Vaa pigo hizi zitakufanya utoke chicha

Vaa pigo hizi zitakufanya utoke chicha

Baadhi ya wanawake na wanaume wengi wanapenda kupendeza, ndiyo sababu hujitahidi kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kutunza ngozi zao, nywele na kuvaa mapambo na mavazi ya kuvutia ili waweze kupendeza.

Moja kati ya vitu ambavyo wanawake hupendelea katika muonekano wa mwanaume ni utanashati ambao hutengenezwa kwa kuvaa nguo safi, kwa mpangilio mzuri.
Akizungumza na Mwananchi Scoop Hamza Masoud amesema kuwa anazingatia mahala anapokwenda anapochagua mavazi ya kuvaa.

"Ninavyovaa ninapokwenda kazini ni tofauti na vile nitakavyovaa ninapotoka katika mitoko ya wikiendi hivyo mahala ninapokwenda ndipo kutanifanya niamue navaa nini,"anasema.

Hajra Mussa mkazi wa Kiwalani jiji Dar es Salaam amesema anavutiwa anapotoka kwenda matembezi na mume wake avae t-shirt na jeans pamoja na raba miguuni.
Yusuph Yasri ambaye ni muuzaji wa nguo za kiume jijini Dar es Salaam anasema mavazi ya wanaume yanayowavutia wanawake wengi na hupendelea wapenzi au waume zao kuvaa ni pamoja na t-shirt na jeans.

Amesema kama mwanaume atapangilia vazi vizuri kwa kuzingatia rangi basi muonekano wake utakuwa wa kuvutia na nadhifu muda wote.

"Lakini pia mwanaume anaweza kuvaa suruali yake ya jeans na shati ambalo anaweza kulivaa lenyewe au akatupia na koti huku chini akiwa amevaa raba au kiatu cha aina nyingine official,"anasema.

Yasri anasema kuwa kama siku za ‘wikiend’ mwanaume anataka kutoka kwenda sehemu za starehe au ametulia nyumbani na familia anaweza akavaa t-shirt na short na akapendeza.

"Siyo kwa sababu unashinda nyumbani ndiyo uvae hovyo unaweza kupata mgeni wa ghafla ukaumbuka, "amedokeza Yasri.

Amesema kuwa vazi jingine ambalo huwavutia wanawake wengi kwa wanaume ni suti.

"Mwanaume anapotaka kushona au kununua suti ili apate muonekano wa kuvutia ni vyema kuzingatia rangi ya ngozi yake mfano mwanaume mwenye ngozi nyeusi hapendezi kuvaa suti yenye rangi ya kuwaka,"anasema.
Ameongezea kuwa baadhi ya wanawake wanapenda kuona wanaume wamevaa mashati ya vitenge na suruali inayoendana na moja ya rangi iliyopo katika kitenge hicho.

"Vazi hili likipangiliwa vizuri mwanaume anapata muonekano wa kuvutia,"anasema

Amesema pamoja na nguo hizo kumpa muonekano wa kupendeza lakini ili kupata muonekano wa kuvutia zaidi anatakiwa kutosahau kuvaa accesories muhimu kwa mwanaume akitolea mfano saa.

Nae muuzaji wa viatu vya kiume Yusuph Abdallah alisema viatu kwa kiasi chake inabeba muonekano wa mwanaume na kumfanya aonekane mtanashati pale atakapovaa kulingana na nguo alizovaa.

"Mfano haipendezi kuvaa suruali ya kuchomekea na sendo au kuvaa suruali ya kitambaa na raba unapovaa nguo za ofisini unapaswa kuvaa kiatu cha ofisini kinachoendana na mavazi hayo na unapovaa tshirt na jeans hapo unaweza kuvaa na raba na ukapendeza,"amesema.

Pia ameongezea kuwa kuna vitu vingine ambavyo si vya lazima lakini husaidia kuongeza muonekano wa mwanaume ambavyo ni miwani, kofia pamoja na mikufu.

"Angalizo katika uvaaji wa miwani ni vyema kuvaa miwani inayoendana na kichwa chako pamoja na aina ya mavazi uliovaa kadhalika katika kofia siyo unavaa suti na kofia utaonekana mlugaluga"alimalizia kusema Yusuph.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags