Nakumbuka kisa hiki nilikutana nacho siku moja majira ya asubuhi.
Nilikuwa nimepanda daladala kutoka Gongo la Mboto kuelekea Posta kibaruani kwangu.
Wanaonijua wanaweza kujiuliza imekuwaje nimelala Gongo la Mboto badala ya nyumbani kwangu Temeke Mikoroshini Kwa Mpelumbe. Msije nitoa roho bure, wala sikulala kwa nyumba ndogo, bali nilikuwa nimelala matanga kwenye msiba wa baba wa rafiki yangu.
Nilipata siti, hasa ukizingatia kwamba, ilikuwa ni asubuhi na usafiri katika viunga hivyo ni wa kugombea kutokana na uwingi wa wakaazi wa maeneo hayo ukilinganisha na idadi ya daladala.
Sikumbuki hasa ilikuwa ni kwenye kituo gani, bali ilikuwa ni katikati ya safari.
Awali nilidhani ni mzaha, lakini kadiri mambo yalivyokuwa yakienda, nilijua kwamba, haukuwa mzaha. Ni kwamba jamaa mmoja mwanaume ambaye alikuwa amekaa kiti kimoja kutoka kile cha nyuma alikuwa akiongea kwa simu. Kuongea na simu haikuwa tatizo, wala jambo la ajabu, lakini alichokuwa akiongea labda kilikuwa cha ajabu.
Ni kwamba jamaa huyu alikuwa akibwata, badala ya kuongea. Kwanza alikuwa akiongea kwa kelele sana na pia alikuwa akiongea mambo ambayo naweza kusema kuwa ni ya ajabu na kukera pia.
Inaonekana huyo mtu aliyekuwa akimwongelea alikuwa amemkera sana.
‘Nani alimwambia aje, kwani tulimwita. Wewe mtu anakomba mboga kiasi kile nani atakubali . Mtu anajua kabisa usawa wenyewe ulivyo lakini anakula kama yuko kijijini, mimi alinikera sana.'
Halafu aliendelea bila kujali.
‘Unajua nini? Niliona tangu mwanzo kabisa wakati msosi unawekwa, nikajua hapa kuna shughuli. Nasikia ndivyo alivyo. Wanasema, hata kule kwa uncle alifukuzwa kwa sababu ya kula. Mimi aliniudhi sana.
Halafu aliendelea
‘Kuna yule mdogo wake, naye hivyo hivyo. Kuna siku aliniabisha kweli ukweni, Kipalang'anda. Tulienda kuwaona tukapewa msosi. Nakwambia, tonge-nyama ile mbaya, hadi mkwe wetu akaguna. Nadhani kwenye familia yao wana tatizo la kula kiaina'
Halafu ilionekana kama vile mada ya kula ilikuwa imeisha. Ghafla ikazuka mada nyingine.
‘Sikumpa, naona alichukua mwenyewe. Ukiweka nguo tu lazima atazivaa. Kuna ile chupi yangu ya Boxer ya rangi ya samawati, ile nilinunua siku ile wakati tunapita mtaa wa Narung'ombe Kariakoo, basi hiyo hiyo'
Abiria walianza kuvutiwa na sauti ya abiria huyo ambaye kwa huku mjini tunasema alikuwa ameulamba, yaani kavaa vizuri.
‘Basi siku hiyo naitafuta niivae siioni. Usiku naona mtu kaitinga. Kwa kweli sikumsemesha, niliamua kumziria. Hebu fikiria, mtu atachukua vipi chupi ya mwanaume mwenzake..!'
Huyu abiria alikuwa anaonekana kabisa kwamba, amejisahau kupita kiasi.
‘Dawa yake ni moja tu, ni kumwambia kwamba hapa mjini hana nafasi'.
Hivi ushawahi kuliona likimega matonge, yaani dizaini ya kijijini jijini kabisa. Kwa kweli kuna siku nilikuja na mheshimiwa wetu yule, aliniangusha sana. Wewe mtu unakula, mamchuzi yanadondokea hadi kwenye viwiko na kila mahali, ndiyo nini.
Nilicheka siku ile ya msiba wa (Anataja jina ), aisee aliadhirika kweli. Kaingia kwa wapishi kaibuka na finyango. Kumbe ya moto bwana, ile anaitia mdomoni, kutoka anakutana na msafara wa kusindikiza maiti, ikabidi aiteme mbele ya watu'
Halafu alitulia kidogo, ilionekana kama huyo mwenzake alikuwa kizungumza.
‘Ni kweli kama mtu anaweza kumega mitonge kama ile ni kwa nini ashindwe kujitegemea. Kajitu kadogo hata mkononi hakajai, lakini kanakula kama vile kametoka Dafur'
Abiria waliangua kicheko mle ndani ya daladala baada ya jamaa kutoa kauli ile. Abiria yule alishtuka na kutazama pande zote akakutana na macho ya abiria wote wakimwangalia. Jamaa alishtuka sana, na inaonekana wazi kwamba alikuwa amejisahau.
Alizima simu hapo hapo na basi lilipofika kituo kilichofuata alishuka huku uso wake ukiwa umesawajika kwa aibu kubwa. Sina uhakika kama alikuwa amefika mwisho wa safari yake maana alishukia pale njia panda ya Kitunda.
Huku nyuma abilira walicheka sana , akawa ameacha mjadala kwenye daladala kila mtu akisema lake kuhusu yale mazungumzo ya jamaa kwenye simu.
Leave a Reply