Chino Kidd amvaa tena Marioo, Amtaja Baba Levo

Chino Kidd amvaa tena Marioo, Amtaja Baba Levo

Kutokana na mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii yakimhusisha mwanamuziki na dansa Chino Kidd kuwa kwenye mgogoro na bosi wake wa zamani Marioo, mkali huyo amefunguka na kuelezea suala hilo kwa undani.

Akizungumza na Mwananchi, Chino amesema mgogoro wao ulitokana na kutokuwa na upendo, hivyo kwa sasa moyo wake una amani na anaendelea na maisha mengine.

“Mimi binafsi tayari moyo wangu una amani kwa sababu nimesamehe vile vyote ambavyo vilikuwepo, naendelea na maisha mengine, sitaki kuongea sana kwa sababu inaweza kumuathiri pia na yeye ni binadamu, hata kama amekosea nahisi atakuwa anajisikia vibaya kwa hicho kinachoendelea," anasema Chino.

Licha ya kusamehe Chino anasema huenda kutakuwa na mtu ambaye anampa maneno Marioo na ndiyo maana ghafla amekuwa na chuki.

“Nahitaji kuacha kuongelea hivyo vitu lakini ilikuwa ni katika kutokuwa na upendo, na hauwezi kujua labda kuna watu wakikaa wanampa maneno, mtu kuwa na chuki ghafla haiwezekani, kwa sababu kila anachotaka nifanye nafanya, show nimemshirikisha kama bosi wangu na yeye ndiye kanipa mpaka jina, kwa hiyo imekuwa ghafla kusikia hataki kuwepo kwenye hii show bila sababu, mimi naamini kuna mtu anakaa na kumpa maneno ambayo siyo mazuri yanayomfanya ‘apaniki," anasema.

Aidha kuhusiano na minong’ono ya baadhi ya watu kudai kuwa kutakuwa na bifu ambao lipo nyuma ya pazia Chino amekanusha jambo hilo kwa kueleza kuwa ugomvi wao mkubwa ni Marioo kugoma kufika katika show yake.

“Hakuna tatizo lolote zaidi ya hilo la kugoma kutokea kwenye show na hakupiga simu, kwa hiyo mimi hicho kitu sikukipenda kwa sababu tunaishi kila siku pamoja, na mimi nasapoti show zake zote, namuheshimu kama bosi, nampenda tumeishi maisha yote tangu tumeanza hatuna kitu mpaka leo, kwanini iwe ghafla hivi kwa hiyo sikupenda,” anasema Chino.

Kutokana na mgogoro huu baadhi ya watu wakiwemo wadau wa muziki wamekuwa wakitoa maoni tofauti. Kwa upande wa msanii Baba Levo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameeleza kuwa Chino hakutakiwa kufikia hatua hiyo  kwa kuwa Marioo ndiye mtu aliyemleta mjini. Hili pia Chino ametolea majibu.

“Kwanza Baba Levo, siyo staa wa kumuongelea, hajawahi kunipenda kwa sababu niliwahi kumfunika kwenye show, huyo labda ananichukia kwa sababu ya maendeleo, binafsi sijawahi kumchukia, kumdharau, sijawahi kugombana naye kwa hiyo mapepe yake tu.

“Mastaa wote wanajua kuhusu hilo, Marioo aliwaambia kuwa hatakuwepo siku ya Jumapili ina maana walikuja kwenye show yangu kwa sababu nawaheshimu na kuishi nao vizuri, hatuna matatizo nao wamekuja kwa sababu ya upendo, hakuna staa anayemuunga mkono zaidi ya Baba Levo kwa sababu yeye na Marioo wote wanachuki,” anasema Chino

Ikumbukwe kuwa Chino Kidd, wengi walimfahamu akiwa dansa wa Marioo. Na bifu hili limeendelea kuchukua vichwa vya habari kwenye mitandao ya kijamii baada ya  Chino kufuta urafiki na Marioo kwenye ukurasa wake wa Instagram, huku sababu kubwa ya  kufanya hivyo ikitajwa kuwa ni baada ya Marioo kugoma kuhudhuria kwenye show yake, iliyofanyika siku ya Jumapili Februari 4.

Hata hivyo Mwananchi limemtafuta Marioo, kuzungumzia juu ya mgogoro huo, lakini kwa upande wake amesema kuwa hawezi kumzungumzia Chino.

"Achana na hizo habari za Chino siwezi kuzungumza kuhusiana na hilo, ila kama kuna mambo mengine mbali na hayo nitazungumza."  Amesema Marioo.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags