Zijue sababu 8 zinazomfanya mwanamke kukosa hedhi

Zijue sababu 8 zinazomfanya mwanamke kukosa hedhi

Na Shufaa Nassor

Wanawake wengi wana tatizo la kukosa hedhi!

Kukosa hedhi au kubadilika kwa mzunguko wa hedhi inaweza kuwa tatizo kubwa kulitatua. Kwasababu hedhi ndio kiashiria chema kuonesha hadhi ya mwanamke. Kama ukikosa hedhi lazima utaanza kupata msongo wa mawazo na kukosa amani.

Kukosa hedhi na kuvurugika kwa mpangilio wa hedhi huwakumba wanawake wengi sana kwa sasa hasa kutokana na mitindo ya maisha inayopelekea kuvurugika kwa homoni za kike.

Mpangilio wa hedhi unaratibiwa na vichocheo kutoka kwenye tezi na ubongo, kwa hivo ni muhimu kurekebisha mtindo wa maisha unaovuruga homoni zako na kukupelekea kuvurugika kwa hedhi.

Ijue Hatari ya Kuvurugika na Kukosa Hedhi ni Kubwa

Kwa mwanamke ambaye ni mzima wa afya kikawaida hutoa yai moja lililokomaa kila baada ya siku 25 mpaka 28 tayari kwa kurutubishwa na mbegu ya kiume kwenye siku za hatari. Japo mzunguko wa hedhi kwa kila mwanamke unatofautiana, wanawake wengi wenye afya njema mzunguko wao huchukua mwezi mmoja.

Mwanamke anapokoma kupata hedhi kabla ya kipindi chake inaonesha kwamba kuna tatizo la kiafya. Kupata hedhi ya kawaida isiyoambatana na maumivu makali kila mwezi ni kiashiria kwamba homoni zako zimebalansi na mfumo wako wa uzazi unafanya kazi ipasavyo.

 Je, Homoni Kuvurugika ni Chanzo cha Kukosa Hedhi? 

Kinyume chake pia ni ukweli kwamba ukiwa unakosa hedhi, hedhi isiyo na mpangilio mzuri, maumivu makali wakati wa hedhi na hedhi kuchukua siku nyingi zaidi ya 7 ni kiashiria kwamba homoni zako zimevurugika. Kama una uhakika kwamba huna ujauzito na unakosa hedhi basi siyo kitu cha kuchukulia kawaida unahitaji kujua chanzo cha tatizo na kuchukua hatua.

Tafiti nyingi zinasema kwamba kundi kubwa la wanawake huficha jambo hili na kutoliripoti kwa daktari pale wanapokosa hedhi mara kwa mara 

Kitendo hiki ni hatari kwani kukosa hedhi na kuvurugika kwa homoni kunaweza kuleteleza matatizo mengine makubwa ya kiafya kama, magonjwa ya moyo, kupungua kwa nguvu ya mifupa, na ugumba.

Je, mzunguko wa hedhi unafanyaje kazi?

Kikawaida kila mwezi mwanamke hutoa yai moja ili lirutubishwe kutengeneza kichanga. Pale yai lisipotolewa kwenye kikonyo chake tunaita anovulation. Moja ya dalili kwamba mayai yako yanapevuka lakini hayatolewi ni kukosa kabisa au kuvurugika kwa hedhi.

Kwa wanawake wasio na ujauzito wenye umri wa kuzaa kuanzia miaka 15 mpaka 40 na hawapati hedhi, hiki ndio kisababishi cha kushindwa kushika mimba kwa karibu 30%.

  • Homoni

Mpangilio wa hedhi unaratibiwa na vichocheo au homoni za mwanamke hasa estrogeni. Homoni za estrogen husaidia kujenga ukuta na mazingira mazuri kwa ajili ya ukuaji wa kiumbe kinachozalishwa. Mwanamke akishakoma hedhi uzalishaji wa estrogen hupungua sana na ndio maana unaanza kukosa siku zako.

Kwa wanawake walio kwenye umri wa kuzaa, kuwa na kiwango kidogo sana cha estrogen husababisha kukosa hedhi na kuvurugika kwa mpangilio wa hedhi. Kwahivo unapoenda hospitali kishiria cha kwanza kwamba una kiwango kidogo cha estrogeni ni ikiwa unakosa siku zako.

Zijue Sababu za mara kwa mara Zinazopelekea Kukosa hedhi na Kuvurugika kwa Mpangilio wa Hedhi.

Ukiachilia mbali ujauzito na kukoma hedhi ambavyo vyote hivi ni vipindi vya kawaida kwa mwanamke kukosa hedhi. Zifuatazo ni sababu ambazo hupelekea mwanamke kukosa hedhi

  • Msongo wa mawazo

Kikawaida mwili unapokutana na kitu cha kuogofya ama kinacholeta msongo wa mawazo unatunza nishati kubwa ili kuzielekeza kupambana na changamoto iliyopo mbele yako. Kwa hivo kila mara unapokuwa na msongo wa mawazo utendaji wa shuguli zingine za mwili unapungua na kudhoofika ikiwemo upevushaji wa mayai.

Homoni ya estrogen inapozalishwa kwa kiwango kidogo pamoja na homoni zingine kama homoni ya LH na FSH ukuta ambao humeguka kila mwezi kutoka pamoja na yai hautajengwa na hivo kupelekea ukose hedhi.


Je, Kwanini Mwili Unapunguza Kasi ya Upevushaji Wa Mayai Wakati Wa Msongo Wa Mawazo?

Mwili unatambua kwamba upo kwenye kipindi cha hatari na unatakiwa upambane ili uishi kutokana na hatari inayokuwa mbele kwa hivo maisha ni kitu cha kwanza ndipo swala na hedhi lifuate. Mwili utatengeneza stress homoni kwa wingi kama cotisoli na adrenalini ili kukuandaa kupambana, ama kukimbia hatari iliyopo mbele yako.

