Fahamu kuhusu ugonjwa wa Hernia

Fahamu Kuhusu Ugonjwa Wa Hernia

Na Aisha Lungato

Hernia ni uvimbe (eneo lililotuna) kutokana na viungo vya ndani ya mwili kusukuma kuta za misuli inayozunguka au kushikilia viungo hivyo.

Hernia hutokea wakati kuna udhaifu au kuna tundu kwenye kuta za misuli inayoshikilia na kuviweka viungo vya tumbo (peritoneum) kwenye sehemu yake.

Udhaifu huo unaweza kuviruhusu viungo vya ndani kusukuma na kupenyeza, na kujenga eneo lililotuna. Unaweza kuwa na hernia ikiwa unaweza kuhisi namna ya eneo laini lililotuna kwenye maeneo ya tumbo au kinena au kwenye kovu ambalo lilitokana na upasuaji.

Eneo hili lililotuna linaweza likapotea ukiminya sehemu hiyo au ukijilaza. Unaweza kupata maumivu kwenye eneo hilo hasa ukikohoa, ukiinama au ukinyanyua kitu kizito.

Hernia ni tatizo linalowasumbua watu wengi katika nchi nyingi duniani.

Hernia mara nyingi hutokea kwenye maeneo ya tumbo, lakini huweza pia kutokea kwenye sehemu ya juu ya mapaja, kwenye kitovu, na kwenye maeneo ya kinena. Hernia haihatarishi maisha mara moja, lakini haiwezi kuondoka yenyewe na inaweza kuhitaji kufanyika kwa upasuaji.

Hernia mara nyingi hupewa majina kutokana na sehemu ya mwili inapojitokeza, ingawa mara nyingine majina huweza kutolewa kutokana na sababu nyingine za kuitambulisha.

Kila hernia hutibiwa tofauti na nyingine kutokana na sehemu iliyopo na sababu nyingine za kitaalamu. Kuwa na elimu ya kutosha ya kila aina ya hernia itakusaidia kujua namna ya kutoa maamuzi sahihi ya tiba yake.

Aina Za Hernia

  1. Inguinal (groin hernia)

Inguinal hernias au groin hernias hutokea pale utumbo au mafuta yanaposukuma na kupenya kwenye misuli ya eneo la kinena. Hii ndiyo aina ya hernia inayowasumbua watu wengi zaidi.

Inguinal hernia inaweza kuonekana kwa wanaume na wanawake lakini huwapata zaidi wanaume kwa sababu tayari wana kijitundu kidogo kwenye misuli ya kinena kwa ajili ya kupitisha arteri, veni na mrija wa mbegu vinavyoelekea kwenye korodani. Asilimia 97 ya aina hii ya hernia huonekana kwa wanaume.

Hernia inaweza kuwa juu ya misuli ya tumbo (direct inguinal hernia) au inaweza ikafuata njia ya mrija wa shahawa pale unapoacha eneo la tumbo na kuelekea kwenye korodani (indirect inguinal hernia).

Inguinal hernia huanza kama uvimbe mdogo ambao huongezeka na muda. Uvimbe unaoonekana ni utumbo au mafuta yanayosukuma misuli.

Uvimbe huweza kupotea kwa kulala na kurudi mwili ukianza shughuli. Uvimbe huu ukiwa mkubwa sana, huenea kutoka kwenye kinena hadi kwenye korodani zenyewe. Hernia ikiwa kubwa sana huleta matatizo kuiondoa.

  1. Umbilical (belly button hernia)

Belly button hernia au umbilical hernia kama inavyoitwa mara nyingine, ni pale utumbo au mafuta yanapopenya kupitia sehemu dhaifu ya misuli iliyopo katikati ya tumbo chini ya kitovu. Sehemu hii ndiyo inayopata udhaifu mara nyingi kwa sababu ndiyo sehemu inayopata minyumbuko zaidi wakati tukifanya shughuli yo yote ya mwili.

Umbilical hernia inaweza kuwa moja kwa moja chini ya kitovu, lakini wakati mwingine inaweza kuwa juu kidogo au chini kidogo ya kitovu. Inaweza kuonekana kama kijikokoto kidogo chini ya ngozi, au ikikua inaweza kuonekana kama kijimpira cha gofu au hata kufikia kimpira cha tenisi kama kikiachwa bila tiba.

Kwa watoto wa kufikia hadi miaka 5, hernia hii kwa kawaida huondoka yenyewe. lakini kwa watu wazima hernia hii haipungui na huwa inazidi kuwa kubwa kila wakati.

Wanawake kwa kawaida hupata umbilical hernia wakati wa ujauzito, na hupotea yenyewe baada ya kujifungua. Kwa baadhi ya wanawake, kijishimo hiki katika musuli hubakia baada ya kujifungua. Inashauriwa kuwa wanawake wasubiri kwa miezi 3-6 kuona kama hernia hii itafunga yenyewe.

