Ustaa bongo ni mzigo wa maumivu

Ustaa bongo ni mzigo wa maumivu

Kama kuna kitu kigumu kwenye huu ulimwengu, basi ni kuishi katika dunia ya umaarufu, hasa unaokulazimu kuficha maumivu na uonyeshe nyakati za furaha pekee.

Huu ndiyo uhalisia wa maisha wanayoyaishi mastaa wengi wa sanaa mbalimbali nchini, ambao vifua vyao vimebeba siri nzito zenye maumivu ndani yake, lakini nyuso zao ni kama fresh tu.

Ni kwa sababu ya umaarufu huo wengine wamejikuta ‘wakifa na tai shingoni’ ili kulinda brand zao lakini ukweli wanaujua wenyewe juu ya magumu wanayopitia.

Lakini ukweli utabaki kuwa, kwa kuwa nao ni sehemu ya binadamu, mishale na mikuki ya maisha haiepukiki, hivyo nao wanayo magumu waliyoamua kuyaficha vifuani.

Katika dhana ya kulinda umaarufu, ndipo misimu kama kiki na mbinu nyingine za kuteka hisia ya jamii zilifanywa na baadhi ya mastaa, kulinda umaarufu wao.

Ugumu wa maisha ya ustaa, unamuibua mtayarishaji mkongwe wa muziki wa Bongoflava, Master Jay anayesema magumu zaidi yanawakabili wasanii wakike na kusababisha baadhi yao waachane na sanaa.

“Changamoto zipo na kweli wamekuwa wakipitia magumu lakini kwa wasanii wa kike, mara nyingi ugumu wao hutoka kwa wanaowasimamia. Anajikuta kimya kwa sababu anaogopa kumkosea anayemfanya aonekane kwenye sanaa,” anasema.

Kwa mujibu wa nguli huyo wa muziki, ukimya wa wasanii hao unatokana na hofu kuwa, wakiyaweka hadharani magumu waliyonayo watapoteza fursa.

“Mimi naamini hii ni changamoto kubwa na sio tu kwenye muziki hata kwa waigizaji ni suala litakalokuja kulipuka siku moja wasanii wa kike watajitokeza na kusema vitu wanavyofanyiwa,” anasema.

Katika maelezo yake, anarejea kilichowahi kutokea nchini Marekani, akifafanua hata Tanzania kitatokea.

Msanii wa Bongo movie, Abduli Hamadi Salum maarufu kama Ben, amesema kupitia sanaa watu wamepata fursa mbalimbali na kuaminiwa na jamii.

“Kiukweli sanaa yetu ilipofikia pazuri watu wamepata fusra nyingi na kuwa mabalozi kwenye maeneo mbalimbali hata zisizokuwa za sanaa,” anasema.

Pamoja na hayo Beni, anasema pamoja na mazuri yaliyopo kubaniana nafasi ni moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya sanaa, lakini wengine hawaaminiani.

“Bado kuna ile hali ya kubaguana, kubaniana na kutoaminiana hasa changamoto hiyo wanaipitia wasanii wa kiume katika upande wa uigizaji.

“Unakuta mtu anashindwa kumuamini mwanaume mwenzake, wakati mwingine ni wivu wa maendeleo kwa kuogopa kuzidiwa mafanikio,” anasema.

Mchekeshaji wa cheka tu, Tina Logat anasema japo wanafanya kazi na kupata pesa, changamoto katika maisha ya umaarufu ni nyingi.

“Changamoto zipo lakini kuna baadhi ya watu hatutaki kuziweka wazi kutokana na kulinda utu wetu. Mimi nipo black and White bosi akinihitaji basi tufanye kazi kweli na sio mambo mengine kwa sababu inaumiza kuona tunadhalilika wakati mwingine, kupita mabosi zetu,” anasema.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags