Hizi hapa Teknolojia zitakazobamba 2024

Hizi hapa Teknolojia zitakazobamba 2024

Dar es Salaam. Umewahi kuwaza kwamba ukuaji wa kasi wa teknolojia unaoshuhudiwa dunia ya leo, unazidi kugusa maisha yetu kadri siku zinavyokwenda?

Inaelezwa lengo la kukua kwa mfumo mzima wa teknolojia ni kurahisisha kazi na maendeleo kwa ujumla. Kutokana na ukuaji wake inamlazimu kila mtumiaji kujifunza kwakuwa hata teknolojia zenyewe zinabadilika kila wakati.

Kupitia utafiti mdogo uliofanywa na Mwananchi Digital leo inakuletea teknolojia zinazoshika kasi mwaka huu ambazo pia kwa namna moja au nyingine zinatumika nchini.

Teknolojia ya Akili Bandia

 

Akili bandia ni nadharia na uundaji wa mifumo ya kompyuta wenye uwezo wa kufanya kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya kibinadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha.

Kupitia Akili Bandia imewezesha kompyuta kuzalisha teknolojia ya kisasa, iliyoleta mapinduzi sekta mbalimbali kwa kuwezesha kuunda maudhui ambayo yanafanana na kazi inayofanywa na binadamu.

Malengo ya akili bandia ni pamoja na kuiga shughuli za utambuzi wa binadamu, akili ya mwanadamu inaweza kufafanuliwa kwa njia ambayo mashine inaweza kuiiga kwa urahisi na kutekeleza majukumu.

Matumizi ya akili ya bandia hayana mwisho. Teknolojia hiyo inaweza kutumika kwa sekta na tasnia nyingi tofauti ikiwemo tasnia ya huduma ya afya kwa kutambua, kusaidia katika taratibu za matibabu.

 

Tovuti ya Simplilearn inasema ubunifu wa siku zijazo unafikiriwa kujumuisha upasuaji kwa kutumia roboti unaosaidiwa na Akili bandia vilevile kudumisha na kufuatilia rekodi za matibabu.

Vilevile inatumika katika biashara mtandao, utambuzi wa sura, michezo, magari yanayojiendesha, hata kuchakata lugha kupitia programu saidizi kama ChartGPT pamoja na utambuzi wa ramani.

Akizungumzia teknolojia hiyo Evelyne Peter kutoka Dar es Salaam amesema kwa ulimwengu wa sasa hazikwepeki kwakuwa ndipo dunia inapoelekea.

Amesema kwa upande wake anatumia ChatGpt na ni nzuri kwa kumsaidia pale kazi yake inapohitajika na muda umeisha lakini anakiri kuwa inapunguza uwezo wa kufikiri.

“Akili bandia inapunguza uwezo wa binadamu kufikiria kwasababu sikuhizi kitu kidogo tu unakimbilia kwenye chatgpt inakuandikia mada yeyote unayotaka,” amesema.

Mathalani anasema changamoto iliyopo katika teknolojia hizo ni uelewa kwa baadhi ya watu kuzifahamu.

 

Uhifadhi taarifa ‘Datafication’

Uhifadhi taarifa ni aina ya teknolojia inayohusisha mchakato wa kubadilisha vipengele vinavyotumika katika maisha kuwa vifaa au programu inayoendeshwa na mtandao.

Hii hutumika kuanzia kwenye simu, mashine, programu za ofisini hadi vifaa vinavyotumia akili bandia, ambapo taarifa hizi hukaa kwa muda mrefu.

 

Kwa hivyo, ili kuhifadhi taarifa kwa usahihi na kwa usalama uhifadhi taarifa imekuwa taaluma inayohitajika sana katika maisha na uchumi wa sasa.

Katika hili faida yake ni kuhitaji wataalamu wa Tehama, wanasayansi wa data, wahandisi, mafundi pamoja na wasimamizi.

 

Teknolojia ya uhalisia ‘Virtual Reality’

Teknolojia hii mara nyingi hutumika kwenye michezo au kutazama filamu kama wengi wanavyodhani lakini ukweli inatumika hata kwenye elimu.

Teknolojia hii pia imekuwa ikitumika katika mafunzo mfano programu ya ‘VirtualShip’, inayotumika kutoa mafunzo kwa manahodha wa meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani.

Mbali na mafunzo ya manahodha lakini teknolojia hii inaweza kutumika kuwafunza madaktari kufanya upasuaji.

Sio Marekani tu hata Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa sasa kinatoa mafunzo ya fani ya matengenezo ya ndege kwa njia hiyo ya kidijitali hatua ambayo ilipongezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alipofanya ziara chuoni hapo Septemba mwaka jana. 

Hata hivyo, Tovuti ya Simplilearn inasema mwaka huu kunatarajiwa kuwa aina hizi za teknolojia zikaunganishwa zaidi katika maisha ya kila siku.

 

Vifaa janja ‘Smart Devices’

Kupitia Akili Bandia ambayo imekuwa na jukumu muhimu katika kufanya ulimwengu kuwa rahisi sio tu kuiga wanadamu bali kwenda mbali zaidi ili kufanya maisha yasiwe na usumbufu.

Kupitia hilo teknolojia imeendelea kuzalisha vifaa bora ambavyo vipo na vinazidi kushika kasi vyenye lengo la kurahisisha pale penye ugumu.

Vifaa hivyo ni kama roboti saidizi za nyumbani za akili bandia, Kamera za ulinzi, runinga janja. Takribani kila sehemu inahitaji programu mahiri za namna hii.

 

5G

Baada ya teknolojia za intaneti za 3 na 4G kuwezesha matumuizi ya mtandao kwa njia rahisi sasa mtandao uliopo ni 5G.

Inawezekana isiwe ngeni kwa baadhi ya watu lakini ukweli ni hudumaya 5G inatarajiwa kuleta mapinduzi katika maisha ya sasa.

Hii inatokana na matumizi ya teknolojia kwa ujumla kutumia huduma ya mtandao hivyo 5G ni huduma itakayotumika nyanja mbalimbali ikiwemo viwandani hata kwenye kampuni.

Hapa nchini baadhi ya mitandao ya simu imezindua hivi karibuni huduma ya 5G ikionesha taswira kuwa teknolojia hiyo ipo nchini.

Blogu maarufu ya teknolojia iitwayo Digi imesema kwa upande wa teknolojia ya 6G yenyewe inatarajiwa kuanza kutumiak kibiashara ifikapo mwaka 2030.

Mdau wa teknolojia, Essa Mohamedali Mwanzilishi mwenza wa Tanzania AI Lab & Community anasema bado kuna changamoto nyingi tunazokabiliana nazo kimatumizi kama taifa ikilinganishwa na nchi nyingine.

Katika kufanikisha hilo Mohamedali amesema kunahitajika vipaji pamoja na vijana wenye ujuzi zaidi. “Tunahitaji miundombinu, lakini pia tunahitaji uwekezaji na ufadhili ili kujenga zaidi,” amesema.

Amesema pia kama taifa inahitaji kujua na kutambua ni sekta gani zinaweza kufaidika na teknolojia hizi mara moja ili kuunga mkono ajenda na vipaumbele.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post