Wanigeria wapigwa na kitu kizito Grammy 2024, Tyla apeta

Wanigeria wapigwa na kitu kizito Grammy 2024, Tyla apeta

Peter Akaro

Dar es Salaam: Kama kuna kitu wasanii wa Nigeria walikuwa na uhakika nacho katika tuzo za 66 za Grammy 2024, ni kuondoka na ushindi mnono kutokana na kuchaguliwa kuwania vipengele vingi, pamoja na kupewa nafasi ya kutumbuiza lakini wamejikuta wakipigwa na kitu kizito.

Tuzo hizo zilizoanzishwa Mei 4, 1959 zikifahamika kama Gramophone, zimetolewa usiku wa kuamkia leo katika ukumbi wa Crypto.com Arena Jijini Los Angeles nchini Marekani ambapo wasanii wengi wakubwa wa Nigeria walihudhuria.

Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021 ndiye msanii wa Nigeria na Afrika aliyechaguliwa kuwania vipengele vinne, Davido vitatu, huku Asake na Ayra Starr wakipata kimoja kimoja.

Mkali wa ngoma 'Last Last' Burna Boy alitajwa vipengele vya Best Global Music Album (I Told Them), Best African Music Performance (City Boys), Best Global Music Performance (Alone) na Best Melodic Rap Performance (Sittin' on Top of the World).

Naye Davido ambaye ni mara yake ya kwanza kuwania Grammy alitajwa vipengele vya Best Global Music Album (Timeless), Best Global Music Performance (Feel, Unavailable) na Best African Music Performance.

Hata hivyo, Burna Boy, Davido na wenzao wameambulia patupu katika vipengele vyote na sasa watarejea nyumbani kwao bila kitu chochote ambacho hata mashabiki na wadau wao hawakukitarajia hapo awali. 

Akizungumza kwa uchungu kupitia Insta Live Mtangazaji kutoka Nigeria, Adesope Shopsydoo amelalamikia kitendo cha Davido kukosa tuzo na kutupa lawama kwa waandaaji, kwa madai wamemtumia msanii huyo kutangaza tukio lao kisha wakamtosa. 

Utakumbuka Davido alishiriki hafla zote zilizoandaliwa na Grammy kuelekea tukio hilo kubwa la kiburudani duniani, huku Burna Boy akitumbuiza na kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kutoa burudani katika jukwaa hilo.

Staa wa Amapiano kutokea Afrika Kusini, Tyla, 22, ndiye msanii pekee wa Afrika aliyeibuka mshindi Grammy 2024 ambapo ameshinda kipengele cha 'Best African Music Performance' baada ya kuwabwaga Asake, Burna Boy, Davido na Ayra Starr.

Ushindi huo unakuja wiki mbili baada ya Tyla anayetamba na wimbo wa 'Water' kusema anaamini atashinda tuzo hiyo kwa kile alichoeleza kama ameweza kuchaguliwa kuwania, basi ushindi pia unawezekana.

"Naamini naweza kushinda tuzo ya Grammy mwaka huu, walipokuwa wanatangaza wateule hata sikufikiria kama nina nafasi ya kuteuliwa, timu yangu ilikuja chumbani kwangu na kunipa simu niangalie tu, kisha niliona nimeteuliwa," alisema Tyla.

Davido kupitia mtandao wa X, zamani Twitter amempongeza Tyla kwa ushindi huo na kusema ni mkubwa kwa Afrika ambayo kwa mara ya kwanza mwaka huu imepewa kipengele chake pekee (Best African Music Performance) na ndicho alichoshinda Tyla.

Ikumbukwe hadi sasa Beyonce kutoka Marekani ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za Grammy duniani kwa muda wote akiwa ameshinda 32, aliandika rekodi hiyo Februari 2023 baada kuivunja rekodi ya George Solti wa Hungary mwenye tuzo 31.

Chini ni orodha ya baadhi ya washindi wengine wa Grammy 2024.

 

Jay-Z - Impact

 

Shakti - Best Global Music Album

 

Taylor Swift - Album Of The Year (Midnights)

 

Gaby Moreno - Best Latino Pop Album (X Mi (Vo.1)

 

Killer Mike - Best Rap Album, Best Rap Performance, Best Rap Song

 

Lil Durk - Best Melodic Rap Performance (All My Life)

 

Victoria Monét - Best R&B Album(JAGUR II) & Best New Artist

 

Kirk Franklin - Best Gospal Song (All Things)

 

Alicia Keys - Best Immersive Audio Album

 

The Beatles - I'm Only Sleeping

 

Billie Eilish - Song Of The Year (What Was I Made For)

 

Miley Cyrus - Best Pop Solo Performance

 

Jack Antonoff - Producer Of The Year

 

SZA - Best Progressive R&B Album (SOS)

 

Cocojones - Best R&B Performance
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags