au kuolewa.
Bila shaka wale wanaokufa kutokana na maradhi ya moyo ndiyo wengi zaidi, kwani hufikia asilimia 40 ukilinganisha na wale waliooa au kuolewa. Kwa hiyo upweke na kushindwa kuwa na msaidizi, huenda ni sababu kubwa.
Wale ambao hawajawahi kuoa au kuolewa na wakawa hawana watoto au wakawa hawana ndugu na jamaa wengi wa kuwa nao karibu, hawa hufa mapema zaidi. Walioolewa na kuachwa au waliooa na kuacha, wanakuwa na mtandao fulani, ambao wanandoa huwa nao kwa kawaida.
Tafiti nyingi za siku za nyuma na hivi sasa zinaonnesha kwamba, kutengwa au mtu kukosa watu wa kuwa karibu naye katika masuala ya kijamii, husababisha kifo cha mapema. Ndoa hujenga ukaribu huo kwa sababu, mtu hujiongezea watu wanaomhusu kutoka kwa mwenzake.
Huenda moja ya sababu ya jamii nyingi kusisitiza suala linalohusu kuoa au kuolewa ni hii ya kutaka watu wake waishi zaidi. Inawezekana wana jamii hawajui ni kwa sababu gani wanasisitizwa kuoa au kuolewa, wanajua baadhi ya sababu tu, lakini hii ya kuishi muda mrefu walikuwa hawajaigundua.
Leave a Reply