Ukweli ni kwamba si jambo la kawaida kukutana na gari, pikipiki au baiskeli yenye tairi la rangi tofauti na nyeusi, na hata kama kukiwa na rangi tofauti na hiyo basi itawekwa kwa mstari mdogo pembeni na siyo eneo ambalo tairi linakanyaga kwenye lami.
Si hivyo tu kama umekuwa mfuatiliaji basi utakuwa umegundua kuwa tairi hata likiwa jipya lazima liwe na vipira virefu vilivyochomoza ambavyo watu wengi huviita vinyweleo vya tairi. Kutokana na hayo fahamu kuwa vyote vimewekwa kwa makusudi na si kwa bahati mbaya.
Matairi huwa na rangi nyeusi ili yaweze kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu, kutumika kwa muda mrefu, na kutoathiriwa na joto kirahisi. Rangi hiyo hutokana na kemikali kwenye mpira inayojulikana kitaalamu kwama ‘Carbon Black’ ambayo ndiyo huipa rangi nyeusi na kuifanya iwe imara.
Ndiyo maana duniani kote wanaitumia kwenye matairi, inaelezwa kuwa asilimia 70 ya kemikali hiyo inayozalishwa duniani, hutumika kutengenezea matairi mbalimbali. Aidha Carbon black huisaidia tairi kutoathiriwa na gesi ya ozone kwani ni moja ya vitu ambavyo huchangia kuharibika sana kwa tairi.
Mbali na uwepo wa rangi nyeusi, vinyweleo vidogo vya mpira kwenye tairi ambavyo watu wengi hasa watoto hupenda kuvivuta na kuziondoa kitaalamu vinatajwa kutokuwa na kazi yoyote yaani viwepo au visiwepo ni sawa tu. Lakini uwepo wake kwenye tairi hujitokeza wakati tairi likiwa linatengenezwa kiwandani.
Leave a Reply