Jeje yamtoa Diamond kimasomaso na kukata mzizi wa fitna!

Jeje yamtoa Diamond kimasomaso na kukata mzizi wa fitna!

Baada ya kukosolewa kwa muda mrefu kuwa video za nyimbo zake zilizotazamwa zaidi YouTube ni zile alizoshirikiana na wasanii wengine wa kimataifa, hatimaye Diamond Platnumz amekata mzizi wa fitna kupitia wimbo wake, Jeje (2020).

Wiki hii video ya Jeje imefikisha 'views' milioni 100 YouTube na kuwa video ya kwanza ya wimbo wa Diamond aliyoimba pekee yake (solo) kufikia namba hizo akiwa ni msanii wa pili Tanzania na Afrika Mashariki.

Hayo yanajiri baada ya Machi mwaka huu video ya Zuchu, Sukari (2021) kufikisha 'views' milioni 100 YouTube na kuwa msanii wa kwanza solo kutoka Tanzania na Afrika Mashariki ikiwa ni miaka minne tangu kusainiwa WCB Wasafi yake Diamond.

Ikumbukwe video ya Sukari ilitoka Januari 30, 2021 ikiwa imeongozwa na Director Kenny wa Zoom Extra, huku ikiandika rekodi ya kuwa video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa mwaka 2021.

Sukari ya Zuchu, wimbo uliotengenezwa na Maprodyuza wawili; Trone na Lizer Classic, video yake ilimaliza mwaka 2021 ikiwa na 'views' zaidi ya milioni 60 YouTube na kufuatiwa na ile ya Wizkid 'Essence' iliyokuwa na 'views' zaidi ya milioni 50.

Ndivyo ilivyokuwa na Jeje ambapo kwa 2020, ndio iliongoza kwa kutazamwa zaidi YouTube Afrika ikimaliza mwaka na 'views' zaidi ya milioni 40. Msanii wa Nigeria, Simi ndiye alishikilia nafasi ya pili kupitia video ya wimbo wake 'Duduke' iliyopata 'views' zaidi ya milioni 29.

Hadi sasa nyimbo nyingine za Bongo Fleva zenye 'views' zaidi ya milioni 100 YouTube ni Kwangwaru (2018) wa Harmonize na Diamond, Yope Remix (2019) wa Diamond na Innoss'B, Inama (2019) wa Diamond na Fally Ipupa, Waah! (2020), Achii (2023) zake Diamond akiwa na Koffi Olomide.

Ulitazama kwa makini utagundua Diamond anahusika moja kwa moja na video zake za Bongo Fleva zenye 'views' zaidi ya milioni 100. Huyu ndiye msanii wa pili kutazamwa zaidi katika mtandao huo Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa ametangulia na mshindi wa Grammy kutokea Nigeria, Burna Boy.
Hata hivyo, wakati wimbo 'Jeje' unatoka ulikosolewa sana kwa madai umechukua vionjo vingi kutoka kwa ule ya Wizkid, Joro (2019). Lakini Meneja wa Diamond, Sallam SK alisema hilo linatokana na nyimbo zote mbili kutengenezwa na Prodyuza mmoja, Kelpvibe kutoka Nigeria.
Pia video ya Jeje ambayo mrembo kutoka kisiwa cha Reunion, Malaika Salatis aliinogesha, uchezaji wake na muonekano wake kwa urefu hauna tofauti na mrembo, Georgia Curtis mwenye asili ya Nigeria na Hispania ambaye alitokea kwenye video ya Wizkid, Joro.

Ikumbukwe Malaika Salatis ambaye alipelekea video ya Jeje iliyofanyika Zanzibar kuwa maarufu sana, amezaliwa na kukulia Reunion ambayo ni idara ya Ufaransa, kisiwa hiki kipo kwenye Bahari ya Hindi, Mashariki mwa Madagascar na Kusini Magharibi mwa Mauritius.
Akiwa na umri wa miaka 25, Malaika aliamua kuifukuzia ndoto yake kwa kuhamia Sydney nchini Australia alipojifunza mengi kuhusu sanaa na sasa anatambulika kama Mwimbaji kitaaluma, Dansa na Mwanamitindo.

Katika mahojiano na 7 Magazine kutoka Reunion, Malaika anasema amekuwa akipenda sana Muziki na dansi tangu akiwa mdogo, hivyo kwenda kuishi Australia na kuanza tena kucheza dansi baada ya kusimama kwa zaidi ya miaka mitano, ilikuwa changamoto kwake.

Hata hivyo, kwa kipindi hicho cha mwaka 2015, haraka Malaika alijiimarisha kama Mwanamitindo na Dansa na baadaye kufanikiwa kutumbuiza na wasanii mashuhuri kama vile Macklemore, Tiwa Savage na wengine wengi na alionekana kwenye vipindi vya Runinga.

Mwaka 2017 Malaika alitafutwa na lebo kubwa, Warner Music Australia na hapa ndipo alianza kujiendeleza kama msanii wa muziki kitaaluma. Katika tovuti yake amesema anatumai atapaza sauti na kuibua msukumo wa ndani ya mioyo ya kizazi kijacho kupitia maono yake ya kisanii.

Hadi sasa Malaika ndiye mrembo pekee ambaye ametokea katika video mbili za Diamond, ukiachana na Jeje, kuna Gidi (2022), ambayo ilitoka siku chache baada ya wawili hao kutumbuiza pamoja kwenye shoo maalum iliyoandaliwa na waandaaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy ijulikanayo kama Global Spin.

Lakini video ya Gidi ambayo sasa ina 'views' zaidi ya milioni 14 YouTube, ilikosolewa sana mtandaoni mara baada ya kuonyesha bendera ya kibaguzi, Confederate flag ya nchini Marekani.

Katika video hiyo iliyotoka Februari 18, 2022, bendera hiyo inaonekana kwenye sekunde ya 32 kwa udogo sana ingawa kwenye picha zilizopigwa wakati video hiyo ikitengenezwa ndipo imeonekana sana.

Bendera hiyo ikionekana popote pale inatoa ujumbe unaosema kuwa wazungu ni watu wenye thamani kuliko watu wengine wenye rangi ya ngozi tofauti na nao. Wenyewe wanaita White Supremacy. Kwa hiyo, bendera hiyo ya ubaguzi wa rangi inahusishwa sana na watu wabaguzi wa rangi wanaojulikana kwa kizungu kama ‘neo-narcists’ na ‘far right extremists’ kama kitu cha kuwatishia Wamarekani Weusi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post