Fahamu mazoezi yanayoboresha tendo la ndoa

Fahamu mazoezi yanayoboresha tendo la ndoa

Dk Anold Kegel ni mwanasayansi wa tiba bingwa wa magonjwa ya wanawake wa Marekani na mgunduzi wa mazoezi yajulikanayo Kegel, yenye kuboresha tendo la ndoa kwa wanawake.

Uzoefu mkubwa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya kwa wanawake kulimwezesha kubaini udhaifu wa misuli ya kitako cha kiuno, kwa wanawake waliotoka kujifungua.

Wazo lake hilo ndilo lilimfanya kugundua mazoezi hayo ambayo yanachangia kuboresha afya ya uzazi kwa upande wa tendo la ndoa.

Kiujumla ni kuwa mazoezi mepesi yote yana mchango mkubwa kwa mwanadamu katika afya ya uzazi, ikiwamo kusaidia kuimarika kwa vichochezi muhimu vya uzazi kwa wanaume na wanawake.

Kwa Dk Kegel alilenga moja kwa moja kwa yale mazoezi ambayo yanaimarisha misuli ya kiunoni, ambayo ndiyo huboresha tendo la ndoa, hatimaye kufanyika kwa ufanisi.

Pia alikuja na kifaa na mazoezi yanayosaidia kukabiliana na tatizo la kushindwa kuzuia mkojo.

Na hii ndiyo sababu kubwa mazoezi haya yakaitwa mazoezi ya Kegel, ambayo tafiti za kitabibu zinayathibitisha kusaidia kuimarika kwa tendo la ndoa kwa wanawake.

Sababu ni kutokana na mazoezi haya kusaidia kuimarisha nguvu ya misuli muhimu ya kitako cha kiuno, ambayo ina athari chanya katika kufanyika kwa tendo la ndoa.

Kutokana na matukio yanayomkuta mwanamke, ikiwamo wakati wa kujifungua, upasuaji, ajali za kiuno, umri mkubwa, shambulizi la magonjwa na unene huweza kudhoofisha misuli.

Misuli hii iko katika kiuno ndani, ndiyo ambayo huipa egemeo ili kushikilia nyumba ya uzazi, kibofu cha mkojo, uke na eneo la mwisho la mfumo wa chakula.

Kuimarika kwa misuli ya eneo hili na kuwa na nguvu husaidia kuongeza msisimko wa kilele cha mapenzi kwa wenza wote wawili, kwani misuli hiyo huikandamiza na kuibana misuli ya uke kwa ufanisi.

Pia ni vizuri kwa ujumla kufanya mazoezi yale mapesi, ikiwamo kutembea, kukimbia kasi ya wastani, kuogelea, kucheza mziki, kuendesha baiskeli, kuruka kamba na mazoezi mchanganyiko ya Gym ili kuboresha afya ya mwili.

Mazoezi kama haya yanasaidia kuboresha kiwango cha vichochezi vya uzazi, hivyo kuboresha afya ya uzazi, ikiwamo kumsaidia mwanamke kuwa na mzunguko usioyumba.

Kwa kawaida mazoezi ya Kegel huhitajika kufanyika wakati kibofu cha mkojo kikiwa kitupu na huku ukiwa umelala chali chini, eneo ambalo lina ugumu wa wastani tu ili kukufanya usione karaha.

Unaweza kuchagua eneo lolote ambalo kwako itakuwa ni burudani kulifanya, ikiwamo nyumbani chumbani, ofisini, katika vyombo vya usafiri. Zoezi hili huweza kulifanya bila mtu mwingine kubaini unachokifanya.

Zoezi hili hufanyika kwa kuikaza misuli ya kitako cha kiuno na ushikilie hivyo kwa muda wa sekunde 3 hadi 5.
Baada ya muda huo kupita acha kuikaza na tulia ili kuilegeza. Rudia kufanya hivyo kwa mara 10 na ufanye mzunguko huo mara tatu kwa siku au kila baada ya saa 8 yaani asubuhi, mchana na jioni.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags