Ally Rehmtullah afunguka nafasi ya kazi ya uanamitindo

Ally Rehmtullah afunguka nafasi ya kazi ya uanamitindo

Ukifikiria kuhusu kazi, watu hufikiria zaidi katika kazi za maofisini kama kazi za benki, na taasisi mbalimbali. Hata hivyo, kuna kazi mbalimbali ambazo zinazidi kutambulika katika miaka ya sasa, ikiwemo katzi katika sekta ya mitindo. 

Sio jina ngeni kulisikia, hasa kama wewe ni mpenzi wa mitindo. Kwani kijana Ally Rehmtullah ni mbunifu na mwanamitindo aliyejipatia umaarufu kutokana na kubuni mavazi, mikoba na vitu vingine vinavyoboresha mwonekano wa mtu.

 Akiwa amezaliwa jijini Dar es salaam, mwaka 1986, katika hospitali ya Agakhan, Ally alianza elimu yake ya shule ya msingi katika shule ya Olimpio, huku sekondari alisomea katika shule ya Mzizima. Baada ya kumaliza elimu yake ya kidato cha nne, akaaenda kuongeza elimu yake nchini Marekani, ambapo alisomea masuala ya mitindo na usanifu kwa takribani miaka minne. 

Safari yake katika mitindo ilianza rasmi mwaka 2007, aliporejea na kuanza kufundisha ubunifu wa mavazi chuo, cha Desktop Publishing Institute (DTP) ambapo alifundisha kwa takribani miezi sita.

Ally Rehmtullah alichagua kazi ya ubunifu kwani ndio kitu alichokuwa akikipenda sana kwani alitamani kufanya mapinduzi katika sekta ya mitindo nchini, vilevile kuimarisha vipaji vya wabunifu chipukizi nchini, na ndio maana alianza kwa kufundisha mitindo baada ya kupata ujuzi nchini Marekani. 

“Fedha nilizopata wakati ninafundisha chuoni hapo, ziliniwezesha kuanzisha biashara iliyonijengea jina nililo nalo hadi sasa,” aliongeza Rehmtullah.

Miaka 12 baadae, Ally Remtullah bado anabaki kuwa katika ya wanamitindo wakubwa nchini, ambao sio tu wameweza kuliteka soko la ndani, lakini soko la nje pia. Sasa jina la Ally Rehmtullah linarindima Afrika nzima, akifanya shoo za mitindo katika nchi mbalimbali, ikiwemo Afrika Kusini.

Alipataje mafanikio kupitia kazi ya mitindo? 

Alianza na mtaji wa Tshs 35,000, gharama aliyoitumia kununua vitambaa, Pamoja na malipo ya fundi, ili kutengeneza nguo yake ya kwanza. Kupitia uthubutu huo wa kuanza mitindo, aliweza kufanya kazi mbalimbali ndogo ndogo hadi biashara ikakua, na hatimaye akaweza kuajiri wafanyakazi wengine 25 wa kumsaidia.

Hata hivyo, baada ya juhudi nyingi, hatimaye alipata fursa ya kusafiri nchi za nje kwa ajili ya kutangaza kazi zake, na kufanikiwa kuonyesha ubunifu wake kwenye majukwaa makubwa ya mitindo, kama vile London Fashion Week na South Africa Fashion Week. 

Ally ni mmoja wa wanamitindo waliofanikiwa kushiriki katika Tuzo za Redd's African Fashion Design (RAFDA), iliyofanyika Desemba 2006, kwa kubuni gauni la jioni zuri kwa mshereheshaji Jokate Mwengelo ambaye pia alikuwa balozi wa mwaka wa Redd's kwa wakati huo.

Kazi hiyo ilimpelekea kuwavalisha viongozi wakubwa hapa nchini wakiwemo Wabunge, Wakuu wa Wilaya, pamoja na wasanii maarufu kama vile Diamond Platnumz kwenye wimbo wake wa Nataka Kulewa, Elizabeth Michael, Chidi Benz kwenye video yake ya Masha'allah, pamoja na Navy kenzo.    

