Jinsi janga la Uviko-19 lilivyoibua fursa kwa Dorice Kaijage (UDSM)

Jinsi janga la Uviko-19 lilivyoibua fursa kwa Dorice Kaijage (UDSM)

Januari 30, 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza rasmi ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Uviko-19) kuwa ni dharura ya jamii kimataifa na Machi 11, mwaka jana likatangaza kuwa ni janga la dunia.

Ugonjwa huu ulipotangazwa, mataifa mengi yaliingiwa na hofu ambayo iliwafanya watu duniani kupoteza maisha huku wengine wakikata tamaa hata ya kuishi.

Hata hivyo, ugonjwa huu uligundulika Tanzania mwezi wa Machi 16, 2020. Hii ni siku ambayo Mtanzania wa kwanza mwenye umri wa miaka 46 alitangazwa kuwa na virusi vya Uviko-19.

Mtanzania huyo ndiye aliyekuwa amesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark na aliporejea Tanzania na kupimwa aligundulika kuwa na virusi hivyo.

Pamoja na ugonjwa huu wa Uviko-19 kusababisha vifo na kuleta athari mbalimbali katika jamii, inaelezwa kuwa ulisababisha pia kasi ya uzalishaji wa chakula, ufanyaji wa biashara katika maeneo mengi duniani kupungua kutokana na watu kuwa na uoga wa kutoka ndani kwenda kufanya shughuli zao.

Kwa mwanadada Dorice Kaijage muhitimu wa Shahada ya Uandishi wa habari mwaka 2021 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ilikuwa ni tofauti kwani katikati ya janga hilo aliona fursa ya kufanya biashara ya kuuza nguo za mitumba.

Dorice ambaye pia ni Mratibu wa Asasi isiyo ya kiserikali iliyopo Mkoani Kagera inayoitwa OmukaHub inayojihusisha na kutoa ujuzi wa kidijitali kwa watu waishio mikoa ya pembezoni, anasema wazo la kufanya biashara alilipata wakati tu ulipozuka ugonjwa wa Uviko 19.

Anasema kipindi cha ugonjwa huo hapo awali vyuo na shule mbalimbali zilifungwa na kufanya watu kukaa nyumbani na hali kuwa ngumu hata vyuo vilipofunguliwa hivyo alipata wazo la kwenda kuchukua nguo za mitumba na kuanza kuuza.

“Biashara hiyo wakati naianza nilikuwa mwaka wa pili hivyo nilianza kuamka alfajiri saa kumi kila jumamosi na kwenda Karume kununua nguo na kurudi kuziuza kwa wanachuo wenzangu,” anasema na kuongeza

“Wazo la kufanya biashara nililipata baada ya kuzuka kwa wimbi la Uviko 19 mwaka 2020 baada ya kuona hali ilivyo ngumu, Mnamo mwezi juni mwaka 2020 nikaamua kuanza kuuza nguo za mtumba na ubuyu, lakini baadaye nikabaki na biashara ya nguo,” anasema.

Anasema biashara hiyo inamsaidia kutimiza mahitaji yake ya muhimu kama chakula, mavazi na malazi.

Anasisitiza kuwa aliamua kufanya biashara ya nguo kwani ndiyo aliyokuwa akiifanya Mama yake kipindi nakua na alikuwa akipata faida.

Kuhusu Changamoto

Anasema moja ya changamoto kubwa katika biashara hiyo ni mtaji. “Biashara yangu nafanyia mtandaoni ila natamani kupata frem kubwa na kuwa uwezo wa kwenda kununua nguo nje nije niziuze Tanzania,”

 Aidha anasema faida alizopata kupitia biashar hiyo ni kuweza kujikimu maisha ya kila siku, kutengeneza marafiki ambao wanasaidiana katika masuala mengine ya kijamii pamoja na kukuza uelewa wa soko.

“Pamoja na faida hizo nashauri vijana wasikubali kukaa bila kujishughulisha hata kama wana ajira au hawana, inabidi watafute kipato cha pembeni kitakachowawezesha kustahimili maisha. Lakini pia unapojishughulisha ndo unavyokuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha,” anasema

Anasema mbali ya ufanyaji huo wa biashara amesomea uandishi wa habari na kusisitiza kuwa anapenda kuandika makala, kuandaa habari na kureport matukio.

“Lakini pia napenda kufundisha juu ya ujuzi wa kidijitali kwa watu wa mikoani ili waweze kujua na kunufaika na fursa za kidijitali zinazopatikana mtandaoni,” anasema

Vilevile anasema anatamani kuja kumiliki kampuni  na biashara tofauti tofauti,  kusaidia jamii inayomzunguka katika kupata suluhu ya matatizo mbalimbali.

Anafafanu kuwa wazazi wake ndo role models wake kwani wamejitoa sana katika kuhakikisha anapata malezi bora na elimu bora, hivyo kujituma kwake anawaangalia wao na wamekuwa wakinipa support kubwa sana.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post