Kassim Mganga atoa maana ya collabo ya kimataifa

Kassim Mganga atoa maana ya collabo ya kimataifa

Miaka kadhaa nyuma nilikuwa nafanya ‘interview’ na msanii wa Bongo Fleva, Kassim Mganga. Ilikuwa ni kipindi ambacho wasanii wa Bongo walikuwa wamechachamaa kufanya kolabo na wasanii wa nje ya Tanzania. Nikamuuliza Kassim, “Tutegeeme lini kuona ukifanya kolabo na msanii wa kimataifa?” Kassim, kwa kujiamini, akanijibu, “Nimewahi.”

Nikamtazama huku akilini nikijiambia, Huyu jamaa ameanza kula mjani nini? Mimi najua ngoma zake zote, na kati ya hizo hakuna hata moja aliyofanya na msanii wa kimataifa. Inakuwaje aseme amewahi kufanya kolabo za kimataifa? Nikamwomba anielezee, nikamuuliza, “Wimbo gani?” Kassim akanijibu, “Wimbo wangu huu mpya.” Wimbo wake mpya alikuwa amefanya na Kilimanjaro Band, unaitwa Somo.

Kimoyomoyo nikapiga mstari Kassim ameshaanza kudata. Amefanya ngoma na hawa wazee wa Tanzania tena wanaimba nyimbo ambazo naweza kuziita traditional, halafu anasema ni kolabo ya kimataifa? Lakini nikaona isiwe kesi, nikamuomba ufafanuzi juu ya hilo.

Kassim alinambia kitu kama hiki:

“Unajua watu wanadhani kufanya international collabo ni lazima ufanye na msanii wa Nigeria au nje ya nchi, kwangu mimi hapana. Kwangu mimi, international collabo ni kufanya kazi na wasanii ambao wana mashabiki zaidi ya Tanzania. Njenje wamekwenda nchi nyingi duniani kufanya shoo, hiyo ina maana kina Njenje ni wasanii wa kimataifa. Kwa hiyo, kufanya nao kazi ina maana nimefanya kazi na wasanii wa kimataifa, na wimbo wangu ni wa kimataifa.”

Binafsi, nilimwelewa Kassim. Niliona alichokisema kina ukweli ndani yake na kilinifanya nijiulize: Ni nini maana ya kufanya kolabo ya kimataifa? Je, ni kufanya tu kazi na msanii wa nje ya mipaka ya nchi yako au kufanya kazi na msanii mwenye uwanda mkubwa wa mashabiki kwenye mataifa mbalimbali duniani?

Kwa mfano, kati ya hawa wawili, ni nani msanii wa kimataifa? Msanii asiyefahamika kutoka Nigeria au Diamond Platnumz wa Tanzania, ambaye ni moja ya wasanii wakubwa wa Afrika wenye uwanda mkubwa wa mashabiki nje ya Bongo? Msanii wa ndani akifanya kolabo na hawa wawili, ipi inaeleweka zaidi kusema ni kolabo ya kimataifa?

Nadhani inabidi tubadilishe maana yetu ya kolabo ya kimataifa. Binafsi, nadhani tunatakiwa kulalia zaidi kwenye upande wa uwanda wa mashabiki wa msanii husika kuliko nchi anayotokea. Kama msanii anaenda Afrika Kusini na kufanya kolabo na msanii asiyejulikana, haina haja ya kuita kolabo ya kimataifa kwa sababu ukweli, msanii aliyefanya naye kazi hakuna anayemjua zaidi ya Waafrika Kusini wenyewe tena usikute hata sio wote wanamjua. Nadhani tunaposema kolabo ya kimataifa, tuangalie nguvu ya msanii kwenye ushawishi wa mashabiki kimataifa. Hata kama ni msanii wa ndani, lakini kama mashabiki kutoka nchi mbalimbali tena nyingi wanamuhusudu, hiyo inafaa kuitwa KOLABO YA KIMATAIFA.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags