Mtayarishaji muziki kutoka Marekani ambaye amewahi kufanya kazi na mastaa kama Kanye West amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 54.
Taarifa ya kifo chake imetolewa kupitia ukurasa wa Instagram wa ‘Def Jam Recordings’ huku ikieleza mchango wake katika tasnia ya muziki wa Hip Hop nchini Marekani.
“Def Jam Recordings na familia ya wasanii, viongozi na wafanyakazi wa Def Jam, wanasikitika sana kwa msiba wa Irv Gotti. Mchango wake katika Def Jam, kama mtendaji wa A&R na kupitia ushirikiano na Murder Inc, ulisaidia kufungua njia kwa kizazi kijacho cha wasanii na watayarishaji, na kuwa nguvu iliyoleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya hip-hop na R&B.
"Uwezo wake wa ubunifu na kujitolea kwa dhati ulizalisha nyimbo nyingi maarufu, ambazo bado zinavuma ulimwenguni kote. Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu,” imeeleza taarifa
Aidha kwa mujibu wa chanzo cha karibu cha Gotti kimeeleza kuwa mtayarishaji huyo alifariki dunia jana Jumatano Februari 5, 2025 huku sababu ya kifo chake bado haijawekwa wazi lakini kuna taarifa kuwa alikuwa akisumbuliwa na kiharusi toka mwaka jana.
Katika moja ya mahojiano yake aliyowahi kufanya hapo nyuma kiongozi huyo wa Murder Inc. Records aliweka wazi ugonjwa wake wa kisukari akisema kuwa hakuwa mwangalifu katika kutumia Insuli kwa makini huku madaktari wakimshauri zaidi kuboresha lishe yake.
Mbali na Kanye mtayarishaji huyo aliwahi kufanya kazi na mastaa mbalimbali akiwemo DMX, Jay-Z, Vanessa Carlton, Ja Rule, Ashanti, na wengineo.
![Irv Gotti Afariki Dunia](https://mwananchiscoop.co.tz/public/uploads/2025/02/06/fr95d184fe892b04705975f7945fa6c0d451a8b3ed.jpeg)
Leave a Reply