Zimesalia siku chache tu kabla ya kuumaliuza mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025. Kwenye burudani kuna matukio mengi kama ilivyo kwenye tasnia nyingine kama michezo ambako mengi yametokea mwaka huu unaokwenda ukingoni.
Yapo matukio katika burudani ambayo yaliteka hisia za watu na kuwa mjadala kwa kipindi fulani kabla ya kuibuka mengine na yenyewe kupita.
Mwananchi linakuchambulia matukio hayo ambayo kwa namna moja au nyingine hayakupita hivi hivi na yaliibua mjadala kwenye vyombo vya habari na mitandaoni.
1. Hamisa na Azizi KI
Huko mitandaoni habari kubwa ilikuwa ni uhusiano wa nyota wa Yanga, Aziz Stephanie Ki na Mwanamitindo na mjasiriamali Hamisa Mobetto. Ubishi ulikuwa mwingi na wapo waliosema ni wapenzi na wengine wakidai wanatafuta kiki.
Ukaribu wao ulikuwa mkubwa na kila mahali kuonekana pamoja, ikiwamo wakati wa tuzo za wanamichezo bora wa msimu wa 2023/24, uzinduzi wa duka la nguo la Hamisa Tandika na Siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi kati ya mengine.
Zaidi ya yote ukaribu wao umezua maswali, kutokana na uvumi Aziz KI amezaa na mwigizaji wa Bongo Movie, Vanessa Kashera na inadaiwa pia staa huyo yupo karibu na mwanamitindo huyo katika kumshikia tu kigogo.
2. Nandy azimia jukwaani
Msanii huyu alianguka ghafla jukwaani kwenye show ya Marioo iliyofanyika Warehouse Masaki na kuzimia na aliwahishwa hospitali akiwa hajitambui, huku sababu ikidaiwa ni kutokana na kuchoka.
3. Marioo akimbia shoo Arusha
Msanii huyu aliingia kwenye kesi ya madai na kampuni ya Kismaty inayojihusisha na kuandaa matukio ya burudani mbalimbali nchini.
Inadaiwa kampuni hiyo iliandaa shindano la Mr & Miss Vyuo Vikuu Kanda ya Kaskazini na ilitarajiwa msanii huyo akatumbuize lakini hakufanya hivyo.
Katika kesi hiyo, kampuni hiyo ilimtaka awalipe Sh550,000,000 kwa kuvunja makubaliano.
Ilivyokuwa; Marioo alilipwa Sh15 milioni kwa ajili ya shoo hiyo iliyotakiwa kufanyika Arusha kwenye ukumbi wa Blue Stone Lounge na alilipwa Sh8 milioni kabla ya kupewa tena Sh 15 milioni kwa ajili ya kupanda jukwaani septemba 25.
Hata hivyo, hakutokea na kampuni hiyo kudai imeingia hasara ya Sh500,000,000 na nyingine ya 50 milioni kutoikana na maandalizi na gharama nyingine na hivyo kuwasababishia hasara.
4. Zuchu yamkuta stejini
Ni katika tamasha la Wasafi Festival lililofanyika jijini Mbeya, Septemba 28 na msanii Zuchu alipanda stejini ili kufanya yake kabla ya balaa kumkuta akiwa katikati ya shoo.
Kilichotokea ni mashabiki waliofurika kutazama shoo hiyo walianza kumrushia vitu mbalimbali ikiwamo chupa za maji na kulazimika kushuka stejini na tukio hilo kuvuta hisia za watu mitandaoni, wengine wakijadili mashabiki kukosa utu na wengine wakilaani alichofanyiwa msanii huyo anayefanya vizuri kwa upande wa wanawake.
5. Chid Benz na yebo yebo zake
Kuna wasanii wana vituko. Hapa kwa Chid Benz acha kabisa. Ilkuwa ni kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama na baada ya DJ kupiga wimbo wake wa 'Dar es salaam Stand Up' msanii huyo ghafla akaibukia stejini katika tamasha kubwa la Best Vibes.
Kilichotokea sasa. Msanii huyo alishushwa jukwaani na mabaunsa kwa sababu hakuwa kwenye ratiba ya watakaotumbuiza huku pia mwonekano alioingia nao wa kuvaa yeboyebo ukileta mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
6. Dulla Makabila atoswa Simba
Kilichomkuta msanii Dulla Makabila mwaka huu yeye mwenyewe hakuamini. Kisa Yanga tu, mashabiki wa Simba wakamtosa asiguse kwenye Simba Day.
