Kumbukumbu ya Zahara kwenye mapenzi yake kwa muziki

Kumbukumbu ya Zahara kwenye mapenzi yake kwa muziki

Siku zote mshumaa ukizimika huacha giza, ndicho kilichotokea kwa wadau na mashabiki wa burudani mwishoni mwa mwaka 2023, licha ya kuwa wapo wasanii wengi chipukizi waliojitokeza mwaka huu, lakini apoteapo mkongwe mmoja basi huacha pengo kubwa kwenye tasnia.

Bulelwa Mkutukana ndilo jina lake kabla ya watu kumfahamu kama 'Zahara', alikuwa moja kati ya watunzi na waimbaji wazuri wa nyimbo kutokea Afrika Kusini akitumia lugha yake ya asili, Kixhosa, na kingereza katika uburudishaji. Wengi walianza kumfahamu baada ya kuingia mkataba na 'lebo' ya TSRecords, ambayo katika kuzungumzia mafaniko ya masanii huyu lazima nayo itajwe.

Baada ya kuingia mkataba na lebo hiyo Zahara aliachia albamu yake ya kwanza mwaka 2011 na kuipa jina la 'Loliwe' ambayo wengi walimfahamu kupitia kazi hiyo iliyopata mafanikio makubwa ikiwemo kuthibitishwa kuwa 'platinamu. Baada ya miaka miwili aliachia tena albamu ya pili iliyoitwa 'Phendula' mwaka (2013), nayo ilipita katika mafanikio kama 'Loliwe' baada ya albamu hiyo kutoa nyimbo tatu bora , zikiwemo 'Phendula', 'Impilo', na 'Stay'.

Kwake ulikuwa kama utaratibu kila baada ya miaka miwili lazima awalishe wadau wa muziki kazi nzuri kutoka kwake, mwaka 2015 alidondosha albamu iitwayo 'Country Girl' ambayo nayo iliingia kwenye 'platinamu' mara tatu.

Baada ya kuachana na 'lebo' ya TS Records mwaka 2017, alitia saini mkataba wa kufanya kazi na 'lebo' ya Warner Music kutoka nchini Marekani hakulaza damu mwaka huohuo aliachia albamu ya nne, iitwayo 'Mgodi', ambayo ikawa albamu yake iliyouzwa zaidi na kuthibitishwa kuwa 'platinamu'. Ilipofika mwaka 2021 Zahara alitoa

albamu yake ya tano iliyoitwa 'Nqaba Yam' nayo ilishika nafasi ya kwanza kwenye iTunes.

Kutokana mafanikio ya kazi zake za kimuziki Zahara alifanikiwa kupata Tuzo 17 za Muziki Afrika Kusini, Tuzo tatu za Metro FM, na Tuzo moja kutoka nchini Nigeria. Wengi walimtazama msanii huyu kwa jicho la kiburudisho kikuu kwao kutokana na sauti yake tamu na tunzi zenje kubeba hisia, lakini kwa sasa kumbukumbu alizoacha kwa mashabiki wake ni kazi zake

Zahara alizaliwa nchini Afrika Kusini na alianza kuimba katika kwaya ya shule alipokuwa na umri wa miaka sita, na akiwa na umri wa miaka tisa alijiunga na kwaya ya wakubwa kwa sababu ya sauti yake. Zahara alizaliwa mwaka 1987 na kufariki dunia Desemba 11, 2023 kutokana na ugonjwa wa ini akiwa hospitalini mjini Johannesburg.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post