20 percent: Siwezi kujishusha kwa sababu ya pesa

20 percent: Siwezi kujishusha kwa sababu ya pesa

Aisha Charles

Isikiwapo ngoma iitwayo Mama Neema au Money Money, wengi inawakumbusha miaka 13 iliyopita, kwa sababu ndiyo nyimbo zilizokuwa zikifanya poa kutoka kwa mwanamuziki  20 Percent ambaye mwaka 2011 alinyakuwa Tuzo tano za Kilimanjaro Music Awards katika vipengele tofauti tofauti.

20 Percent aligusa nyoyo za mashabiki kutokana na tungo zake zilizokuwa zimebeba ujumbe mzito, zinazogusa jamii ya Kitanzania. Utakumbuka kati ya nyimbo zake ni Tamaa Mbaya, Nia Yao, Ningekusamhe na nyingine nyingi.

Akizungumza na Mwananchi Scoop 20 Percent ameeleza namna ambavyo kutoogopa kulivyofanya ajizolee umaarufu miaka 14 iliyopita.

 “Siku zote asili yangu ya muziki ipo kwenye damu na ninashukuru wakati naanza muziki haikuwa ngumu jamii kunikubali kutokana na uhalisia wa ujumbe wangu, na kusema kweli mimi huwa siongopi katika muziki ndiyo maana niliutambulisha vizuri muziki wangu tofauti na sasa”.  Alisema

Pia aliongezea kuwa kukubalika na kuutambulisha muziki wake mbele ya mashabiki kulimfanya azidi kujituma katika ubunifu wake wa kufuatilia kinachoendelea katika jamii ambayo inapokea kazi zake.

Hawezi kujishusha kwa sababu ya pesa

Ameeleza kuwa yeye hawezi kujishusha kwa mtu hasa aliyemzidi pesa kwa sababu anajiamini hivyo hawezi kuwa mtumwa wa mtu.

“Ifike mahali kila mtu ajiamini, kama mimi siwezi kutoka nikaenda kwa mtu kumnyenyekea kwa sababu yuko juu na ana kipato.” alisema

Pia amewataka wasanii wakongwe kama yeye kutojishusha kwa kutaka pesa kwa sababu ni kujidhalilisha.

“Ukiona binadamu anaacha kujiamini huo unakuwa utumwa na kujidhalilisha kuna mtu mmoja aliwahi kuwa chini ya wadogo zake lakini ameishia kudhalilika tu na wadogo zake wakanufaika kupitia yeye, nataka wasanii wengine watambue kwamba mtu akitaka kukusaidia lazima na yeye afaidike” alisema Twenty. 

Sababu ya kutosikika kama mwanzo 

Twenty ameeleza sababu za ngoma zake kutofanya vizuri kama ilivyokuwa zamani

“Muziki ni kama chakula na una wakati kwa sababu ukitaka kula huwezi ukala kila siku chakula cha aina moja sasa inategemea kwa sasa watu wanapenda muziki wa aina gani na ndiyo maana kwa wakati huu muziki wa aina yangu hausikilizwi sana kama zamani.

Lakini siyo kwamba sifanyi muziki la hasha nafanya ila ni ngumu kwa sasa muziki wa aina yangu kusikika masikioni mwa watu kwa sababu sasa tuna vizazi tofauti kama vizazi vya Instagram haviwezi kupata muziki wangu kwa urahisi”. Alisema Twenty

Wasanii wamehamia kwenye muziki wa kuiga

Ameeleza jinsi wasanii walivyojikita kwenye muziki wa kuiga kutoka nje na kuacha asili yao ya zamani.

“ Sasa hivi wanamuziki wamekuwa wakiiga sana muziki wa nje yaani hawashughulishi akili zao,  hii itaendelea kwa Tanzania kutokana na wasanii wengi badala ya kufanya kazi ya kutoa ujumbe, wao wanafanya biashara” alisema msanii huyo.

Hakuna anayeimba Amapiano Bongo

Twenty amedai kuwa kwa hapa Bongo hakuna anayeweza kuimba muziki wa Amapiano bali wasanii wamekuwa wakiiga muziki huo lakini siyo kuimba kama wenyewe wa Afrika Kusini.

 

“Kwanza hapa Bongo bado sana na hakuna anayeweza kuimba muziki wa aina hiyo kwa sababu wenyewe Afrika Kusini huwa wanasikiliza Amapiano za kwao tu na ndiyo wanazoziamini sisi tumekuwa watu wa kuiga tu kwa kile wanachofanya wenzetu”. Alisema Twenty

Hata hivyo aliongezea kwa kusema siku zote wasanii wa Bongo hawana misimamo katika kusimamia chao.

Ana mpango wa kuanzisha bendi

Twenty amesema ana mpango wa kuanzisha band, ambayo hata asipokuwepo itaendelea kufanya vizuri kutokana na watu atakaoshirikiana nao.

“Shauku yangu kubwa ni kuwanufaisha watu wanaonizunguka kwa kuwarithisha ninachokifanya na kuwapatia ajira kupitia muziki maana ninampango wa kuanzisha bendi ambayo hata nisipokuwepo itaendelea na watu wengine kufaidika kupitia bendi hiyo kwa sababu nina watu wengi ambao ni zao langu ” alisema Twenty.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post