Wanawake watakiwa kutumia akili na nguvu zao kufanyakazi kwa bidiii

Wanawake watakiwa kutumia akili na nguvu zao kufanyakazi kwa bidiii

Wanawake nchini wametakiwa kutumia akili na nguvu walizonazo kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuwania nafasi za uongozi huku wakisisitizwa kuacha kusema tamaduni zinawakwamisha.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) upande wa fedha na utawala, Zainabu Mshana wakati wa kongamano la wanawake wa chuo hicho.

Mshana amesema tamaduni zipo hivyo wanawake wanapaswa kuzichukulia kama moja ya vitu zinazofanya watu kuheshimiana na wala hazijachukua akili, uwezo wala nguvu zao kufanya kazi.

“Mwanzoni tulikuwa tukisema tamaduni tulizonazo ndizo zinakwamisha au ni kikwazo kwa wanawake kufikia malengo yao, sasa hivi tuache hiyo kwani hizi tamaduni wala hazijachukua akili, uwezo wala mikono yetu.

“Tuamke sasa tuweze kujitoa katika kufanya kazi huku tukitambua kuwa hakuna ardhi au nafasi iliyowekwa kwaajili ya wanaume au mwanamke peke yake, kila mtu anaowajibu wa kuongoza na kushika nafasi mbalimbali kama utajituma na kuwajibika ipasavyo,” amesema   

Aidha amesema NIT wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha wanawake wanakuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kutimiza malengo waliojiwekea.

Awali akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Chuo NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema wanawake wakiwa mstari wa mbele kwenye masomo ya sayansi hasa ya hisabati, jamii itapata maendeleo haraka.

Aidha Prof. Mganilwa amesema kuwa Chuo hicho wiki mbili zilizopita kimetoa timu maalumu ya hamasa iliyokwenda Mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwenye shule za mikoa hiyo kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya Sayansi.

“Tunaye mwanafunzi wa kike hapa aliyepata daraja la juu la kwanza la Hesabu ambaye tunatazamia kumpatia ajira hapa kwani tunaimani huyu anapokwenda kuhamasisha wanafunzi wengine ataeleweka zaidi kwa kuwa yeye ni miongoni mwa wanawake walioweza kusoma masomo hayo,” amesema

Hata hivyo ameeleza kuwa chuo hicho kina mifano mingi yenye kutoa hamasa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa Mkuu wa Idara ya Komputer na Idara ya Hesabati na Sayansi ya jamii ni wanawake .

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags