Aliyetamba Na Wimbo Wa Pretty Little Baby Afariki Dunia

Aliyetamba Na Wimbo Wa Pretty Little Baby Afariki Dunia

Mwanamuziki mkongwe kutoka Marekani, ambaye kwasasa anatamba na wimbo wa ‘Pretty Little Baby’ katika mtandao wa Tiktok, Connie Francis amefariki dunia Julai 17,2025 akiwa na umri wa miaka 87.

Taarifa ya kifo chake imetolewa na rafiki yake wa karibu Ron Roberts, ambaye pia ni Rais wa lebo ya muziki ya Concetta Records, kupitia ukurasa wa Facebook Alhamisi, Julai 17, 2025.

"Ni kwa moyo mzito na huzuni kubwa ninawaarifu kuhusu kifo cha rafiki yangu mpendwa Connie Francis usiku uliopita. Ninajua kwamba Connie angependa mashabiki wake wawe miongoni mwa watu wa kwanza kujua habari hizi za kusikitisha. Maelezo zaidi yatafuata baadaye,”ameandika Roberts

Inaelezwa kuwa Connie alilazwa hospitalini kufuatiwa na maumivu makali yanayodhaniwa kuwa ni matatizo ya nyonga ambapo kupitia chapisho lake la Facebook la Julai 2, mwanamama huyo alichapisha taarifa kuwa alitoka salama hospitalini.

Connie alianza kujulikana miaka ya 1950 na 1960, huku akiendelea kuiteka dunia kupitia sauti yake, Septemba 1962 baada ya kutoa wimbo wa "Vacation," wimbo ambao ulifanikiwa kuingia katika chati za Billboard Hot 100 ukishika nafasi ya 10.

Kwa sasa msanii huyo anatamba katika mtandao wa Tiktok kupitia wimbo wa "Pretty Little Baby" ambao umerudi tena kwenye chati za muziki duniani, ikiwa ni zaidi ya miongo sita tangu utolewe kwa mara ya kwanza mwaka 1962.

Awali, wimbo huo ulitolewa kama nyongeza (B-side) katika single ya “I’m Gonna Be Warm This Winter” na pia ulijumuishwa kwenye albamu ya "Connie Francis Sings Second Hand Love and Other Hits," ambayo ilitoka rasmi Aprili 10, 1962.

Kwa kuzingatia mafanikio hayo mapya, lebo ya Concetta Records iliamua kuutoa upya wimbo huo Mei 16, 2025, hatua ambayo imemrudisha Connie Francis kwenye orodha za juu za muziki duniani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags