Diamond, Jason Derulo ni ukurasa mpya baada ya miaka 10

Diamond, Jason Derulo ni ukurasa mpya baada ya miaka 10

Na Peter Akaro

Ni ukurasa mwingine kwa Diamond Platnumz baada ya kuachia remix ya wimbo wake, Komasava (2024) ambao ameshirikiana na Jason Derulo kutoka Marekani pamoja na Khalil Harisson na Chley wote kutokea Afrika Kusini.

Wimbo huo ambao ni wa tatu kwa Diamond kuachia kwa mwaka huu baada ya Mapoz na Raha, unatarajiwa kuendeleza kulipaisha jina la staa huyo wa WCB kimataifa kutokana na ubunifu wake lakini pia ukubwa wa Jason Derulo.

Hii inaturudisha nyuma miaka 10 iliyopita ambapo Diamond aliachia remix ya wimbo wake, My Number (2014) akimshirikisha Davido kutoka Nigeria na tangu hapo akaanza kufanya vizuri kimataifa.

Ni wimbo uliomfanya Diamond kuwania vipengele viwili katika Tuzo za MTV MAMA 2014 kama Msanii Bora wa Kiume na Wimbo Bora wa Kushirikiana, huku akitumbuiza katika hafla ya utolewaji wa tuzo hizo uliofanyika Durban, Afrika Kusini.

Hivyo, Komasava iliyokuja baada ya miaka hiyo 10 akiwa na Jason Derulo, mwanamuziki aliyeuza rekodi zaidi ya milioni 250 duniani kote, ni ukurasa mwingine kwa Diamond katika kulishika soko la kimataifa kupitia remix za nyimbo zake.

Ikumbukwe hii sio mara ya kwanza kwa Diamond kufanya kazi na msanii wa Marekani kwani albamu yake ya tatu na ya mwisho, A Boy From Tandale (2018) chini ya Universal Music Group (UMG) ilishirikisha wasanii watatu wa nchi hiyo.

Kwanza ni Ne-Yo aliyesikika katika Wimbo Marry You (2017) uliokuwa unasubiriwa tangu wawili hao walipokutana kwenye MTV Africa Music Awards Kwazulu-Natal-2015 (MAMA) huko Durban, Afrika Kusini.

Vilevile alifanya kazi na Rick Ross, Waka (2017), wimbo uliokuja kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) mnamo Februari 2018 kwa kukiuka maadili, huku Omarion akisikika katika Wimbo African Beauty (2018).

Katika albamu yake ya saba Alicia Keys, ALICIA (2020) ambayo ilishinda Tuzo ya Grammy 2021 kama 'Best Immersive Audio Album', Diamond amesikika katika wimbo 'Wasted Energy' umbao ulipata mapokezi mazuri kwa Afrika kutokana na ushawishi wake.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags