Licha ya kukaa miaka zaidi ya minane bila kutoa kazi mpya, bado nyimbo za Shaa zilizompatia umaarufu zinaendelea kumtambulisha na kushikilia heshima yake katika muziki wa Bongofleva ulioajiri vijana wengi.
Shaa akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne, alikuja katika Bongofleva na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuimba, kucheza na mitindo kitu kilichosababisha kuonekana yupo mbele ya wakati. Fahamu zaidi.
Wasanii wa kimataifa waliomvutia hadi kuona anaweza kufanya muziki ni pamoja na Aaliyah, Brandy, Toni Braxtin, Mary J. Blige, Whitney Houston, Madonna na kadhalika, na hiyo ni baada kumsikia dada yake akisikiliza nyimbo za wasanii hao kila mara.
Rapa wa kundi la Chemba Squad, Ngwea aliyetikisa na albamu yake, A.K. A Mimi (2004) ndiye aliyempa jina hilo la Shaa ambaye alipozaliwa wazazi wake walimpa jina Sarah.
Na Ngwea aliyefariki mwaka 2013 nchini Afrika Kusini, ndiye aliyetohoa jina la aliyekuwa mtangazaji wa XXL ya Clouds FM, kutoka B Twelve kwenda B Dozen inayotumika hadi sasa.
Licha ya kushinda Coca-Cola Popstar (2004), Shaa hakuwa na mpango wa kushiriki shindao hilo bali alimsindikiza rafiki yake ila alipofika waandaji walimpa nafasi ya kushiriki na alivyojaribu akashinda na mengine sasa ni historia.
Baadaye alikuja kuungana na washindi wenzake, Witness na Langa na kuunda kundi la Wakilisha ambalo ni muunganiko wa majina yao. Wakilisha ndio walikuwa washindi kutokea Tanzania, huku Kenya wakiwa ni kundi la Sema na Uganda wakiwa ni Blu 3
Wimbo wa kwanza wa Wakilisha 'Hoi' ulirekodiwa Afrika Kusini na hata video yake ilifanyika huko, kwa ujumla walirekodi nyimbo nne chini ya MJ Records wakiwa huko, na walitakiwa kufanya albamu watakaporejea Bongo ila ikashindikana.
Na baada ya Shaa kujitoa katika kundi la Wakilisha kwa kile kilichoelezwa ni mgogoro wa kimaslai, Witness na Langa ambaye sasa ni marehemu wakaunda kundi lao walilolipa jina la Wakili na wimbo wao wa kwanza kutoa unaitwa No Chorus.
Shaa ndiye msanii wa kwanza wa kike kusainiwa MJ Records, lebo ambayo alifanya nayo kazi kwa kipindi cha takribani miaka 10 na kuachia albamu yake ya kwanza kama solo, Zamu Yangu.
Ikumbukwe kundi la Wagosi wa Kaya linaloundwa na Dr. John na Mkoloni, ndio wasanii kwanza kusainiwa MJ Records na ndio waliomfanya Master J kuanzisha lebo hiyo baada ya awali kujikita na studio tu, MJ Production.
Baada ya kuachana na MJ Records, Shaa alianzisha lebo yake, SK Music, huku akifuatiwa na wasanii wengine wa kike Bongo kama Vanessa Mdee (Mdee Music), Hamisa Mobetto (Mobetto Music), Shilole (Shishi Gang), Nandy (The African Princess).
Kabla Zuchu hajatoka kimuziki chini ya WCB Wasafi, aliwahi kumwandikia Shaa wimbo. Hiyo ni sawa la Lady Jaydee ambaye amewahi kuwaandika wasanii kama Nakaya Sumari, Keisha, Patricia Hillary, Papii Kocha na kadhalika.
Wimbo wa Shaa, Sawa (2016) umeandikwa na kundi la Yamoto Band wakishirikiana na Kayumba ambaye ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2015. Wasanii wengine waliomwandikia Shaa ni H. Mbizo (Toba) na Barnaba (Promise).

Leave a Reply