Rhobi Chacha
Taasisi ya Aisha Masaka Foundation, iliyoanzishwa na mchezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania na klabu ya Brighton & Hove Albion F.C. ya Uingereza, Aisha Masaka, kwa kushirikiana na Amani Foundation inayoongozwa na msanii wa hip hop Frida Amani, wamezindua kampeni iitwayo “Amka Malkia” yenye lengo la kumsaidia mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.
Uzinduzi wa Kampeni hiyo umeambatana na Mchezo wa mpira wa miguu ambao utachezwa Juni 06, 2025 kwenye uwanja wa KMC Mwege jijini Dar es Salaam, na utahusisha timu mbili ambazo ni Timu Aisha Masaka pamoja na timu ya Frida Amani ambapo mapato ya fedha yatakayo patikana katika mchezo huo yataenda kusaidia katika sekta ya elimu mkoani Lindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mei 16, 2025, wakurugenzi wa Taasisi hizo mbili, wameeleza kuwa kampeni hiyo ni mahususi kwa ajili ya kuwajengea wasichana kujiamini pamoja na kuwafungulia milango ya mafanikio.
Kwa upande wa Aisha Masaka amesema ndoto yake ya kucheza mpira ilianzia akiwa shuleni hivyo aliona ni vizuri kuanza kwa kusaidia Wanafunzi kupitia kampeni hiyo.
“Nitashirikiana na wachezaji wenzangu wa ndani na nje ya Tanzania kwa wachache watakaopata nafasi ambao hawatakuwa na ratiba za kubana kwenye vilabu vyao watashirikiana nami kucheza mechi hiyo ya Juni 6, 2025,” amesema Aisha
Naye msanii wa Hip Hop Frida Amani amesema, katika mechi hiyo naye ataonesha kipaji chake cha kucheza mpira ambacho watu wengi hawakifahamu.
“Amka Malkia niwakati sasa wa mwanamke kujiamini na kujiongeza kwa kutimiza ndoto zao, kwa kile alichokuwa akikitamani ,siku hiyo mimi nitacheza mpira wa miguu, kitu ambacho watu wengi hawajui kama nina kipaji hicho, nitaandaa kikosi changu kitaingia nacho uwanjani ila najua timu Aisha Masaka tutawafunga magoli mengi tu,”amesema Frida

Leave a Reply