Jay Moe aelezea anavyomkumbuka Mangwea

Jay Moe aelezea anavyomkumbuka Mangwea

Tarehe kama ya leo mwaka 2013 alifariki mwanamuziki Albert Keneth 'Mangwea', aliyewika miaka ya 2000 kwa ngoma kama vile 'Ghetto Langu','Kimya Kimya'
'Nipe deal','Alikufa kwa ngoma','Napokea simu', 'Weekend', She got a Gwan na nyinginezo.

Mangwea alikuwa ni miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri katika miaka hiyo na kusababisha aibuke mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania kama Msanii Bora wa Hip Hop mwaka 2005.

Akizungumza na Mwananchi Mwanamuziki Juma Mchopanga 'Jay Moe' ambaye alikuwa miongoni mwa rafiki zake wa karibu amesema, ukaribu wake na Mangwea ulitokana na wao kuwa majirani, pia walitoka katika lebo moja.

"Ukaribu wetu ulikuwa kwa sababu wote tulikuwa tunaishi jirani pili tulikuwa kwenye lebo moja ambayo ni Bongo Records na pia alikuwa msanii wa hip-hop na mimi pia nilikuwa hivyo, kilichotuunganisha ni muziki kwa sababu kabla hatujaunganika tukiwa Bongo Records tulikuwa wote tupo mtaani.

"N muziki ulituunganisha mimi na yeye tukajuana japo tulikuwa majirani lakini kulikuwa na umbali kidogo kwa hiyo bila kujali umbali huo kwa sababu ya muziki alichokuwa anakipenda yeye na ndoto ya muziki aliyokuwa nayo yeye ndiyo hivyo hivyo ilikuwa kwangu," anasema.

Jay Moe anasema anachokumbuka kutoka kwa Mangwea ni kipaji chake na aina ya mashairi na uwakilishi wake kuwa na ubora.

"Ninachomisi mimi ni kama wanachomisi Watanzania na wengine duniani, ambao walikuwa wanamfahamu na wakajua ubora na ukubwa wa kipaji chake, maana yake ninachomisi mimi ni hiyo talent yake na vitu alivyokuwa anafanya na aina ya ushairi na uwakilishi wake ni vitu ambavyo vilikuwa na ubora na upekee zaidi," anasema.

Hata hivyo, anakumbushia namna ambavyo lebo na studio zilivyokuwa chache kwa miaka hiyo ya nyuma.

"Wote tulivyokuwa tunatoka na tukapata nafasi ya kujulikana na kupata sifa ya kuitwa wasanii wazuri ndoto yetu ilikuwa wengi wapate nafasi ya kusikika na wengi sasa hivi tunaona wakiwa wamepata.

"Watu wengi wanapata nafasi ya kujulikana ni juu yao kuweza ku-maintain hiyo nafasi ya kujulikana na kuboresha uandishi wao na production nadhani hata yeye pia anafurahi huko aliko kuona kwamba wanamuenzi vizuri na wengi wanamzungumzia na kujikuta wanataka ku-rap kama yeye kwenye positive way,"anasema.

Kipi watu wajifunze kutoka kwa Mangwea?

"Alikuwa mtu ambaye hakuwa anaishi maisha ya u-super star alikuwa ni rafiki wa kila mtu na hiyo ndiyo hali ambayo wasanii wa sasa hivi na vijana ambao wanachipukia kwenye sanaa wanatakiwa wajifunze na kujua kwamba huyo Ngwea ambaye wanasema wanampenda ni mtu ambaye hakuwa na fake alikuwa so real.

"Kama alikuwa anataka kupanda daladala alikuwa anapanda, kama kutembea alikuwa anatembea kama bodaboda alikuwa ni mtu ambaye hakuwa anachanganya kati ya Ngwea na Albert ambaye ni msanii hicho ndicho kitu ambacho mimi na wengine tunatakiwa kujifunza na kukienzi",anasema.

Utakumbuka kuwa msanii huyo alifariki dunia 28, Mei 2013 na kuzikwa Juni 6, 2013 kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Monica eneo la Kihonda, nje kidogo ya Morogoro.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post