Fikiria pale unapotembea usiku na ukaona kitu kisicho cha kawaida mbele yako, tazama mwili unavobadilika, sasa mabadiliko ya homoni pale unapokutana na kitu cha hatari ni sawa na vile unapopata msongo wa mawazo. Kadiri mawazo yanavokuathiri ndipo unaharibu mpangilio wako wa mwili na kukupelekea ukose hedhi.

  • Lishe mbaya

Lishe mbaya yenye upungufu wa virutubisho ikiwemo vitamini na madini na yenye sukari na viambata vya kuongeza ladha kwa wingi hupelekea tezi za *Adrenal na Thayroid* kufaya kazi kupita kiasi. Kitendo hichi hupelekea uzalishaji wa kichocheo cha cotisoli ambacho kinapunguza uzalishaji wa homoni za uzazi.

Cortisol inapokuwa nyingi zaidi pia taweza kuleteleza madhara mwilini kama udhaifu wa mifupa, ngozi kuharibika, tishu za ubongo  na misuli kudhoofika. Kwahivo mtiririko huu unapojirudiarudia  kila mara ndipo hali ya mwili huwa mbaya zaidi.

  • Uzito mdogo kupita kiasi

Ili kupima uzito wako kama uko sawa kiafya, tunatumia kipimo cha BMI yaani body mass index ni kipimo kinachotumika kupima uwiano wa uzito na urefu wako. BMI= Uzito wako kwa kg gawanya kwa (urefu kwa mita x 2). BMI kuanzia 18.5 mpaka 25 inaonesha kwamba uzito wako ni mzuri. Ukipata zaidi ya 25 maana yake uzito wako ni mkubwa na ukipata chini ya 18.5 ni kwamba una uzito mdogo kupita kiasi. 

  • Kufanya mazoezi kupita kiasi

Mazoezi ni muhimu kwa mwili katika kurekebisha athari za msongo wa mawazo, kuweka sawa shinikizo la damu, usingizi mzuri na kuweka sawa uzito wamo.

Ila kumbuka kufanya mazoezi kupita kiasi kunachosha sana mwili kupelekea uzalishaji mkubwa wa cotisoli ambayo ndio kizuizi cha kuzalishwa kwa homoni za uzazi. Kwahivo hakikisha unafanya mazoezi mara 3 kwa week na yasiwe mazoezi yanayokula nguvu yako nyingi na kukuacha mdhaifu.

  • Matatizo kwenye tezi ya Thairodi.

Tezi ya thairodi ni kiungo chenye umbo la kipepeo. Kiungo hichi kipo kwenye shingo chini ya koromeo la sauti. kazi kuu ya Tezi hii ni kuzalisha homoni za (T3) na (T4), ambazo kwa pamoja hufanya kazi ya kurekebisha mzunguko wa damu na kazi mbalimbali za mwili.

Matatizo kwenye tezi ya Thairodi kama kushuka kwa uzalishaji wa homoni ama tezi kufanya kazi kupita kiasi huweza kuleta mabadiliko pia kwenye kiwango cha estrogeni na cotisoli. Kiwango cha cotisoli kwenye damu kinapokuwa kingi hupunguza uwezo wa tezi ya thairoidi ambapo matokeo yake ni kushuka kwa kazi za mwili kama upevushaji wa mayai na uzalishaji wa homoni za kike

  • Matumizi ya dawa za kupanga uzazi

Baadhi ya wanawake hukosa hedhi kwa muda mrefu baada ya kuacha kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Japo madactari hushauri kwamba hali itakaa sawa baada ya kuacha kumeza vidonge lakini bado hali huwa mbaya kwa wanawake wengine kwani tayari vidonge vimevuruga vichocheo. 

Kikawaida mpangilio wa hedhi unakuwa na kipindi cha kupanda na kushuka kwa homoni za estrogeni na progestene kwa kupishana, lakini vidonge vya uzazi wa mpango hufanya estrogeni kuwa juu muda wote na kuudanganya mwili kwamba una ujauzito wakati huna na hivo kukosa hedhi kabisa. Inachukua miezi ama miaka mingi mpaka mwili kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

  • Ugonjwa wa PCOS

Polycyst ni wingi wa neno cyst, Neno cyst ni kitu chenye uwazi kwa ndani na kimezungushiwa ukuta mwembamba na laini (Membrane). Na mle ndani kunaweza kukaa damu,usaha,maji nk. kwa upande wa mwanamke hizo follicles nyingi ambazo zimekomaa na zimeshindwa kutoa mayai zinafanishwa na Cysts .Sasa inapotokea Kila mwezi hupati hedhi na vimbe hizi zinakuwa nyingi tunaziita Polycyst.

Na mkusanyiko wa dalili mbalimbali kama uzito mkubwa na kitambi, kupanda kwa sukari kwenye damu, kuwa na chunusi nyingi, kuota ndevu na hedhi kuvurugika ndizo tunaziita syndrome au Polycystic Oarian syndrome. Wanawake wenye PCOS hukosa hedhi kutokana na kuvurugika kwa homoni zao.

  • Alegi ya vyakula 

Mwili kushindwa kuchakata baadhi ya vyakula kama vyakula vya ngano na maziwa ama kuwa na aleji na vyakula baadhi husababisha mwili kukosa virutubisho muhimu  na hivo kuzalisha magonjwa sugu

Je, suluhisho lake ni Nini?

Unapohisi moja ya changamoto za kukosa hedhi usisite kwenda kituo cha karibu chenye huduma rafiki au kuonana na daktari kwa uchunguzi zaidi na matibabu ya haraka!!

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post