Basata yatolea tamko vita ya Barnaba, Marioo

Basata yatolea tamko vita ya Barnaba, Marioo

Kutokana na mgogoro unaoendelea kwenye mtandao wa Instagram kati ya wanamuziki Elias Barnabas, ‘Barnaba’ na Omary Ally,‘Marioo’, kuhusu Tuzo za Muziki Tanzania kutotenda haki Basata imetoa tamko.

Kumekuwa na majibizano kwenye mitandao ya kijamii baada ya Marioo kuwatuhumu waandaaji wa tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kuwa hawatendi haki kwani ile ya album bora iliyotolewa mwaka 2023, alikuwa anastahili kushinda yeye.

Mkurugenzi wa Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa ‘Basata’ Edward Buganga akizungumza na Mwananchi leo, amesema utolewaji wa tuzo hizo huzingatia taratibu na kufuata vigezo.

“Hayo ni maoni ya watu, maoni na utaratibu ni vitu viwili tofauti, lakini inapotokea tuzo kuna taratibu zinafuatwa za kuwatunuku watu, kuna vigezo maalumu lazima vinafuatwa kimoja baada ya kingine,” amesema Buganga.

Vita iko hivi, Ikumbukwe mgogoro huo ulianza baada ya Marioo kulalamikia albamu yake (𝐓𝐇𝐄 𝐊𝐈𝐃 𝐘𝐎𝐔 𝐊𝐍𝐎𝐖) kutoshinda tuzo na badala yake ikashinda (Love Sounds Different) ya Barnaba kama Albamu Bora Mwaka 2022, ambayo tuzo yake ilitoka 2023.

“Nawauliza waandaaji, kwa nini mnatoa tuzo kama hazitendi haki? Mnaombaje ushauri kwa wanaoshindania? that was not fair at all. Inasikitisha na inakatisha tamaa. This time around jipangeni.

“Albam ya #Tkyk ilikuwa ina hits kubwa, yaani sio ngoma kali tu, hits kubwa zaidi ya 4, lakini cha kushangaza imeshinda albamu ambayo ina hit song moja, sijui mbili na sio kubwa na hit yenyewe niliandika mimi kwenye hiyo albam”. Aliandika Marioo kwenye ukurasa wake na kupelekea Barnaba kumsusia tuzo hiyo.

Ambapo Barnaba aliandika:"Nimeamua kwenda kubadilisha tuzo hi leo, ku print na nimekuwekea jina lako! Nadhani unastahili so popote uliko nitakuletea au uniambie wapi wakuletee mdogo wangu”.

Kutokana na mgogoro huo, Buganga amesema hadi sasa bado wasanii hao hawajafikisha malalamiko yoyote Basata.

“Suala hilo halijafika kwetu, likitufikia kuna utaratibu wa kufanyia kazi, mlalamikaji na mlalamikiwa, tuna wataalamu wa kutosha wa kushughulikia suala hilo, kuna timu ya wanasheria, likifika tutashughulika nalo.
“Lengo letu ni kufanya kazi vizuri na wasanii wote wana haki sawa na Basata ni nyumbani kwao,” amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags