Claudian Benet: Kijana anayefanya kazi za ubunifu wa tekonolojia na matangazo

Claudian Benet: Kijana anayefanya kazi za ubunifu wa tekonolojia na matangazo

Ni ukweli uliyowazi kuwa wabunifu ni wadau muhimu katika ukuzaji wa sayansi, tekonolojia na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa ilitoa ripoti yake inayoonyesha ongezeko maradufu la thamani ya biashara ya bidhaa zitokanazo na ubunifu kutoka dola bilioni 208 mwaka 2002 hadi dola bilioni 509 mwaka 2015.

Ripoti hiyo ambayo ni toleo la pili la tathmini ya uchumi utokanao na bidhaa za ubunifu ilizunduliwa huko Geneva, Uswisi ambapo ilieleza kuwa China ndio inaongoza kwa kiasi kikubwa katika biashara hiyo ya bidhaa za ubunifu inayohusisha ubunifu wa majengo, mitindo ya mavazi na maonesho, usanifu wa ndani ya nyumba na hata sanaa za filamu na vikaragosi.

Ukiangalia ripoti hiyo utatambua kuwa ubunifu ni jambo la muhimu sana na linapaswa kupewa kipaombele ili kuweza kufikia malengo na maendeleo katika nchi.

Kutokana na umuhimu huo, kijana Claudian Benet ambaye ni muhitimu wa Kozi ya Design kutoka Taasisi ya Sanaa nchini California anafunguka ndani ya mwananchiscoop kuhusu masuala mbalimbali ya ubunifu.

Benet alisema kwa sasa anafanya biashara ya ubunifu wa matangazo na teknolojia (creative and technology business) kupitia kampuni yake ya Centric Creative Studios.

Alisema kampuni hiyo inajihusisha na utengenezaji wa matangazo na mifumo mbalimbali ya kidigitali kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa shughuli za kampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Pia inatoa mafunzo ya ubunifu wa kidigital (Digital and Creative Design) kupitia chuo cha change Centric Design Academy ambapo anafundisha masomo ya utengenezaji wa matangazo ya picha, video na sauti pamoja na utenezaji wa tovuti (web design) na Mifumo ya simu na computer (Apps).

Kwanini anafanya kazi hiyo

Alisema aliamua kufanya kazi hiyo kwa sababu ya mapenzi binafsi ya ubunifu wa matangazo na teknolojia pia uhitaji mkubwa wa watu wa namna hiyo katika tasnia ya ubunifu wa matangaazo na mifumo ya kidigitali hapa nchini.

“Kabla ya kupokea mafunzo kamili ya ubunifu wa mifumo ya kidigital, nilianza kujifunza mwenyewe kupitia mtandao wa youtube na kufanya mazaoezi tofauti ya utengenezaji wa mifumo hii.

“Nashukuru Mungu jambo hilo lilinisaidia na kuifanya kazi yangu kuwa rahisi nilipofika chuoni kwenda kujifunza mambo hayo kwa undani zaidi,” alisema

Changamoto anazokumbana nazo

Benet anafunguka na kusema kuwa suala la ubunifu ni muhimu na linapaswa kupewa kuipaombele na kila mtu nchini.

Alisema watu wanapaswa kuthamini na kutambua mchango wa wabunifu kwani wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali ambazo ndizo zinawaingizia kipato na kujikwamua kimaisha.

“Pamoja na kwamba tunajituma kufanya biashara kwa bidii tumekuwa tukikumbana na changamoto ya watu wengi kutokuwa na ufahamu na uelewa kuhusu biashara ya ubunifu hivyo kusababisha kutothamini kazi na mchango wa wabunifu katika kuendeleza biashara zao,” alisema.

Aidha alisema changamoto zingine ambazo ukumbana nazo ni gharama za uendeshaji kuwa kubwa kutokana na vitendea kazi kuwa ghari na kutopatikana kwa urahisi hapa nchini.

“Ila uwepo wa watu wengi kutoka nje ya nchi wanaofanya kazi hizi umekuwa ukipunguza motisha na nafasi kwa watanzania kufanya kazi hizi,” alisema

Faida aliopata kupitia bishara hiyo

Alisema moja ya faida aliyoipata kupitia biashara hiyo ni kuanzisha kampuni inayompa kipato kinachoendesha maisha yake na familia kwa ujumla ya kila siku.

“Niweza kutambulika katika jumuiya mbalimbali za wabunifu wa mifumo ya kidigital nje na ndani ya nchi, lakini pia nimebahatika kukutana na watu tofauti tofauti na kujifunza zaidi kuhusu biashara hii ya ubunifu na zingine nyingi,” alisema

Alisema faida nyingine aliyoipata ni kuwezesha vijana wengine kujifunza na kuingia katika tasnia na ubunifu wa mifumo yakidigital kupitia mafunzo yatolewayo na Centric Design Academy pamoja na wengine kupata ajira baada ya kuhitimu mafunzo.

Ushauri wako kwa vijana

Alisema vijana wanapaswa kuwa tayari kujifunza vitu mbalimbali na kubadilika kulingana na mazingira, sababu dunia ya

sasa hivi ina kazi nyingi mpya ambazo hazikuwepo hapo zamani, hususani zile zinazoleta maendeleo ya kidigitali.

“Pia wanapaswa kuwa tayari kujitolea kwa muda ili kupata uzoefu utakaosaidia katika ufanyaji wa kazi zingine baadae,” alisema

Kitu kingine anachopenda kukifanya

Alisema anapenda kuandaa matamasha mbalimbali ya sanaa na muziki kwani ni moja ya maeneo anayoyapenda pia.

Aidha alisema anatamani kuwa mmoja wa watu ambao wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kidigital hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Alisema anaamini baada ya muda atakuwa na uzoefu mkubwa katika kazi hii na pia kusaidia vijana wengi zaidi ambao watakwenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali hivyo kuleta athari chanya kwenye sekta ya kidigitali hapa nchini.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post