Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa Marburg

Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa Marburg

Mark Lewis

Hivi karibuni waziri wa afya, jinsia na ustawi wa jamii, Ummu Mwalimu alithibitisha watu watano kati ya wanane kufariki dunia kutokana na
ugonjwa wa virusi vya homa ya Marburg katika mkoa wa Kagera

Kabla ya kuthibitisha kwamba ni homa ya Marburg, kulizuka sintofahamu kubwa kutokana na kutajwa kuwa ni ugonjwa usiojulikana na baadhi ya watu walianza kuuhusisha ugonjwa huo na ugonjwa wa ebola ambao uliua maelfu ya watu katika nchi jirani ya DRC na kusambaa katika nchi ya Uganda.

Ugonjwa huu unaoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu unatajwa kutokuwa na tiba bali hutibiwa kwa dalili husika anazokuwa nazo mtu.

Hili linaufanya ugonjwa huu kuwa hatari kama magonjwa mengine ya mlipuko yasiyo na tiba ya moja kwa moja.

Ungana nasi kujua Zaidi kuhusiana na ugonjwa huo…

Homa ya kuvuja damu (kwa Kiingereza: Marburg hemorrhagic fever au Marbur virus disease) ni ugonjwa mkali wa wanadamu na wanyama kama vile tumbili, nyani, sokwe, ambao husababishwa na virusi vya Marburg vya aina mbili.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt. Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Na miongoni mwa wanadamu, huenezwa zaidi na watu ambao wamekaa kwa muda mrefu katika mapango na migodi iliyo na popo.

Milipuko mikubwa ya ugonjwa wa Marburg virus kuwahi kutokea.

2017, Uganda: visa vitatu, watu watatu walifariki

2012, Uganda: visa 15, watu wanne walifariki

2005, Angola: visa 374, watu 329 walifariki

1998-2000, DR Congo: visa 154 cases, watu 128 walifariki

1967, Ujerumani: visa 29, watu saba walifariki

Chanzo: WHO

Ugonjwa huu husababishwa na maambukizi ya Virusi vya Marburg vyenye sifa ya RNA kutoka familia ya Filoviridae. Virusi vya ugonjwa huu hupatikana katika familia moja na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola.

Njia Za Maambukizi Za Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Kwa mara ya kwanza, binadamu hupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu kutoka kwa wanyama hasa popo, kwa kula au kugusa mzoga wake.

Mara mtu anapopata maambukizi hayo kutoka kwa mnyama, maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu kati ya binadamu na binadamu mwingine huanza kutokea kupitia mguso wa moja kwa moja.

Virusi vya Marburg vinaweza kupenya na kuingia mwilini kupitia sehemu za wazi kama vile vidonda, au kupitia ngozi laini za sehemu ya macho, midomo na pua kutoka kwenye;

Damu au majimaji ya mwili kama vile Mkojo, mate, jasho, choo, matapishi, maziwa na shahawa.

 

  • Vifaa vilivyoguswa na majimaji kutoka kwenye mwili wa mgonjwa, au mtu aliyefariki kwa ugonjwa huu kama vile matambara, nguo, shuka, viwembe pamoja na sindano.
  • Kwa kushiriki tendo la ndoa kwa namna yoyote na binadamu aliyeambukizwa ugonjwa huu. Taarifa za kina kuhusu njia hii hazipo wazi sana, lakini inafahamika kuwa virusi vya Marburg huwa na uwezo wa kubaki kwenye korodani za mwanaume kwa siku kadhaa baada ya kupona kama ilivyo kwa virusi vya Ebola. 

Kutokana na njia ambayo ugonjwa huu huambukizwa, wahudumu wa afya na watu wengine wanaohudumia wagonjwa na marehemu wenye changamoto hii ikiwemo ndugu huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi.

Dalili za ugonjwa wa Marburg

Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Marburg huanza ghafla kwa homa kali, maumivu makali ya kichwa pamoja na maumivu ya misuli. Dalili zingine ni pamoja na;

Dalili za ugonjwa wa Marburg zimegawanyika hutokea katika majira tofauti. Zipo dalili za mwanzoni, mara tu baada ya maambukizi na zipo zinazotokea baadaye. Dalili za mwanzoni ni pamoja na;

  • Homa
  • Mwili kuishiwa nguvu
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Maumivu ya misuli
  • Macho kuwa mekundu
  • Vidonda vya koo
  • Vipele vya ngozi
  • Maumivu ya tumbo.

Dalili za baadaye ni pamoja na;

  • Kutokwa na damu puani na mdomoni
  • Kutokwa na jasho
  • Kutapika damu
  • Kuhara damu.

 

Matibabu Ya Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Ugonjwa huu hauna tiba ya moja kwa moja isipokuwa kushughulikia dalili zinazoonekana kwa wakati huo. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa virusi vya Marburg huwa na hadi 88% ya uwezekano wa kusababisha kifo.

Jinsi ya Kujikinga na Ugonjwa wa virusi vya Marburg

Pamoja na kuonekana mara chache sana kwa binadamu, ugonjwa huu unaweza kuambukiza kirahisi hasa kwa watumishi wa afya wanaohudumia wagonjwa pamoja na ndugu wa karibu wanaoishi na kutoa huduma kwa mtu mwenye ugonjwa huu.

Aidha, watu wanaotoa huduma kwa mgonjwa wanapaswa kuvaa vifaa maalumu vya kujikinga mfano gloves, gauni maalumu na barakoa, kumtenga mgonjwa kwenye eneo lililodhibitiwa pamoja na kutakasa au kuangamiza kikamilifu masalia ya vifaa alivyotumia mgonjwa vyenye sifa ya kubeba vimelea ya ugonjwa. Zifuatazo ni baadhi ya njia za kujikinga na ugonjwa wa Marburg

  • Epuka kugusa maji ya mwili wa mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg mfano damu, mate, jasho, matapishi, mkojo, na kinyesi.
  • Epuka kugusana na mtu mwingine mfano kusalimiana kwa kukumbatiana, kupeana mikono au kubusiana.
  • Epuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa wa Marburg bila kutumia vifaa kinga.
  • Epuka kugusa au kula mizoga mfano popo, nyani, tumbili au swala wa msituni.
  • Wahi au muwahishe mtu mwenye dalili za ugonjwa huu wa Marburg katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kuepuka kueneza maambukizi katika jamii.
  • Nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara. 

Endapo umebainika na moja ya dalili kama za ugonjwa wa Marburg toa taarifa haraka katika kituo cha afya.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags