Unaweza kusema ni lugha gongana kutokana na kauli za mama wa msanii na mfanyabiashara Hamisa Mobetto, Shufaa Rutiginga kuhusu ndoa ya binti yake na nyota wa Yanga Stephanie Aziz Ki.
Mama huyo ameendelea kuwaacha mashabiki wa mwanae katika maswali baada ya kuwa na kauli zenye sintofahamu kila anapoonge na vyombo vya habari kuhusu tukio hilo.
Utakumbuka akiongea na Mwananchi Februari 6,2025 alipoulizwa kuhusu tetesi za ndoa ya binti yake na nyota huyo wa Yanga, alikanusha na kudai hata yeye anaona kwenye mitandao ya kijamii.
"Kiukweli mimi hapana, sijui habari za ndoa wala sijapokea posa ya huyo mchezaji, mie nasikia tu kama unavyosikia wewe na kuona kwenye mitandao, nami ndiye mama mzazi na Hamisa, na mwanangu Hamisa huwa hanifichi kitu chochote, tumezoea kuzungumza kila wakati na kupeana ushauri wa mambo mbalimbali, ila kwa hili kama lipo ningelijua tu," alisema mama huyo.
Hata hivyo baada ya kudai hayo kwenye mitandao ya kijamii ziliendelea kusambaa video na picha za Aziz na Hamisa zikionesha ratiba ya tukio lao. Ambapo ratiba ya tukio hilo la ndoa inasomeka Februari 15,2025 (mahari), Februari 16,2025 (ndoa) na Februari 19, 2025 (harusi).
Licha ya kukanusha kuwepo kwa posa ya Aziz, mama huyo alifanya mahojiano na Vidox wa Millard Ayo, jana Februari 11, 2025 alipoulizwa kuhusu ndoa ya binti yake alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
"Jambo lipo kama mlivyoliona mahari tunapokea Jumamosi, bibi harusi anataka kupeleka harusi kijeshi lakini michango lazima mtoe. Shughuli zote ni hapa Tanzania labda baada ya yote hayo ndiyo wataplani nje. Shughuli zitakuwa risepsheni terehe 19,2025 alafu tarehe 15,2025 mahari
"Nimefurahi sana kwa kweli Mungu amenihurumia, yaani kwanza Aziz ni kijana ambaye ni mstaarabu, ana upendo anatupenda ni mwanaume ambaye amekuja wakati sahihi nilivyokuwa naomba ndiyo Mungu amejibu nilikuwa naomba mwanangu apate mwanaume sahihi,"alisema
Hata hivyo leo Februari 11, 2025 mama huyo alipozungumza na 'Hekaheka' ya Clouds Fm ameibua mapya baada ya kusema wawili hao walifunga ndoa miezi minne iliyopita.
“Eeeh ndoa ni siku nyingi kwa kweli ila hii ya kuhalalisha hivi ndio inafanyika sasa hivi, lakini ile ndoa yenyewe imepita siku nyingi, walikuja baadhi ya watu wa familia ya GSM walituma wawakilishi kuleta posa na shughuli nyingine ziliendelea hapo kati. Aziz na Hamisa ni mke na mume halali muda mrefu imefika miezi minne tangu wafunge ndoa yao,” amesema mama Mobetto

Leave a Reply