Head Master, Afunguka wachekeshaji wa zamani kukosa soko, Amtaja Joti

Head Master, Afunguka wachekeshaji wa zamani kukosa soko, Amtaja Joti

Na Aisha Charles

Ni wazi kuwa baadhi ya vijana wameendelea kujipatia umaarufu na kipato kupitia sanaa ya vichekesho, kati ya vijana hao walionyakuwa fursa katika upande huo ni  Abdul Hussen Chacha maarufu kama Head Master ambaye amesema katika harakati za kujitafuta aliwahi kukosa pesa ya kodi kwa sababu ya kulinda sanaa yake.

“Ugumu wa maisha ulinifanya nipitie mengi ilifikia kipindi nilitumia pesa yangu ya kodi kwa ajili ya kufanyia nauli ya kwenda location, mama mwenyenyumba alichukua uamuzi wa kuchukua vitu vyangu vya ndani kufidia kodi yake,” anasema.

Hata hivyo anasimulia kuwa kabla ya kuingia kwenye sanaa alikuwa dereva wa bodaboda mkoani Mwanza

Rafiki zake hawakuamini anachofanya

Kwenye kutafuta mafanikio au kupambania ndoto ni kawaida kukutana na baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kukatisha tamaa ambapo Head Master ameeleza kuwa marafiki zake walikuwa mstari wa mbele kumtaka aachane na sanaa.

 “Washikaji niliokuwa nao walikuwa hawapendi sanaa yangu waliniona napotea, japo kuna kipindi maneno ya watu yanaweza kuharibu unachotamani kufanya,”amesema.

Hata hivyo ameeleza kuwa kati ya hao waliotamani aachane na sanaa walikuwepo baadhi waliotamani afike mbali kupitia sanaa.

“Unajua kwenye msafara wa Mamba na Kenge hawakosi kupitia kikundi changu cha bodaboda ambao walikuwa wanatumia muda mwingi kuisema sanaa yangu kuna watu wawili wa tatu walikuwa wakiniunga mkono katika kila ninachofanya huku wakisema ipo siku nitatoboa,” amesema.

Alivyopata mchongo usalama barabarani

Safari moja huanzisha nyingine hivi ndivyo tunavyoweza kusema kwa mchekeshaji huyu ambaye sanaa ya vichekesho ilifanya apate mchongo kufanya kazi na Jeshi la Polisi, kama balozi katika kuelimisha jamii kuhusu usalama barabarani kwa njia ya kuchekesha.

“Leo hii kuaminika mpaka kufanya kazi na Jeshi la Polisi ni kwa sababu ya sanaa yangu, ni kitu kikubwa ambacho kimenifunza kupanga mambo makubwa ya kuelimisha jamii kupitia ninachofanya,” amesema na kuongezea

“Rai yangu kwa wasanii wenzangu tusiishie kuchekesha pia tuelimishe jamii kupitia tunachofanya kwa sababu, jamii inatuangalia kwani tunaweza kumpotosha mtoto wa mtu pia tunaweza kumuelimisha,” amesimulia.

Wachekeshaji wa zamani kukosa soko kwa sasa

“ Unajua katika sanaa, watu wanashindwa kujua kuwa kila kitu kina wakati wake na ndiyo maana kumekuwa na ushindani mkubwa hususani kwenye sanaa ya vichekesho kwa hiyo huwezi kulinganisha  ubora aliokuwa nao mchekeshaji wa zamani na wa sasa, huyo wa zamani alikuwa anafanya kwa nafasi yake wa sasa pia nafanya kwa nafasi yake .

 “Naamini zamani kulikuwa na generation ambayo ilikuwa inakubali kazi za kina Joti, Mpoki na wengine wa zamani lakini, kwa sasa kuna kizazi kinaamni komedi ya sasa kwa hiyo point yangu inakuja pale ubora wa kitu unatokana na wakati huo,” amesema.

Anawazungumziaje wachekeshaji wakongwe?

Aidha Head Master ameeleza kuwa kuna wasanii wa zamani mpaka leo wapo katika hits wanafanya vizuri kupitia kufanya ubunifu, kuendana na mazingira na bado kazi zao zinaishi akimtolea mfano mchekeshaji maarufu Joti.

“Kuna wasanii wa vichekesho mpaka leo kazi zao zinaishi tuchukulie mfano Joti mpaka leo ile style yake ya kujigeuza kuwa babu, kuwa mwanamke bado watu wanapenda hivyo anaishi kupitia hivyo na watu bado hawajamchoka kwa sababu wanaendelea kumfatilia,”amesema.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post