Athari za kupeana kazi kwa kujuana

Athari za kupeana kazi kwa kujuana

Na Glorian sulle

Sidhani kama kuna mtu atakuwa hafahamu maana halisi ya kazi/ajira. Kwa tafsiri rahisi hii ni shughuli ambayo mtu hufanya kwa kubadilishana na malipo ya kifedha au faida nyingine, kuna ajira zinahusisha mikataba na zingine zinahusisha makubaliano/ mapatano baina ya mwajiri na mwajiriwa na pengine taasisi.

 

Kila ofisi au taasisi ina mfumo rasmi wa kuajiri au kupata wafanyakazi na vivyo hivyo inapaswa kuwa, katika haya kuna baadhi ya taasisi au ofisi hupeana ajira kwa kujuana huu si mfumo halisi wa kupata ajira katika sehemu husika.

 

Kama ilivyo ada Mwananchi Scoop imeangazia  athari za kupeana kazi au ajira kwa kujuana.

 

Baadhi ya athari za kupeana kazi kwa kujuana ni pamoja na

 

Kupunguza ufanisi

 

Katika mfumo wa kutafuta wafanyakazi moja ya vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na ufanisi wa kazi, hii ni kutokana na misingi ya kampuni iliyojiwekea kuhusu upataji wa wafanyakazi.

Unapofanya maamuzi ya kutoa ajira kwa kujuana moja kwa moja utakuwa kinyuma na malengo ya kampuni, hii itakupelekea kutoa ajira/kazi kwa mtu asiye na vigezo ila tu kwa vile ni ndugu yako au mnafahamiana.

 Hii itashusha ufanisi wa kazi na pengine ukashindwa kumuonya muhusika kwa kumuonea haya.

 

Kupunguza motisha

 

Kuna baadhi ya wafanyakazi ni wawajibikaji katika majukumu wanayokabidhiwa pia wanajifunza kila iitwapo leo, hali hii hubadilika pindi wanapogundua kuwa ajira haitolewi kwa msingi wa uwezo bali kwa kujuana kimsingi hichi kitendo hupunguza motisha kwa wafanyakazi na hatimaye kazi kutokufanyika inavyotakiwa hii hupelekea kampuni kutofikia malengo.

 

Kupoteza imani

Mfumo wa ajira uliojengeka kwa kujuana unaweza kusababisha kupoteza imani katika mchakato wa kuajiri na uadilifu wa shirika au taasisi na hatimaye kampuni au ofisi kutofanya shughuli zake kwa ufanisi unaohitajika.

 

Kupotosha maendeleo ya kitaaluma

 

Watu waliopewa ajira kwa sababu ya kujuana wanaweza kukosa fursa za kujenga uzoefu na ujuzi wa kitaalam ambao ungeweza kupatikana  kwa kuchagua mtu kwa msingi au uwezo, asilimia kubwa ya wanaopewa kazi kwa kujuana hawana vigezo vinavyotakiwa.

Ubaguzi

Kumpa kazi mtu asiye na uwezo ni sawa na kumbagua yule mwenye uwezo zaidi lakini ambao hawana uhusiano wa kifamilia au urafiki na watu muhimu katika uamuzi wa ajira.

 

Kujuana kuna athiri vibaya utendaji wa shirika, kujenga mazingira ya kazi yasiyo ya haki, na kuzuia maendeleo ya kiuchumi na kitaaluma kwa watu ambao wangeweza kuchangia zaidi kwa jamii au biashara.

 

Hivyo basi kama kampuni au taasisi ni vyema kuajiri watu kwa uwezo walionao na siyo  kujuana, kwa kuzingatia haya kutakuwa na utendaji kazi wenye hadhi lakini pia itaongeza kasi ya utendaji kazi na hatimaye kufikia malengo waliyowekwa na pengine kuvuka matarajio.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post