BASATA na mchakato wa kufanya marekebisho kwenye kanuni zake

BASATA na mchakato wa kufanya marekebisho kwenye kanuni zake

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) chini ya katibu mkuu Kedmon Mapana ameeleza kuwa wapo katika mchakato wa kufanya marekebisho kwenye kanuni zake.

Marekebisho haya yanakuja baada ya malalamiko kutoka kwa wadau waliokuwa wakielezea changamoto walizopitia kutokana na kanuni zilizokuwa zikipunguza fursa za maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano na wadau wa tasnia ya sanaa siku ya jana Ijumaa, Novemba 22, Katibu Mkuu wa BASATA, Kedmon Mapana, alitangaza kuwa baraza hilo limekamilisha mapitio ya kanuni hizo na kuziwasilisha Wizara husika kwa uchambuzi zaidi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mabadiliko haya mapya yataleta mageuzi makubwa na ya msingi. Tumeyasikiliza malalamiko yenu na tumefanya marekebisho mengi, ikiwemo kurahisisha lugha ya kanuni hizo,” alisema Mapana,

Aliendelea kueleza kuwa vifungu vilivyopitwa na wakati vitaondolewa, na kwamba jukumu la BASATA sasa litajikita katika kuwaunga mkono wasanii wa Tanzania na waandaaji wa matukio badala ya kuwazuia.

“Hakutakuwa tena na sheria zinazowatisha Watanzania kwa kuwaambia kile wasichopaswa kufanya. Lengo letu ni kuinua na kuwawezesha,” alisisitiza.

Mabadiliko Muhimu kwa Waandaaji wa matamasha
Moja ya mabadiliko makubwa yatakayowanufaisha waandaaji wa matukio ni kuondolewa kwa malipo ya vibali kwa wale wanaoandaa matamasha kwa mara kwanza.

Chini ya kanuni mpya, BASATA haitahitaji tena waandaaji wa mara ya kwanza kulipa ada za vibali. Badala yake, wataungwa mkono na baraza hilo kwa mwaka mmoja, na malipo yataanza kufanyika baada ya tukio hilo kuwa kubwa.

Mabadiliko mengine muhimu ni kuondolewa kwa ada ya Shs1.5 milioni iliyokuwa ikitozwa kwa wasanii wa kigeni wanaokuja Tanzania kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa kitamaduni au kielimu.

“Mwaka jana, kwaya moja kutoka Congo ilialikwa kuimba kwenye tamasha la Pasaka. Walilazimika kulipa ada ya Shs1 milioni kila mmoja, hali iliyomfanya muandaaji wa tukio hilo kushindwa kumudu gharama. Kanuni hii mpya itaondoa vizuizi kama hivyo na kuruhusu wasanii zaidi wa kimataifa kuja Tanzania,” alieleza Mapana.

Aidha, kanuni hizo mpya zinarahisisha ada za vibali kwa matamasha yanayotoza viingilio. Gharama hizo sasa zitategemea bei ya viingilio. Kwa matamasha yenye viingilio kati kati ya Shs1,000 na Shs50,000, ada ya kibali itakuwa Shs200,000.
Kwa matamasha yanayotoza kati ya Shs51,000 na Shs100,000, ada itakuwa Shs300,000, huku matamasha yenye viingilio za zaidi ya Shs1 milioni yakitozwa ada ya Shs500,000.

Mapokeo Chanya kutoka kwa Wadau
Mabadiliko haya yamepokelewa kwa shangwe kubwa na wadau wa tasnia hiyo. Daniel Joachim, muandaaji wa matamasha, alielezea matumaini yake kuhusu athari chanya ambayo marekebisho haya yatakuwa nayo kwenye sekta hiyo.

“Mara nyingi tumekuwa na changamoto za kuwaalika wasanii wa kigeni kwa ajili ya matamasha ya kielimu kutokana na gharama kubwa za vibali. Mabadiliko haya yatafanya iwe rahisi zaidi kuleta vipaji vya kimataifa, jambo ambalo litaathiri sekta kwa njia chanya,” alisema Joachim.

Mtunzi wa nyimbo za Bongo Flava, Mariam Ramadhani, pia alisifu juhudi za BASATA. “Mabadiliko ambayo tumeyaona hadi sasa yanaonyesha kuwa baraza limejikita kusaidia tasnia hii. Huu ni mwelekeo mzuri, na ninafurahia kile kinachokuja,” alisema.

Mapana aliwasihi wadau kuwa na subira wakati mchakato wa kukamilisha kanuni hizo ukiendelea.
“Tumejidhatiti kuhakikisha malalamiko yenu yanashughulikiwa. Inaniuma kuona changamoto kwenye tasnia. Hebu tushirikiane na kukubali mabadiliko haya,” alihitimisha






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags