Ray C na Babu Tale wametoka mbali sana!

Ray C na Babu Tale wametoka mbali sana!

Baada ya miaka mitano akiwa kama Mtangazaji wa Radio, Ray C aliamua kujaribu bahati yake katika Bongofleva, basi sauti yake nzuri, nyembamba na ya kuvutia pamoja na uchezaji wake uliokosha wengi hadi kumuita 'Kiuno Bila Mfupa' vikafanikisha safari yake.

Ray C ameshinda tuzo za ndani na nje, ametoa albamu moja, Mapenzi Yangu (2003), ni miongoni mwa waimbaji wachache wa kike walioshiriki kuikuza na kuitangaza Bongofleva na nyimbo zake zitasikilizwa kwa wakati wote. Songa nayo;

Ray C alimlipa mwimbaji wa Taarab, Mwanahela ili kurudia nyimbo zake mbili, 'Mahaba ya Dhati' na 'Nimezama' ambazo zilifanya vizuri na kuanza kumtambulisha kwenye muziki. Ila nyimbo zake nyingine zilizofuata kama Upo Wapi, Na Wewe Milele n.k aliandika mwenyewe.

Lady Jaydee na Ray C waliwahi kuwa katika lebo moja, Smoth Vibe, walirekodi wimbo ambao ulitakiwa kuwepo kwenye albamu ya kwanza ya Jide, Machozi (2002) lakini haukufanikiwa kujumuishwa katika albamu hiyo.

Tuzo ya kwanza Ray C kushinda katika muziki ilikuwa 2004 kutoka Tanzania Music Awards (TMA) kama Msanii Bora wa Kike, huku Banana Zorro akishinda kama Msanii Bora wa Kiume.

Ray C alikuja kushinda tuzo hiyo tena 2007 katika kipengele hicho, huku tuzo yake ya kimataifa ni kutoka nchini Kenya, Kisima Awards 2004 kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.

Akiwa na umri wa miaka 17 tu, Ray C alianza kazi ya Utangazaji wa Radio, alitangaza East Africa Radio na baadaye Clouds FM kabla ya kuja kuwa Staa mkubwa katika muziki wa Bongofleva.

Hiyo ni sawa na TID, Lady Jaydee na Vanessa Mdee ambao kwa nyakati tofauti walitangaza Magic FM, Clouds FM na Choice FM kisha wakaja kuvuma kwenye Bongofleva.

Wimbo wa kwanza wa kundi la Tip Top Connection walimshirisha Ray C, unakwenda kwa jina la Nani Mwenye Thamani, hilo lilifanikiwa kutokana na ukaribu wa kikazi kati ya Ray C na Babu Tale ambao ulikuwepo kwa muda mrefu.

Muimbaji mkongwe wa muziki wa asili Bongo, Saida Karoli aliyetamba na kibao chake 'Maria Salome' anaamini kuwa sauti ya Ray C haina upinzani kwenye muziki wa Bongofleva hadi sasa.

Director Adam Juma ndiye alimuomba Ray C kushiriki katika wimbo 'Mama Ntilie', hiyo ni kutokana kwa wakati huo AJ alikuwa anawasimamia AT na Gelly waliosikika pia katika ngoma hiyo.

Basi Ray C akaingia studio na ndani ya muda wa saa moja tu akawa amemaliza kurekodi na video yake waliishuti ndani ya siku moja na kumaliza.


Ray C akiwa Mtangazaji wa East Africa Radio 1997 alikuwa anampa nafasi Babu Tale kuigiza sauti (jingle) za watu maarufu katika kipindi chake kitu ambacho alikuwa anakifanya Tale hapo awali. Ray C ni miongoni mwa watu waliomshika Tale mkono wakati anaanza kuingia katika tasnia ya burudani.

Ilimchukua saa moja tu Ray C kurekodi 'cover' ya wimbo wa Recho, Upepo iliyokuja kufanya vizuri, wakati Prodyuza Nahreel ilimchukua dakika 10 tu kutengeneza mdundo wa ngoma ya Joh Makini 'Don't Bother' akimshirisha AKA.

Kolabo ya Ray C na Mez B 'Kama Vipi' ilianzia Leaders Club walipokutana na kujadiliana kuwa wanaweza kufanya kazi pamoja, ndipo wakaenda studio kwa Miikka Mwamba kurekodi, ila Noorah ambaye naye kashirikishwa alikuja kuweka 'verse' yake baadaye sana.

Marehemu Mez B ambaye alikuwa miongoni mwa wasanii wa kundi la Chamber Squad alifanya shoo nyingi sana kutokana na kufanya vizuri ngoma hiyo na mara kadhaa alitumbuiza na Ray C na kupata shangwe kubwa. Hadi sasa ni moja ya kolabo kali za Bongofleva kwa muda wote.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags