Waitara awataka wanafunzi kuwa wabunifu, kusoma kwa bidii

Waitara awataka wanafunzi kuwa wabunifu, kusoma kwa bidii

Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amewataka wanafunzi kuwa wabunifu na kusoma kwa bidii ili wanapomaliza masomo yao waweze kuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha.

Waitara ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 37 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo amesema maarifa na ujuzi utawawezesha wahitimu kujiajiri au kuajiriwa.

“Ubunifu utawawezesha kujiajiri au kuajiriwa hasa ukizingatia Uchumi wa Viwanda unahitaji nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi zaidi. Hivyo, rai yangu kwa wanafunzi wajitume katika masomo yao,” amesema.

Aidha amesema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, inafahamu vizuri changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu na majengo, uhaba wa ofisi za wahadhiri na uhaba wa nafasi za mabweni kwa wanafunzi.

“Serikali itaendelea kushirikiana na chuo katika kuhakikisha changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi. Aidha, ninauagiza Uongozi kuendelea kutumia mapato ya ndani katika kuendeleza na kuboresha miundombinu ya chuo,” amesema Waitara

Naye Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa na chuo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka hivyo kupelekea ongezeko la wataalam katika sekta ya uchukuzi.

“Katika kipindi cha miaka mitano idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa asilimia 67 kutoka 7,752 mwaka 2016/2017 hadi wanafunzi 12,980 mwaka 2021/2022,” amesema.

Hata hivyo amesema chuo hicho kina mikakati mbalimbali ya kutayarisha rasilimali Watu watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira kwenye sekta ya uchukuzi na usafirishaji hasa kwa kuzingatia utekelezaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi ambayo Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kuyafanya.

“Tuna mkakati wa kuanzisha na kuhuisha mitaala mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahadahadi shahada ya uzamili.Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia hii ikiwa ni ukarabati na ujenzi wa majengo mapya, ununuzi wa vifaa vya maabara na karakana,” amesema.

Amesema katika maandalizi ya mafunzo ya urubani, chuo kimepeleka wafanyakazi wanne nchini Afrika ya Kusini kusomea urubani na ukufunzi wa mafunzo ya urubani katika vyuo viwili ambapo wafanyakazi wawili wapo Blue Chip Flight School na wengine wawili wapo 43 Air school.

“Chuo kinaendelea na hatua ya nne kati ya hatua tano za kupata ithibati ya utoaji wa mafunzo ya urubani kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA). Hatua hiyo ni Demonstrationand Inspection inayoenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia ikiwemo ndege.

“Mara baada ya ndege kuwasili, Chuo kitakamilisha hatua hiyo ya nne na kumalizia hatua ya tano (Certification Phase) na hivyo kupata ithibati na kuanza mafunzo,” amesema

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo hicho, Profesa Blasius Nyichomba amesema baraza hilo la uongozi limefanikiwa kusimamia uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kufundishia nakujifunzia, uboreshaji wa mafunzo yanayotolewa na chuo, pamoja na kuimarisha rasilimali watu ya chuo.

“Usimamizi huu unalenga kukiwezesha chuo kufikia malengo ya uanzishwaji wake, ili kuchochea maendeleo ya Taifa ya uchumi kama yalivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025,” amesema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags