Diamond kajimilikisha namba moja!

Diamond kajimilikisha namba moja!

Peter Akaro

Ndivyo tunaweza kusema kufuatia Diamond Platnumz kuendelea kuwa kinara wa mambo mengi katika tasnia ya muziki hasa ule wa Bongofleva ambao umempatia mashabiki wengi tangu mwaka 2009 alipovuma kwa mara ya kwanza.

Katika orodha ya wasanii waliofanya vizuri kwa mwaka 2024 katika majukwaa ya kusikiliza muziki, Diamond amekuwa namba moja katika mitandao yote huku kukiwa na utofauti mkubwa wa namba kati yake na wenzake.

Utakumbuka Diamond alitoka na wimbo, Kamwambie (2009) uliomfanya kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2010 kama Msanii Bora Chipukizi na hadi sasa ameshashinda tuzo hizo 22 akiwa ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi.

Na huyu ndiye msanii Bongo aliyefanya vizuri zaidi YouTube 2024 ambapo ametazamwa (views) zaidi ya mara milioni 440 akifuatiwa na Rayvanny mwenye milioni 182 ambaye namba zake hata ukizizidisha mara mbili bado hamfikii Diamond!.

Upande wa Boomplay Music, nyimbo za Diamond kwa 2024 zimesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 132, akifuatiwa na Jay Melody mwenye milioni 110, kisha Marioo (80), Zuchu (78), Harmonize (72), Mbosso (58), D Voice (53) na Rayvanny (49).

Tukija Spotify, wimbo kutoka Tanzania uliofanya vizuri katika jukwaa hilo 2024, ni wake Diamond 'Komasava' uliosikilizwa zaidi ya mara milioni 9, ukifuatiwa na wake Jaivah 'Kautaka' wenye milioni 3, namba ambazo hata ukizizidisha mara mbili haziifikii Komasava.

Utakumbuka wimbo 'Komasava' akiwashirikisha Khalil Harisson na Chley kutokea Afrika Kusini, mwaka uliopita uliingia Billboard U.S Afrobeats Songs na kumfanya Diamond kuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kuingia katika chati hizo kubwa.

Hata hivyo, Diamond hajapata namba hizo au kufiki mafanikio hayo kwa kubahatisha bali huo ni mwendelezo wake miaka nenda rudi, akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi, muziki wake umekuwa na athari chanya katika ukuaji wa tasnia.

Lebo yake ya WCB Wasafi imekuwatoa wasanii wengi wakubwa, mmoja wapo ni Rayvanny ambaye ni msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo ya BET, alifanya hivyo 2017 akiwa ni wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda hapo 2015.

Diamond, mshindi wa tuzo nane za AEAUSA Marekani, ndiye msanii pekee Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa YouTube zaidi mara milioni 100, anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020 na Nana (2015).

Ndiye msanii mwenye ushawishi zaidi katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki na Kati akiwa ni namba moja kwa kuwa na wafuasi wengi katika mitandao ya Instagram, Facebook, X, TikTok na YouTube ambapo pia ni namba moja Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ikumbukwe hadi Desemba 2015 Diamond alikuwa ndiye msanii mwenye wafuasi wengi Instagram Afrika akiwa nao milioni 1.5, ila kufikia Septemba 2016 akashushwa na Davido wa Nigeria aliyefikisha wafuasi milioni 2.9 kwa wakati huo.

Diamond ni msanii wa kwanza Tanzania kumiliki redio na TV (Wasafi Media) akiwa wa pili Afrika baada ya Youssou N'Dour wa Senegal, na katika eneo hilo wasanii wengine Bongo wanafuata nyayo zake baada ya Alikiba kuanzisha Crown Media.

Staa huyo mwenye albamu tatu na EP moja, ndiye msanii wa kwanza Tanzania kumiliki gari la kifahari aina ya Rolls-Royce Cullinan akiungana na mastaa wengine wa muziki Afrika kama Burna Boy, D'Banj, Phyno, Davido, Mr. P, J Martins, DJ Cuppy n.k.

Pia Diamond ndiye msanii wa kwanza Afrika kushinda tuzo mbili za MTV Europe Music Awards (EMAs) kwa mpigo na hadi sasa akiwa nazo tatu sawa na Tyla kutokea Afrika Kusini, hawa ndio vinara wa tuzo hizo barani Afrika.

Ikumbukwe Rayvanny aliyetolewa na Diamond, ndiye msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza tuzo za MTV EMAs, mwaka 2021 alipanda katika jukwaa hilo akiwa na Maluma kutokea Colombia na kuimba wimbo wao, Mama Tetema (2021) uliotayarishwa na S2kizzy.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags