Zimebaki siku kadhaa kuingia mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Mwezi ambao hupambwa kwa swala na nyimbo mbalimbali za Kaswida. Ni ngumu mwezi huo kumalizika bila kusikia wimbo uitwao 'Ramadhan' ulioimbwa na mwanamuziki Zain. Fahamu zaidi.
Jina kamili la msanii wa wimbo huo ni Maher Zain. Mwanamuziki maarufu wa R&B aliyezaliwa Lebanon lakini kwa sasa anaishi Sweden tangu familia yake ilipohamia huko akiwa na umri wa miaka minne.
Msanii huyo anafahamika sana kwa nyimbo zinazobeba ujumbe wa Kiislamu. Zikiwemo 'Ramadhan', na 'Antassalam'.
Licha ya kufanya muziki lakini pia ana shahada ya uhandisi wa anga. Lakini maisha yake ameyaelekezea kwenye muziki. Ambapo amewahi kufanya kazi kama mtayarishaji wa muziki huko Sweden na New York.
Kati ya watu aliowahi kufanya nao kazi ni RedOne, ambaye ni mtayarishaji wa muziki kutoka Morocco,Kat DeLuna na Lady Gaga.
Hata hivyo, mwaka 2009 baada ya kuamua kurudi kwenye imani yake ya Kiislamu kwa kuwa mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za dini hiyo, alijiunga na rekodi lebo ya 'Awakening Record'. Ndipo mwaka huohuo aliachia albamu yake ya kwanza, 'Thank You Allah'.
Hata hivyo, mwaka 2020 aliachia wimbo 'Antassalam' kwa ajili ya mwezi Mtukufu wa Ramadan pia akaachia na mwingine ambao unasikilizwa sana katika mwezi huo 'Ramadhan'.
"Tuna mpango wa kuachia nyimbo kila Ramadan. Na hii itakuwa maalum zaidi kwa sababu itatufanya tukumbuke nyakati ngumu ambazo ulimwengu wetu ulipitia kutokana na hali ya janga la virusi vya corona," Zain aliwahi kusema wakati akizungumza na Shirika la Habari la Anadolu.
Mbali na hayo mwimbaji huyo ana uwezo wa kuimba kwa lugha saba ikiwemo Kituruki, Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kiindonesia, Kimalai na Kihindi. Na amekuwa akifanya hivyo katika nyimbo zake
Kati ya nyimbo ambazo ameimba katika lugha mbalimbali ni 'Insha Allah' ambayo inapatikana kwa Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kituruki, Kimalai, na Kiindonesia
'Asalamu Alayka' imeimbwa kwa Kiarabu, Kiingereza, Kituruki, na lugha nyingine
Hivyo basi video ya wimbo wake 'Ramadhan' ambao umeimbwa kwa lugha ya Kiingereza hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 75 kwenye mtandao wa YouTube. Huku ukiwa umeachiwa miaka 11 iliyopita
Nao 'Ya Nabi Salam Alayka' ukiwa katika lugha ya Kiarabu hadi sasa umetazawa zaidi ya mara milioni 602. Aidha 'Number One For Me' umetazamwa zaidi ya mara milioni 165.

Leave a Reply