Kimenuka Tena Kundi La P-Square

Kimenuka Tena Kundi La P-Square

Mwanamuziki wa Nigeria Paul Okoye ‘RudeBoy’ wa P-Square amesema pacha wake Peter ‘Mr P', ndiye aliyehusika kumuweka gerezani kaka yao mkubwa Jude Okoye. Aliyekuwa meneja wao katika kundi la P-Square.

Rude ameyasema hayo Machi 4, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akiahidi kumsaidia kaka yake atoke gerezani.

“Sitamuacha kwa sababu ninasimama upande wa ukweli. Ukweli ni kwamba Peter ndiye anayempitisha Jude katika haya yote. Ni Peter anayefanya haya. Amemuweka gerezani, na mimi niko hapa kumtoa. Ninasimama tu kwa ajili ya ukweli, kwa sababu ikiwa Jude ana hatia ya uhalifu huu unaodaiwa, basi Peter pia ana hatia, na mimi pia,” amesema RudeBoy

Utakumbuka Tume ya Kupambana na Uhalifu wa Kiuchumi na Fedha (EFCC) ilimshitaki Jude, kwa makosa ya utakatishaji fedha zenye thamani ya Naira 1.38 bilioni ikiwa ni zaidi ya Sh 30 bilioni.

Jude alifikishwa katika Mahakama ya Shirikisho jijini Lagos pamoja na kampuni yake, Northside Music Ltd, mbele ya Jaji Alexander Owoeye siku ya Jumatano Februari 26,2025. Akikabiliwa na mashtaka saba huku akikana mashtaka yote akidai kuwa hana hatia.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Larry Peters Aso uliomba Jude awekwe kizuizini. Hata hivyo, wakili wa mshtakiwa, Inibehe Effiong, aliwasilisha ombi la dhamana, akitaka Jude aendelee kuwa chini ya uangalizi wa EFCC hadi kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Utakumbuka mwanzoni mwa Agosti 2024 Paul Nonso Okoye ‘Rudeboy’ alithibitisha kusambaratika kwa kundi la PSquare kwa mara nyingine. Kwa kudai toka walivyoungana hakuna cha maana kilichowahi kufanyika.

Kundi la P-Square lilisambaratika kwa mara ya kwanza mwaka 2016 na kuungana tena mwaka 2021, huku mwishoni mwa mwaka juzi kukiwa na tetesi kuwa wawili hao wamegawanyika tena.

Tangu kuanza kwa bifu la wawili hao, limewakosesha michongo ya fedha kadhaa ukiwemo mchongo wa kutumbuiza katika tuzo za Grammy mwaka huu ambapo walipewa ofa ya dola 4 milioni ikiwa ni zaidi ya Sh 10 bilioni lakini walikataa.

Wawili hao wamewahi kutamba na ngoma kama ‘Taste The Money (Testimony )’, ‘Personally’, ‘Forever’ Do Me, More Than a Friend pia wamewahi kutoa kolabo na mwanamuziki Diamond wimbo uitwao ‘Kidogo’






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags