Mtayarishaji maarufu kutoka India, Rakesh Roshan ambaye ni baba mzazi wa mwigizaji Hrithik Roshan amemkabidhi kijana wake huyo mikoba ya kuongoza filamu maarufu ya ‘Krrish 4’.
Roshan amelithibitisha hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram wikii chache zilizopita huku akimtakia mema mwanaye huyo katika jukumu lake hilo jipya.
“Miaka 25 nyuma nilikuzindua kama muigizaji na leo tena baada ya miaka 25 nakuzindua tena wewe kama mkurugenzi na mwogozaji wa filamu. Utaongoza ‘Krrish 4’ ukishirikiana na watengenezaji wawili ambao ni Aditya Chopra na mimi mwenyewe kuipeleka mbele filamu yetu ya ‘Krrish 4’. Nakutakia mafanikio mema katika filamu yako hii mpya,”ameandika Roshan
Aidha filamu hiyo itakuwa chini ya kampuni mbili ambazo ni ‘FilmKraft’ ya Rakesh pamoja na ‘Yash Raj Film’ inayoongozwa na Aditya Chopra huku ikidaiwa kuwa ndio filamu itakayotumia gharama kubwa zaidi katika utengenezaji wake.
Rakesh Roshan amewahi kutamba na filamu mbalimbali zikiwemo Koi... Mil Gaya, Kaho Naa... Pyaar Hai, Koyla, Khoon Bhari Maang, Krrish 1-3. Huku muendelezo wa Krrish 4 ukitarajiwa kuanza kurekodiwa mapema mwaka 2026.
Hata hivyo kwa upande wa Hrithik Roshan amethibitisha kupokea mikoba hiyo ambapo amekiri kuwa na wasiwasi katika jukumu lake jipya alilokabidhiwa na baba yake.
“Siwezi kuwaambia jinsi ninavyohisi wasiwasi. Nahitaji msaada wenu wote, uzoefu wangu wa kukaa nyuma ya kamera ulikuwa kwenye filamu ya Koyla, lakini sikukaa muda mrefu na ilikuwa ni zamani sana lakini hili jukumu la sasa ni zito sana,”amesema Hrithik wakati alipokuwa kwenye mahijiano yake huko Atlanta, Georgia

Leave a Reply