Kama ilivyo kwa hernia nyingine, dalili za kawaida ni maumivu kwenye kitovu. Kutokana na mafuta au misuli kupita kwenye hernia hii, uvimbe utaonekana chini ya ngozi kwenye eneo hilo. Baada ya muda, kama hernia itakuwa kubwa sana, utumbo unaweza kunaswa kwenye hernia hiyo na kuleta madhara kwenye utumbo, vikiambatana na kichefuchefu, kutapika, na kufunga choo.

Kwa sababu hakuna hernia inayopona yenyewe, upasuaji unahitajika. Njia inayopendekezwa hapa ni open surgery kwa sababu tundu ni dogo.

Sababu Za Hernia

Ukiondoa hernia inayotokana na upasuaji wa awali, mara nyingi hakuna sababu inayoeleweka ya kusababisha hernia. Watu walio kwenye hatari zaidi ya kupata hernia ni wenye umri mkubwa, na wanaume wapo kwenye hatari zaidi kuliko wanawake.

Hernia inaweza kujitokeza mtoto anapozaliwa au kwa watoto waliozaliwa na dosari kwenye kuta za matumbo yao.

Shughuli au madawa yanayosababisha mgandamizo kwenye kuta za tumbo vinaweza kusababisha hernia. Vitu hivi ni pamoja na:

. Kujikamau kwa nguvu wakati wa haja kubwa kutokana na choo kuwa kigumu

. Kikohozi cha mara kwa mara

. Kuwa na tatizo la cystic fibrosis

. Kuvimba kwa tezi dume

. Unene wa kupindukia

. Kukojoa kwa shida

. Kunyanyua vitu vizito

. Maji tumboni

. Lishe duni

. uvutaji wa tumbaku

. Korodani zisizoshuka

. Uchovu wa mwili

Dalili Za Hernia

Mara nyingi, hernia ni uvimbe unaoonekana usio na mauvimu na usiohitaji tiba ya haraka. Lakini wakati mwingine, inaweza kukukosesha raha na kuwa na maumivu, dalili zikiongezeka wakati umesimama au wakati unanyanyua vitu vizito. Watu wengi huona uvimbe ukizidi na hatimaye humwona daktari.

Kuna wakati ambapo hernia inahitaji huduma ya haraka ya upasuaji, kwa mfano, pale sehemu ya utumbo inapokuwa imezibwa na hernia ya tumbo (inguinal hernia).

Hatua za haraka za uchunguzi zinatakiwa zichukuliwe wakati inguinal hernia inapoanza kuonyeza dalili kali za:

. Maumivu

. Kusikia kichefuchefu

. Kutapika

Uvimbe wa hernia yenye dalili hizi mara nyingi ni mgumu na huleta maumivu na hauwezi kusukumwa urudi ndai ya tumbo.

 

Hiatal hernia inaweza kuleta dalili za acid refluc kama kiungulia, kinachotokana na tindikali za tumboni kupanda kwenye koromeo.

Tiba Ya Hernia

Hernia isipokuwa na dalili mbaya, njia bora ni kuiacha na kusubiri, ingawa hii inaweza kuwa njia sahihi kwa hernia za ina fulani, kama femoral hernia.

Madaktari bado hawajafikia kukubaliana wote kuhusu faida za kufanya upasuaji kwa inguinal hernia ambayo haijaanza kuleta usumbufu ambayo inaweza kusukumwa ndani ya tumbo. Madaktari wengi wa nchi ya Marekani wanashauri kusubiri badala ya kufanya upasuaji. Wengine wanashauri kufanya upasuaji ili kuiwahi kabla haijaweza kuziba sehemu za utumbo.

Uamuzi wa kufanya upasuaji unategemea hali iliyopo, pamoja na sehemu hernia ilipo, ambapo kuna upasuaji wa aina mbili unaoweza kufanyika:

. Open surgery

. Laparoscopic operation (keyhole operation).

Open surgery huziba hernia kwa kutumia nyuzi (sutures), mesh au vyote na kidonda juu ya ngozi kuzibwa kwa nyuzi, staples au surgical glue.

Laparoscopic repair hutumika kwa upasuaji wa kujirudia ili kukwepa makovu, igawa ni ghali zaidi, inapunguza uwezekano wa kuleta madhara hasa ya maambukizi ya vijidudu.

Kwa kulinganisha upasuaji huu wa aina hizi mbili, asilimia za uwezekano wa hernia kujirudia zinalingana, ingawa open surgery inaweza kusababisha madhara zaidi, kama maambukizi ya vijidudu.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Janeth Jovin

A writer, reporter, presenter and news anchor for Mwananchi Scoop. Her writings are based on business, money management on Tuesday and health on Thursday on Mwananchi Scoop. Her famous segments on Mwananchi Scoop include KARIA and FASHION.


Latest Post