Khalid Chokoraa: Muziki wa dansi una unafiki mwingi

Khalid Chokoraa: Muziki wa dansi una unafiki mwingi

Mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Khalid Chuma 'Chokoraa' amesema, ndani ya muziki huo kuna unafiki mwingi kitu kinachokwamisha kuwapo kwa ushirikiano wa kuupeleka mbele zaidi ya ulipo.

Mtunzi na mwimbaji huyo wa bendi ya Twanga Pepeta International ambaye pia ni bondia wa ngumi za kulipwa, amesema wanamuziki wengi wa dansi ni wanafiki, kiasi watu wanaogopana kushirikiana kwa kuhofia kufanyiwa usnichi na kufanya dansi lidorore.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chokoraa anasema endapo wasanii wa dansi wangeacha unafiki, wangefanya makubwa kwani mashabiki wanatamani kuona ushirikiano wao kwenye kazi zao na hata kuupambania muziki huu.

"Unajua kuna wakati ifikie hatua tusiwalaumu sana media kuwa ndio wanaoshusha muziki wa dansi, hapa kikubwa ni sisi wenyewe kwanza wasanii wa muziki wa dansi kuacha unafiki, chuki na tamaa ambazo zinapelekea kukosa ushirikiano wa kuupambania muziki wetu.

"Tena kuna haya magroup ya whatsApp ndio unafiki mkubwa unapoanzia na kubeba yote haya, sema wengi hawajui tu, sababu utakuta mtu umetuma kazi yako ya bendi au binafsi anaweza tokea shabiki akaponda hiyo kazi, lakini anakuja msanii wa dansi anakufuata inbox anatoa comments za kusifia, anaacha kukomenti palepale kwenye group.

"Sasa unajiuliza huyu ni msanii, kwanini asikupambanie palepale kwa group na comments za mashabiki ili kuonyesha ile nguvu moja? Na sio hili tu, mtu anaweza kukuchukia tu bila sababu kisa tu unatunzwa sana stejini au umetoa kazi imekubalika kwa mashabiki, mtu anaweka chuki nawe badala ya kukusapoti."

MIAKA 20

"Mimi naweza kusema nina miaka ishirini na zaidi kwenye huu muziki na ni Mzaramo wa kwanza kuacha alama kwenye muziki wa dansi, yaani nina rap kibao na nyimbo kibao ambazo za zamani zinaendelea kuishi kwa kufanya vizuri hadi leo."

Kuhusu jina la Chokoraa, mwanamuziki huyo anasema; "Hili jina bana, si unajua mie naitwa Khalid Chuma hili la Chokoraa nililipata kwa ajili ya utukutu usioumiza yaani ni mtukutu, lakini siwaumizi watu nikiwa jukwaani, ndio mashabiki wakanipa hili jina kutokana na utukutu wa kuimba na kucheza jukwaani."

Juu ya siri za tunzi zake kudumu kwa mashabiki Chokoraa anasema huku akitabasamu; "Jamani watu inabidi wafahamu kuwa kuna watunzi na wapepesaji, sasa mimi ni mtunzi japo wapo wengine watunzi na nawaheshimu ila Tanzania mimi ndio namba moja halafu hao wengine ndio wanafuata na siri yangu kubwa ni kutunga nyimbo zinazogusa jamii yaani kujua mashabiki kwasasa wanataka nini na hata tungo nyingine zinanihusu mim."

WIMBO MKALI

Chokoraa anasema licha ya kutunga na kuimba nyimbo nyingi, lakini kuna ngoma kali moja anayoikubali na kuitaja;

"Naukubali sana wimbo wa 'Kuachwa', nashukuru wimbo ambao unakubalika na mashabiki hadi leo."

Anapoulizwa kibao hicho alijitungia mwenyewe ama ilikuwaje naye anajibu; "Hapana, na watu wengi wanadhani huu wimbo nimeutunga sababu ya mimi niliwahi kuachwa, huu wimbo ni mawazo tu yalikuja nikatuunga, hivi unajua mimi ni mgumu kuachwa? Yaani kwenye mapenzi sitakagi usumbufu, hapo zamani kuna msichana mmoja kila nikigombana naye anasema 'anaondoka anaondoka' basi ikafika siku nikamwambia nenda na nilikuwa nampenda huwezi amini."

"Siri ya wimbo wa kuachwa bana, ngoja leo niweke wazi, nilienda Tanga kwa babu nikamuachia CD wiki nzima kabla sijautoa huu wimbo, nikarudi Dar es Salaam, baada ya muda nikarudi Tanga kuichukua ile CD nikaanza kuisambaza kwa redio mbalimbali yaani mapokezi yake ya wimbo hata mimi nilishangaa maana ni makubwa sana," anafafanua Chokoraa, akikanusha sio kazi zote huzipeleka Tanga.

"Hapana, sababu huyo mzee ameshafariki, hivyo napambana tu mwenyewe hivyo hivyo na nashukuru mapokezi sio mabaya," anasema na kuongeza kwa kuzitaja nyimbo nyingine kali anazojivunia.

"Kuachwa niliutoa nikiwa katika bendi ya Mapacha Watatu, kuna 'Sumu ya Mapenzi' wa Twanga Pepeta, 'Shika Ushikacho' wa Mapacha, 'Karibu Yangu' ft Christian Bella, 'Zungu la Roho', 'Umasikini Mbaya' na nyingine nyingi ukiwamo huu wa sasa wa 'Mbeya' wa Twanga Pepeta."

HISTORIA YAKE

"Nilianzia muziki Zanzibar kwenye bendi ya Coconut, kule Zanzibar nilienda kusomea Chuo cha Veta mwaka wa kwanza na wa pili, wakati huo akili yangu ilikuwa muziki tu, hivyo nikatafuta bendi wapi wanapiga nyimbo za kukopi hotelini, nikajichomeka chomeka, baada ya hapo nikaja Dar kwenye bendi inaitwa Mokibo, nikatoka nikaenda Tanga kuna bendi inaitwa Capital Sound, nikarudi Dar es Salaam, nikatua kwenye bendi ya Extra Bongo ya Ali Choki, baada ya hapa nikaingia Twanga Pepeta na wimbo wa kwanza kuimba ni 'Safari' aliutunga Msafiri Diouf, nilikaa miaka kadhaa nikatoka tukaanzisha bendi yetu ya Mapacha Watatu nikiwa mimi, Jose Mara na Kalala Junior, nikatoka nikaanzisha bendi yangu 'Mapacha Music Band' hapa niliiacha hii nikajiunga tena na Twanga na hadi leo nipo hapa Twanga Pepeta."

Kuhusu ratiba ya chakula anasema;

"Mimi bwana nina ratiba yangu kabisa nyumbani kwangu, asubuhi sipendi kunywa chai, mimi nikiamka asubuhi napenda kunywa supu ya mboga za majani, na kuwa na bakuli langu kabisa, mchana ugali na mboga mboga za majani, usiku matunda au mboga za majani na ugali.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post