Ilikuwa hivi. Kwanza imekuwa kawaida kwa Makabila kuhama timu hizo za Kariakoo na mara ya mwisho alirudi Yanga akitokea Simba na kabla ya hapo alihamia Simba akitokea Yanga.
Sasa bana, si akaibukia Simba, mashabiki wa kamkataa na baadaye akaenda kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuwaeleza anaenda kupika bonge moja la dude na watamkubali watake wasitake.
Hapo sasa. Hata baada ya dude hili kutoka mashabiki bado walimkazia na kujikuta akirudi zake Yanga na kuomba radhi huku akidai atafanya shoo tano za bure kama sehemu ya adhabu.
7. Malu Stonch kufariki stejini akiwa anaimba
Nyota mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Malu Stonch amefariki mwaka huu, alifariki dunia baada ya kuanguka ghafla jukwaani katika ukumbi wa Target akiwa anaimba.
Skendo hii ilizungumza sana katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ambao kila mmoja alikuwa anaongea la kwake.
8. Caren Simba awachanganya Pacome, Aucho
'Wanafeli uwanjani kisa mrembo Caren Simba.' Ndiyo maneno yaliyozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii hasa baada ya kuonekana kwa Pacome Zouzoua na Khalid Aucho wakiwa na mrembo huyo kwa nyakati tofauti.
Kilichopo sasa. Kwa nyakati tofauti mastaa hao wanaokipiga Yanga wamekuwa wakikanusha kutoka na mrembo huyo, huku pia Caren akidai ni washkaji tu.
Kilichoibua mjadala zaidi ni aliwahi posti kwenye ukurasa wake wa Instagram kupost picha akiwa amevaa jezi ya Aucho.
Alivyowajibu sasa; “Sio tu Pacome kuwa naye karibu, mimi karibia wachezaji wote wa Yanga nipo nao karibu, kwa nini waseme Pacome? Nieleweke jamani, Pacome sio mpenzi wangu.”
“Jamani hawa watu mnaonipa wana wapenzi wao, sasa kwa nini mimi nahusishwa? Sasa kama Aucho naye nahusishwa naye kisa tu amenipa zawadi ya jezi, ina maana mimi sipaswi kupewa zawadi na mtu? Tena Aucho ni mshkaji sana na tunaheshimiana sana, wala sio mpenzi wangu, nawezaje kuwa na wapenzi wote hao wa timu moja, huku si kujiaibisha?”
Mwanaspoti lilishawahi kuongea na Pacome na kudai Caren ni rafiki tu si mpenziwe.
9. Nay wa Mitego na Basata
Mwaka huu alikabiliwa na mashtaka ya ukiukwaji wa kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kutokana na kutoa wimbo wake mpya 'Nitasema' Septemba 24, 2024 bila ya kuwa na kibali. Baraza liliainisha makosa manne yanayomkabili ikiwano kutoa bila kibali, maudhui yenye uchochezi, kupotosha jamii na kukashifu mataifa mengine.
Kutokana na makosa haya, Basata likamtaka msanii huyo kufuata sheria na taratibu zinazohusu usambazaji wa kazi za sanaa nchini. Hatua zaidi za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yake ikiwa atapatikana na hatia ya makosa yaliyotajwa.
10. Diamond nyumbani kwa P.Diddy
Hili ndilo tukio lililofuatiliwa sana na mashabiki mtandaoni kutokana na ukubwa wake likimhusisha mkali wa Hip Hop Marekani, Sean John Combs 'P. Diddy'.
Wengi wakidai ni uzushi, wengine wakitengeneza stori ilimradi tu mjadala. Na kweli kwa mwaka huu ulitikisa.
Kilichotokea ni baada ya mkali huyu ewa Bongo Fleva, Diamond Platnumz siku moja kuhojiwa na kufunguka aliwahi kufika kwenye nyumba ya rapa huyo na alidai kuna mambo waliyofanya katika karamu iliyoandaliwa kwenye jumba la msanii huyo na hayakutakiwa kujadili na kuchukua picha na video.
Kutokana na kauli hiyo na baada ya mkali huyo wa 'I need a Girl' kukamatwa na polisi wa Marakani kutokana na tuhuma za unyanyasaji wa kingono, huku mtandaoni kukaibuka mjadala wa nini walichofanya ingawa hadi sasa hakuna jibu na rapa huyo anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya kesi hiyo inayomkabili.
Leave a Reply