Changamoto za kazi hiyo

  • Kutokana na viwanda vingi vya nguo nchini kutozalisha kwa wingi na ubora unaohitajika, Rehmtullah anasema wabunifu wanalazimika kuagiza malighafi kutoka nje jambo linawaongezea gharama za uzalishaji.

“Tunalima pamba na kuuza nje ya nchi lakini hatujitoshelezi nchini na wabunifu ni miongoni mwa kundi linaloathirika zaidi. Serikali iliangalie hili na kuhakikisha viwanda vya uzalishaji vinaongezwa nchini,” alisema Rehmtullah..

  • Soko limebadilika kwa sasa, kwani mitindo imepungua sana kwa sababu wabunifu wengi.

Aliongeza, “Wafanya biashara kwa kutumia mitandao wameongezeka ukilinganisha na hapo awali, hivyo yale matamasha yaliyokuwa yanaandaliwa kama mwanzo siku hizi ni nadra kutokana mabadiliko ya teknolojia.”

Nafasi ya Soko la Mitindo Duniani

 

  • Wakati wabunifu wakihangaika kuwa wabunifu, mwaka 2015 Jarida la The Economist liliitaja Tanzania kuwa katika nafasi ya 17 kwenye orodha ya nchi zenye uwekezaji mkubwa wa viwanda, vilevile, kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Tanzania ina zaidi ya viwanda 54,000 - Dar es Salaam vikiwepo viwanda vikubwa na kati 157.

 

  • Vazi ambalo linakubalika sana kwenye kazi yake ni vitenge pamoja na vitambaa ambapo ameweza kupata umaarufu mkubwa kwenye shindano la london fashion week ambapo alitoka kwenye chipukizi hadi kufikia kuwa maarufu. 

 

  • Soko kubwa la soko la mitindo ni wanawake, na ndio maana anavalisha hao zaidi.

Madhalani, Meneja Masoko na Mauzo wa kiwanda cha Urafiki Selina Otacho alieleza kuwa teknolojia ndio tatizo kubwa kwa viwanda vya uzalishaji kama Urafiki kwani  tatizo hilo linawarudisha nyuma katika masuala ya uzalishaji wa malighafi zilizopo.   

Gharama za uzalishaji wa teknolojia hii ni kubwa hata taka inayozalishwa kutokana na teknolojia hii ni kubwa pia ukilinganisha na teknolojia za nchi za wenzetu.  

"Unakuta kiwanda cha Urafiki gharama nitakazotumia mita 1 ya kitambaa kinachozalisha khanga nitatumia shilingi elfu 2500 au zaidi wakati huo nimeweka bei ya hasara kabisa" alisema. 

 Akijibu suala la Ubora wa bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini jambo ambalo linalalamikiwa na wabunifu anaeleza kuwa ubora wa bidhaa unasababishwa na teknolojia.  

 "Kama unatumia mashine iliyopitwa na wakati yaani ni ya muda mrefu huwezi kuzalisha kitu chenye ubora" aliongeza.

Kama huna mashine bora, kutengeneza nyuzi uwe na uhakika kabisa kuwa ile nyuzi itakapotoka haitatoka kwenye ubora, vilevile kama huna mashine bora ya kufuma kitambaa, huwezi kutoa kitu ambacho kinaubora uliotarajia. 

Pia amesisitiza kuwa wabunifu watakiwa kuungana kwa pamoja na viwanda vya uzalishaji ili kushauriana kuhusiana na hali ya soko na mambo yalivyobadilika kufanya hivyo kutasaidia kukuza soko la uzalishaji hapa nchini. 

Hata hivyo ameiomba serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukiwezesha kiwanda hicho kwa teknolojia ya kisasa na kutupia jicho kwenye kiwanda hicho kwa kuwawezesha kuwaletea mashine za kisasa ambazo zitaendana na soko la dunia.

Kazi ya ubunifu na uanamitindo ni kazi ambayo sasa inapewa heshima kubwa, na vijana wengi wamekuw wakiingia katika tasnia hii. Uboreshwaji wa viwanda, Pamoja na malighafi husika kutawawezesha vijana wengi kuweza kubuni mitindo mbalimbali, na kama kijana Ally, waweze kutengeneza ajira kupitia sekta hii.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags