Baada ya kusambaa kipande cha video kinachowaonesha wanafunzi wa shule za msingi wakicheza wimbo wa msanii #Zuchu 'Honey' wilayani Tunduma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameagiza walimu wakuu wa shule hizo wavuliwe vyeo.
Amesema hayo jana Novemba 2, 2023 nje ya Bunge jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu video hiyo ambapo pia amepiga marufuku wanafunzi kucheza nyimbo zisizo na maadili na kuwataka walimu kuwa wasimamizi wa maadili pindi wanafunzi wawapo shuleni.
"Tumeshatambua shule yenyewe iko Tunduma, kulikuwa na kikundi kimeenda kutoa msaada shuleni pale, baada ya kutoa msaada ule kikaweka na muziki halafu wanafunzi wakacheza, na maudhui ya muziki wenyewe kila mtu ameusikia sina haja ya kuurudia.
Tumeongea na wadhibiti ubora wapeleke taarifa kule, mkurugenzi awaondoe walimu wakuu wa shule mbili; moja shule ya Tunduma na nyingine ambazo ni kama shule pacha, waondolewe madaraka ya ukuu wa shule watafutwe wakuu wengine wa shule. Tunafanya hivi ili kutuma ujumbe, walimu wakuu tusaidieni msiruhusu vitu kama hivi viingie mashuleni," amesema Profesa Mkenda.
Leave a Reply