Aloooh! Haya wale wavivu leo nimekuja na kiboko yenu, msipoacha mwaka huu mniite mbwa, niko nimekaa pale. Leo bwana katika kazi nimekujia na makala ambayo itakusaidia wewe katika kuondoa uvivu na uchovu pindi uko kazini.
Maarifa ni njia moja wapo ya kufanikiwa katika kila jambo unalofanya, iwe ni biashara au kazi, lakini kuna wakati tunajikuta katika hali ya kuchoka na kushindwa kufanya yale tunayotarajia kuyafanya.
Hali hiyo hutafsiriwa kama uvivu wa kutokufanya kazi fulani kwa muda ambapo husababisha mipango iliyopangwa isifanyike kwa wakati husika au isifanyike kabisa.
Kama uvivu utapewa nafasi kubwa katika shughuli za kikazi na biashara nk, basi unajenga tabia ambayo ikiota mizizi inaathiri kabisa mwenendo wa kazi na mpangilio kwa ujumla. Huenda na umekuwa ukijiuliza kwanini mambo yako hayaendi, basi jua kabisa una ugonjwa wa uvivu ambao utakurudisha nyuma kimaendeleo na kukufanya usifanikiwe maisha yako yote.
Fanya haya kuepuka uvivu katika shighuli zako.
Kamilisha kazi kwa wakati
Acha tabia ya kuairisha kazi uliyoanza kuifanya, kama utaendelea kuairisha ukidhani una muda mwingi wa kuifanya, utajikuta unaingiwa na uvivu na matokeo yake itajengeka tabia ndani yako ya kushindwa kukamilisha kazi kila unapoanza. Hivyo basi, ili mtu aondokane na kuahirisha mambo ni lazima atumie muda wake vizuri na kuigawanya kazi katika vipengele ili kufahamu itatumia muda gani kuikamilisha.
Ongeza ubunifu
Mafanikio ya kibiashara au kazi hutegemea zaidi uwezo wako wa kubuni mambo mapya ili kuboresha utendaji kazi wa kila siku na kuongeza tija. Epuka mambo yale yale kila siku, akili inachoka na kuzoea na kujenga tabia ya uvivu kwa kua kila siku unafanya kitu kimoja kinacho jirudia.
Ichangamshe akili kwa kufanya tofauti na ulivyozoea ili kuiamsha kutafuta namna ya kuendana na mabadiliko katika maisha yako ambapo itakuongezea nguvu ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa so unatakiwa kufanya kazi kwa bidii kuacha alama.
Wachunguze marafiki zako
Marafiki wana nafasi kubwa ya kukukwamisha au kufanikisha katika Maisha. Chagua marafiki wachapa kazi ambao wakati wote watakuhimiza kufanya kazi na kutekeleza mipango yako.
Tengeneza mtandao wa marafiki wanaopenda kujifunza, hii itakusaidia sana pindi utakapokuwa unatumia muda nao kwa sababu utaona namna wanafanya kazi kwa kujituma, utavutiwa nawe utahamasika na kuacha uvivu.
Weka malengo ya maisha
Acha kuishi bila mpangilio, fahamu hakika nini kusudio la maisha yako, weka vipaumbele na wekeza muda na nguvu zako katika kutekeleza. Kukosa malengo ama uelekeo wa maisha ni njia mojawapo ya kukaribisha uvivu ambao utakukudimiza kabisa.
Usiishie tu kujiwekea malengo lakini bali panga namna ya kuyatekeleza kwa awamu kwa kujikumbusha mara kwa mara. Hii itakuwasaidia kukuondolea uvivu katika mwili wako. Pale unapokuwa na malengo katika maisha huwezi kuwa mvivu, utakuwa unajituma kuhakikisha unafanikisha malengo yako hayo. Lakini pia hakikisha unajikumbusha malengo yako kila siku ili upate nguvu ya kuyafanya na usijisahau.
Jenga mazoea ya kufanya mazoezi
Kuna wakati unakuwa unahisi kuchoka katika kazi unayofanya. Kama uko ofisini, simama na fanya mazoezi ya kujinyoosha au toka nje ya ofisi pata upepo kidogo alafu rudi ndani hii itakupa nguvu nyingine na ari ya kufanya kazi yako.
Kama uko nyumbani, punguza kukaa muda mrefu na kuangalia televisheni badala yake fanya matembezi ili kupata hali tofauti na uliyozoea nyumbani. Hii itakusaidia kujifunza vitu vingi njiani ikiwemo kukutana na watu wapya wenye mawazo chanya.
Leave a Reply