Wasanii Bongo walivyokwepa albamu na kugeukia EP

Wasanii Bongo walivyokwepa albamu na kugeukia EP

Utoaji wa albamu kwa wasanii ni moja ya kitu kinachotafsiriwa kama mafanikio yake kwenye kazi ya muziki. Licha ya kuwa albamu hutafsiriwa kwa upande huo, lakini kwa sasa wasanii wengi wanaonekana kuondoka kwenye upepo huo na kuhamia kwenye utoaji wa EP (Extended Playlist).

Tafsiri ya EP ni rekodi ya nyimbo zilizowekwa pamoja lakini huwa chache kuliko albamu, mara nyingi zina nyimbo hadi nane na zina muda wa kucheza kati ya dakika 15 hadi 30.

Huenda hufanya hivyo kutokana na matakwa ya Dunia kwa sasa yalivyo. Ni zama za Kidijitali tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wasanii wengi walipimwa au kujitengenezea ukubwa zaidi kwa kutoa albamu.

Uwepo wa mtindo huu mpya unaonekana kuwa moja ya mabadiliko yanayopelekea albamu kutoka kwa nadra huku EP na ngoma mojamoja kuonekana kuwa dili licha ya kuwa haifuti uhalisia kuwa albamu ni heshima kwa msanii katika kazi yake ya sanaa.

Akizungumzia sababu ya wasanii wengi kuhamia kwenye utoaji wa EP, Mwanamuziki wa Hip-Hop, Rashid Rais 'Maarifa Big Thinker' amesema kufanya albamu au EP ni mtazamo wa msanii husika kulingana na biashara yake.

"Ni maamuzi ya msanii kufanya EP au albamu kutokana na sababu za kibiashara. Kuna watu wananufaika kwa kutoa albamu na wengine EP lakini vilevile kuna ambao wamefanya hivyo na haijawapa mafanikio," amesema Maarifa anayetamba na ngoma kama Sishirikishi Mtu, Karibuni Kibaha na Acha Nipepee.

Mbali na hayo amesema kuwa wakati mwingine upepo wa gemu hupelekea mabadiliko hayo kwenye muziki.

 "Mambo haya wakati mwingine inategemea na upepo ulivyo. Unatakiwa kujua watu wanataka nini katika wakati gani.

Ukiachana na maudhui pamoja na biashara, watu pia wanataka burudani hivyo lazima uzingatie yote hayo katika kufanya maamuzi," amesema Maarifa aliyeanza muziki mwaka 2019 na sasa ametoa ngoma tano huku akifanya Freestyle kibao na kushirikishwa kwenye ngoma kadhaa.

Naye mkali wa Hip-Hop, Stamina amesema wasanii wengi wanaogopa kutoa albamu kutokana na uzembe wao.

"Wasanii wamekuwa wakitoa EP kwa sababu ya uvivu na kukosa ubunifu, wanakwepa kufanya albamu kwa sababu inahitaji muda mwingi zaidi wa kuandaa kwani inakuwa na nyimbo nyingi zenye dhamira za kufuatana kwa hiyo mimi kwa upande wangu EP siyo mbaya lakini albamu ni kitu bora zaidi hasa kwa upande wa Hip-Hop,” amesema Stamina mwenye albamu moja iitwayo Paradiso.

Kwa upande wake mtayarishaji wa muziki nchini, Marco Chali amesema wasanii wamehamia kwenye EP kwa sababu haichukui nyimbo nyingi.

"Ukizungumzia albamu ni kitu kikubwa kwa hiyo wanamuziki wameingia kwenye kutoa EP kwa sababu haichukui nyimbo nyingi ni kama staili ya sasa na hasa imekuwa ikitumika kwa wanamuziki chipukizi kwenye kujikita zaidi katika soko la muziki na kwenda na wakati," amesema Marco Chali.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post